Jumanne, 23 Juni 2026

MAHAKAMA IENDANE NA KASI YA KUKUA KWA UCHUMI: JAJI KIONGOZI

  • Ataka huduma kutolewa kwa haraka

Na FAUSTINE KAPAMA na Noel Daud-Mahakama, Songea

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, amewahimiza Watumishi wa Mahakama ya Tanzania kwenda na kasi ya maendelea na kukua kwa shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini.

Mhe. Dkt. Siyani ametoa wito huo leo tarehe 23 Juni, 2026 mjini Mbinga, alipokuwa anazungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Mbinga katika siku ya pili ya ziara yake ya kimahakama, kukagua Mahakama na Magereza mkoani Ruvuma.

“Shughuli za kiuchumi zinapokuwa kubwa kama kwenye Mji wa Mbinga, mashauri kama ya mirathi, ardhi ambayo ni mengi, shughuli za kibiashara na mikataba, yatakuja mahakamani. Mahakama lazima iendane na kasi hiyo ya kukua kwa uchumi,” amesema.

Amewaambia Watumishi hao kuwa ili kuendana na kasi ya maendeleo ambayo Wananchi wanajifanyia na Serikali inawezesha, kuna mambo ambayo uongozi wa Mahakama unaweza kufanya kama kuboresha maslahi na miundombinu, hivyo wao kama watoa huduma hawatakiwi kuachwa nyuma.

“Kwa hiyo, ni waombe inapowezekana, sisi tutagulie. Siyo tu tuende na kasi ya kukua kwa uchumi na shughuli za watu, ikiwezekana sisi tutangulie mbele, tusiwe tunafukuza maendeleo,” Jaji Kiongozi amesema.

Amesisitiza kuwa Mahakama inatakiwa kuwa kinara wa kuonesha njia, ili watu wakifika mahakamani waone, pamoja na uchakavu wa miundombinu iliyopo, wasiwakute Watumishi wakiwa wanyonge, bali wapate huduma na waondoke wakiwa wameridhika.

“Huduma zitolewe haraka, mashauri yasichukue muda mrefu mahakamani, kwa kadri inanyowezekana tutoe haki mapema na tuweke mazingira ya kuwa na wepesi wa kupatikana huduma zenyewe,” Mhe. Dkt. Siyani amesema.

Aidha, Jaji Kiongozi amewataka Watumishi wa Mahakama kutokuwa kikwazo kwa watu kuja mahakamani na pia wanapaswa kujiuliza ni kwa namna gani kila mmoja anapokea Wananchi wanaokuja mahakamani na jinsi gani anavyotoa huduma bila kuwa na upendeleo.

Amebainisha kuwa Watumishi wa Mahakama wanapaswa kutambua kuwa wao ni sehemu ya Mahakama, kwani wakitoa huduma vizuri Mahakama na wao binafsi watapata sifa, tofauti na hivyo Mahakama itachafuka.

“Kila Mtumishi anatakiwa kujua kuwa anao mchango anaopaswa kuutoa ili kuboresha huduma za Mahakama na hivyo kujenga imani ya umma kwa Mahakama. Msipofanya hivyo, watu hawatawaheshimu na Mahakama haitapewa hadhi inayostahiki,” amesisitiza.

Akizungumzia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Jaji Kiongozi amewaeleza Watumishi hao kuwa pamoja na ugumu wa miundombinu na mazingira yaliyopo, Mahakama haiwezi kurudi nyuma.

Mhe. Dkt. Siyani amewapongeza Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Mbinga kwa kazi nzuri wanaoifanya, kwani taarifa ya utendaji iliyowasilishwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Lome Mwapemela, imeonesha kutokuwa na mlundikano wa mashauri na Wananchi wa Mbinga wanaendelea kupata huduma za haki.

Kwenye taarifa yake, Mhe. Mwapemela ameeleza kuwa mashauri yaliyobaki Desemba, 2025 katika ngazi ya Mahakama ya Wilaya yalikuwa 30, yaliyofunguliwa kati ya Januari 2026 hadi Juni 19, 2026, yalikuwa 77 na yaliyoamuriwa kwa kipindi hicho ni 84.

Kwa mujibu wa taaarifa hiyo, hapakuwepo na mashauri yaliyovuka mwaka 2025 katika ngazi ya Mahakama za Mwanzo na mashauri yaliyofunguliwa kati ya Januari na Juni 19, 2026 yalikuwa 425 na yaliyoamuriwa ni 376.

Hakimu Mfawidhi ameeleza pia kuwa, kwa kipindi cha Januari hadi Juni 19, 2026, mashauri ya mirathi sita yamefungwa kati ya mashauri 14 ambayo uteuzi wa msimamizi wa mirathi umefanyika. Amebanisha kuwa kati ya mashauri hayo, mawili ni ya Mahakama za Mwanzo na mashauri nne ni Mahakama ya Wilaya.

“Mashauri ambayo hayajafungwa bado Wasimamizi wapo ndani ya muda wa kutekeleza majukumu yao. Tumekuwa tukichukua namba za simu za Msimamizi wa Mirathi na za watu wao wa karibu ili kuhakikisha wanapatikana baada ya kuteuliwa,” ameeleza.

Katika siku hiyo ya pili ya ziara yake, Jaji Kiongozi pia ametembelea Magereza mawili ya Mkwaya na Kitai, yote yakiwa katika Wilaya ya Mbinga. Akiwa kwenye Magereza hayo, Jaji Kiongozi amepokea changamoto mbalimbali za Wafungwa, ambazo amezipatia ufunguzi papo kwa papo.

Aidha, Jaji Kiongozi ametumia fursa hiyo kuwaomba Wafungwa watakaobahatika kutoka wawe raia wema, kwani kukaa kwao gerezni hakuna faida kwa nchi.

Katika ziara hiyo, Jaji Kiongozi ameambatana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Songea, Mhe. James Karayemaha, Jaji wa Mahakama Kuu Songea, Mhe. Emmanuel Kawishe, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa na Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu Songea, Mhe. Elizabeth Nyembele na Mhe. Asha Waziri.

Wengine ni Mtendaji wa Mahakama Songea, Bw. Allan Mwela, Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya ya Nyasa na Mbinga Songea na Watumishi wengine wa Mahakama Songea.

Kesho tarehe 24 Juni, 2026, Jaji kiongozi anatarajia kuendelea na ziara yake kwa kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, na baadaye kufanya ukaguzi katika Gereza Kuu Songea na kisha kutembelea Mahakama Kuu Songea na kuongea na Watumishi.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Mbinga (hawapo kwenye picha.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mbinga, Mhe. Lome Mwapemela, akiwasilisha taarifa ya utendaji wakati wa kikao hicho.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Songea, Mhe. Elizabeth Nyembele, akitoa utambulisho wa Viongozi mbalimbali wakati wa kikao hicho. 

Sehemu ya Viongozi wa Mahakama kutoka Makao Makuu Dodoma (juu) na Viongozi kutoka Mahakama Kuu Songea (picha chini) wakiwa kwenye kikao hicho.


Sehemu ya Watumishi wa Mahakama (juu na chini) ikifuatilia kilichokuwa kinajiri.


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, akiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya Viongozi. Picha chini ni sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Mbinga.


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, akiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu nyingine ya Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Mbinga (juu na chini).


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, akipokea salamu baada ya kuwasili kwenye Gereza la Kilimo Kitai. Picha chini ni sehemu ya Maofisa Magereza, Wadau na Watumishi baaada ya ukaguzi wa Gereza hilo kufanyika.



Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, akiwasili kwenye Gereza la Mkwaya kufanya ukaguzi na kuzungumza na Wafungwa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni