Jumatano, 24 Juni 2026

JAJI MKUU AMUAPISHA HAKIMU MKAZI MPYA WA MAHAKAMA YA MWANZO

Na MARY GWERA & HALIMA MNETE, Mahakama-Dodoma

·       Jaji Mruma ampa Wasia Hakimu huyo kutoa maamuzi yanayozingatia Mila na Desturi za Jamii husika

·       Naye Jaji Tiganga amtaka kutoa haki kwa kuzingatia misingi ya Katiba, Sheria za Nchi

Katika jitihada za kuendelea kuimarisha utoaji haki nchini kupitia kuongezwa kwa watumishi wenye weledi na uadilifu, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 24 Juni, 2026 amemuapisha Mhe. Rose Baltazar Ngero kuwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo.

Uapisho huo umefanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jaji Mkuu, Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, katika hafla iliyobeba uzito wa kiutumishi na kisheria, ikionesha dhamira ya Mahakama ya Tanzania ya kuendelea kuimarisha Mhimili wa utoaji haki kuanzia ngazi za chini kabisa zinazogusa wananchi moja kwa moja.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali Waandamizi wa Mahakama akiwemo Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga, baadhi ya Naibu Wasajili, watendaji pamoja na watumishi wengine wa Mahakama.

Akitoa wasia kwa Hakimu huyo mpya mara baada ya uapisho, Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma amemsisitiza juu ya umuhimu wa kuzingatia sheria sambamba na mila na desturi za jamii husika katika utekelezaji wa majukumu ya kimahakama.

“Katika kiapo chako umeahidi kusimamia sheria, mila na desturi. Ni muhimu kuelewa kwamba mashauri mengi katika Mahakama ya Mwanzo yanahusu maisha halisi ya jamii, hivyo uelewe mazingira na desturi za watu unaowaamria,” amesema Mhe. Mruma.

Jaji Mruma amesema mashauri mengi yanayofikishwa katika Mahakama za Mwanzo huhusisha masuala ya kijamii kama mirathi, talaka na migogoro ya kifamilia ambayo mara nyingi huongozwa na mila na desturi za jamii husika, hivyo ni muhimu kwa Hakimu kuwa na uelewa mpana wa mazingira anayofanyia kazi ili kutoa uamuzi wenye haki na unaokubalika kijamii.

Mhe. Mruma amebainisha kuwa, uwezo wa Hakimu kuelewa na kutafsiri Sheria za Kimila kwa usahihi unaweza kusaidia Mahakama kutoa maamuzi yanayozingatia haki huku yakibaki karibu na uhalisia wa jamii, jambo linaloongeza imani ya wananchi kwa mhimili wa Mahakama.

“Wakati mwingine suluhisho la mgogoro haliishii kwenye vifungu vya sheria pekee, bali linahitaji pia uelewa wa historia, utamaduni na namna jamii husika inavyoendesha maisha yake. Hapo ndipo busara ya hakimu inapokuwa muhimu,” amesisitiza.

Aidha, Mhe. Mruma amemtaka Hakimu huyo kuzingatia maadili ya kazi na kulinda heshima ya taaluma ya sheria.

“Jiepushe na mazingira au mienendo inayoweza kushusha hadhi ya kazi yako. Uadilifu wako binafsi ndio msingi wa wananchi kuendelea kuiamini Mahakama,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga, amesema kazi ya utoaji haki ni dhamana kubwa inayopaswa kutekelezwa kwa kuzingatia misingi ya Katiba, Sheria za Nchi pamoja na maadili ya Viongozi wa Mahakama.

Amesema, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka wazi mamlaka ya Mahakama kama Mhimili huru wenye jukumu la kutafsiri sheria na kusimamia utoaji haki kwa usawa kwa wananchi wote.

“Kazi ya uamuzi si kazi ya kawaida; ni kazi inayogusa maisha ya watu moja kwa moja. Katiba imeweka mamlaka huru ya Mahakama kutafsiri sheria, hivyo kila uamuzi unaofanya unapaswa kuzingatia haki, sheria na maslahi mapana ya taifa,” amesema Mhe. Tiganga.

Mhe. Tiganga ameongeza kuwa, pamoja na kuongozwa na sheria, mtumishi wa Mahakama anapaswa kuwa na uadilifu, hofu ya Mungu na kujiepusha na tamaa zinazoweza kuathiri utoaji haki.

“Hii ni kazi ya Kimungu. Fedha isikuharibu wala tamaa isikupoteze, unapaswa kuwa na hofu ya Mungu kwa sababu wakati mwingine maamuzi yako yanaweza kubadili maisha ya mtu milele,” amesema.

Sambamba na hilo, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano, nidhamu ya kiutumishi na kuheshimu mamlaka ndani ya Taasisi ya Mahakama, huku akibainisha kuwa, hata wale walio na umri mdogo lakini wakabeba dhamana za kiuongozi wanastahili kupewa heshima inayostahili.

“Mahakama inajengwa kwa ushirikiano. Waheshimu wenzako, shirikiana nao na jifunze kila siku. Maarifa yapo mengi, hata kupitia Katiba, miongozo na hotuba mbalimbali zinazopatikana katika tovuti za Mahakama,” amesisitiza.

Uapisho wa Mhe. Rose Baltazar Ngero unaongeza nguvu katika jitihada zinazoendelea za Mahakama ya Tanzania za kujenga mfumo wa utoaji haki ulio karibu zaidi na wananchi, wenye ufanisi, unaozingatia maadili na unaoendelea kujenga imani ya umma kwa mhimili wa Mahakama. Kupitia watumishi wenye weledi, uadilifu na utayari wa kulitumikia taifa, Mahakama inaendelea kutekeleza wajibu wake wa msingi wa kusimamia haki na kulinda utawala wa sheria nchini.

Dhamira ya Mahakama ya Tanzania ni kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma za kimahakama mapema ipasavyo, kwa weledi na kwa kuzingatia misingi ya sheria, haki na usawa. Mahakama za Mwanzo zina nafasi muhimu katika mfumo wa utoaji haki nchini kwa kuwa ndizo ngazi za mwanzo zinazopokea na kusikiliza mashauri mengi yanayohusu maisha ya kila siku ya wananchi, hususan migogoro ya kifamilia, ardhi, mirathi na masuala mengine ya kijamii.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akimuapisha Mhe. Rose Baltazar Ngero kuwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo leo tarehe 24 Juni, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


Mhe. Rose Baltazar Ngero akila kiapo mbele ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo leo tarehe 24 Juni, 2026 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Mhe. Rose Baltazar Ngero akisaini hati ya kiapo mara baada ya kuapa kuwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo leo tarehe 24 Juni, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Viongozi mbalimbali wa Mahakama walioshiriki hafla fupi ya uapisho wa Hakimu Mkazi mpya wa Mahakama ya Mwanzo, Mhe. Rose Baltazar Ngero aliyeapishwa leo na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza jambo baada ya kumuapisha Mhe. Rose Baltazar Ngero kuwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo leo tarehe 24 Juni, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma akitoa wasia kwa Mhe. Rose Baltazar Ngero, Hakimu Mkazi mpya wa Mahakama ya Mwanzo aliyeapishwa leo tarehe 24 Juni, 2026 na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga akitoa neno kwa Mhe. Rose Baltazar Ngero, Hakimu Mkazi mpya wa Mahakama ya Mwanzo aliyeapishwa leo tarehe 24 Juni, 2026 na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju.

Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na Hakimu Mkazi mpya wa Mahakama ya Mwanzo, Mhe. Rose Baltazar Ngero (aliyesimama) aliyeapishwa leo tarehe 24 Juni, 2026 na Jaji Mkuu. Kushoto ni Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma na kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga.


Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi wa Mahakama walioshiriki katika hafla ya uapisho wa Hakimu Mkazi mpya aliyeapishwa leo tarehe 24 Juni, 2026 na Jaji Mkuu. Kushoto ni Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma na kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga.

Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Naibu Wasajili wa Mahakama walioshiriki katika hafla ya uapisho wa Hakimu Mkazi mpya aliyeapishwa leo tarehe 24 Juni, 2026 na Jaji Mkuu. Kushoto ni Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma na kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)











 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni