Jumatano, 24 Juni 2026

CHAMA CHA MAJAJI NA MAHAKIMU MKOANI SONGWE CHAKUTANA

Na. ELIUD KIWANGA – Mahakama, Songwe

Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (TMJA) Mkoa Songwe wamefanya kikao cha kutathmini utendaji kazi pamoja na kukuza malezi ya kitaaluma, kubadilishana uzoefu na kuwakaribisha wananchama wapya, kikao kazi hicho kilifanyika katika ukumbi wa Simple Palace uliopo mji wa Vwawa wilayani Mbozi.

Katika kikao hicho, Mwenyekiti wa TMJA Mkoa wa Songwe Mhe. Magreth Kannonyele alimkaribisha Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Gabriel Pascal Malata ambaye alitambulishwa kama mlezi wa Chama cha TMJA Mkoa wa Songwe kwani Katiba ya TMJA inamtambua Jaji Mfawidhi kama mlezi wa matawi yote yaliyo chini ya Masjala husika.

Sambamba na hilo, Mwenyekiti huyo alimkaribisha Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Abubakar Mrisha, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Joyce Minde pamoja na wanachama wengine wapya TMJA Mkoa wa Songwe.

Akiwasilisha taarifa ya Chama ya mwaka 2025/2026 Naibu Katibu wa TMJA Mkoa wa Songwe Mhe. Ian Mnyigumba alisema Chama kilifanikiwa kufanya safari za kitalii katika maporomoko ya Kalambo Mkoa wa Rukwa na Beach ya Kasanga na baada ya safari hizo walifanikiwa kuchagua viongozi wa TMJA Mkoa wa Songwe.

Aidha, Chama kilifanikiwa kutoa elimu kwa shule za Msingi na Sekondari zikiwemo, Shule ya Msingi Nungwi iliyopo Wilaya ya Mbozi na Shule ya Sekondari Tunduma iliyopo Halmashauri ya Mji wa Tunduma.

Vilevile, wanachama wa TMJA Mkoa Songwe walishiriki kutoa Elimu ya usuluhishi wakati wa wiki ya suluhishi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Songwe.

Mnamo Juni, 2025 TMJA Mkoa wa Songwe walishiriki mafunzo ya utafiti wa Sheria “Legal Research” chini ya aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Joachim Charles Tiganga, sambamba na hayo wanachama walifanikiwa kufanya bonanza la michezo mbali mbali ikiwemo drafti na karata.

Vilevile, Chama cha TMJA Mkoa wa Songwe kilifanya matendo ya huruma ikiwa ni pamoja na kutembelea Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tunduma na kutoa misaada mbali mbali kwa wagonjwa, Pia waliweza kutoa misaada kwa mahabusu na wafungwa katika baadhi ya magereza yaliyopo Mkoa wa Songwe.

Kuhusu ada ya uanachama Naibu Katibu Mhe. Ian Mnyigumba alisema kuwa, michango hiyo hutumika kuendesha Chama cha TMJA Mkoa wa Songwe ikiwa ni pamoja na kufarijiana pale mwanachama anapougua, anapofiwa, anapouguliwa na kupongezana katika nyakati za furaha, aliendelea kusema kuwa ada ya uanachama hutumika pia kama mtaji wa kuendesha miradi mbalimbali ya Chama kama vile kutengeneza T-shirt, Kofia na Vikombe.

Mhe. Mnyigumba alisisitiza kuwa, wateja wakubwa wa miradi hiyo yote ni wanachama wa TJMA Mkoa wa Songwe, pia alihimiza wanachama kuendelea kununua bidhaa zinazotokana na miradi hiyo ili kukuza mfuko wa chama hicho.

Aidha, kuhusu idadi ya wanachama Mhe. Mnyigumba alisema kuwa, TMJA Mkoa wa Songwe ina jumla ya wanachama 32 wakiwemo Majaji wawili, Naibu Msajili na Mahakimu wa ngazi mbali mbali.

Katibu wa chama TMJA Songwe alimuomba mlezi wa chama hicho awasaidie katika kuhimiza wanachama kulipa ada zao kwa wakati kwasababu ada ya uanachama ndio mapato pekee na pia ni mtaji wa kuendesha miradi mbalimbali ya Chama.

Akielezea kuhusu mafanikio ya ubunifu wa miradi wa chama cha TMJA Mkoa wa Songwe walifanikiwa kupata tuzo ya ubunifu bora wa miradi kutoka TJMA Taifa kwenye mkutano uliofanyika Dodoma mwezi Junuari, 2025.

Akiwasilisha taarifa ya fedha na miradi mweka hazina wa chama TMJA Mkoa wa Songwe Mhe. Martha Malima alisema kuwa, ada za uanachama ziliwezesha miradi ya T-shirt, Kofia, Vikombe na Badge vyote vikiwa na nembo za TMJA.

Mhazini wa Chama alisoma gharama na faida walizozipata kutokana na  miradi hiyo, pia alitaja bidhaa zilizosalia na wanachama kwa pamoja walikubaliana kuzitoa baadhi ya bidhaa kama zawadi kwa mlezi wa Chama ambaye ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Songwe, Mhe. Gabriel Pascal Malata, Jaji wa Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Songwe Mhe. Abubakar Mrisha na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Songwe Mhe. Joyce Minde.

Mhe. Martha Malima mhazini wa Chama TMJA Mkoa wa Songwe alikabidhi tuzo ya ubunifu bora wa miradi waliyoipata mwezi Januari, 2025 kwa mlezi wa chama TMJA Songwe.

Kwa upande mwingine wanachama wa TMJA Mkoa wa Songwe kupitia kikao hicho waliridhia kufanya marekebisho ya katiba kutokana na mapungufu waliyoyabaini kwenye katiba iliyopo. Wanachama walimchagua Mhe. Raymond Kaswaga kama mjumbe wa kamati ya maboresho ya katiba ya chama cha TMJA Mkoa wa Songwe na kila Wilaya ilichagua mjumbe mmoja ili kukusanya maoni ya katiba mpya.

Wajumbe kwa pamoja walikubaliana kuwa, mapendekezo hayo yatawasilishwa meza kuu mwezi Agosti 2026, wajumbe wataamua kama wameyakubali mabadiliko hayo ili mabadiliko ya katiba yaweze kwenda sanjari na hali ya sasa.

Mwenyekiti wa TMJA Mhe. Magreth Kannonyele na Mhe. Abubakar Mrisha aliwashauri wajumbe waliochaguliwa kuisoma vyema na kuielewa vizuri katiba iliyopo kabla ya kuanza zoezi la ukusanyaji wa maoni.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Songwe Mhe. Gabriel Malata alitoa elimu kuhusu Applicability of Electronic Evidence in Primary Court, aliwasisitiza wanachama wa TMJA Mkoa wa Songwe kuendana na teknolojia kwasababu Mahakama Kuu ya Tanzania imeruhusu electronic evidence kutumika mahakamani, ambapo kwa mara ya kwanza Commercial Court ilikubali matumizi ya electronic evidence na sasa imeruhusiwa pia kutumika katika Mahakama za Mwanzo.

“Sisi kama kama Mahakimu na Majaji tunalazimika kusoma na kuielewa vilivyo sheria ya kimtandao Electronic Transaction Act ya 2015 ili itusaidie katika kufanya maamuzi sahihi ya mashauri ya aina hiyo,” alisisitiza Mhe. Malata.

Mhe. Malata aliwashauri wanachama wa TMJA Mkoa wa Songwe watambue kuwa, kwa sasa Songwe imepewa mamlaka kamili hivyo ni wajibu wa kila mmoja kutimiza majukumu yake ipasavyo.

Kwa upande wa Chama, Mhe. Malata alisisitiza kuwa, kila mwanachama ana wajibu wa kutekeleza majukumu ya chama ikiwa ni pamoja na kulipa ada za uanachama kwa wakati, kushiriki kikamilifu shughuli zote za chama na kununua bidhaa za chama ili kuboresha mfuko wa chama.

Wanachama wa TMJA Mkoa wa Songwe, Mwenyekiti wa TMJA Mkoa wa Songwe Mhe. Magreth Kanonyele (katikati), Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Gabriel Malata (wa pili kushoto), Jaji wa Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Abubakar Mrisha ( wa pili kulia) wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kikao hicho.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Gabriel Malata (kushoto) na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Abubakar Mrisha wakiteta jambo wakiwa kwenye kikao cha TMJA Mkoa wa Songwe.


Mwenyekiti wa TMJA Mkoa wa Songwe Mhe. Magreth Kannonyele (kushoto) mara baada ya kukabidhi tuzo ya ubunifu bora wa miradi kwa mlezi wa TMJA Mkoa wa Songwe ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Gabriel Malata.

Sehemu ya wanachama waliohudhuria kikao cha TMJA Mkoa wa Songwe.

Mwenyekiti wa TMJA Mkoa wa Songwe Mhe. Magreth Kannonyele akipeana mkono  na Jaji wa Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Abubakar Mrisha wakati wa kumkabidhi zawadi.

Mwenyekiti wa TMJA Mkoa wa Songwe Mhe. Magreth Kannonyele (kushoto) akimkabidhi zawadi Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Joyce Minde (kulia).

Mwenyekiti wa TMJA Mkoa wa Songwe Mhe. Magreth Kannonyele (aliyesimama) akifafanua jambo kwenye kikao cha TMJA Mkoa wa Songwe.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe Mhe. Francis Kishenyi akiwa katika kikao cha TMJA Mkoa wa Songwe akifuatilia mawasilisho. 


Viongozi wa TMJA Mkoa wa Songwe wakiongozwa na Mwenyekiti Mhe. Magreth Kannonyele (wa pili kushoto), Makamu Mwenyekiti Mhe. Machumu G. Pamba (katikati), Mhazini wa Chama Mhe. Martha Malima (wa pili kulia), Mwakilishi TMJA Taifa Mhe. Linah Okello (wa kwanza kulia), na Kaimu Katibu wa chama Mhe. Ian Mnyigumba (wa kwanza kushoto)wakiwa kwenye kikao cha TMJA Mkoa wa Songwe.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni