Jumatano, 24 Juni 2026

JAJI MUGETA AKABIDHI OFISI RASMI KWA JAJI DKT. MAMBI

Na. Christopher Msagati – Mahakama, Manyara

Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Manyara, Mhe. Ilvin C. Mugeta amekabidhi ofisi kwa Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara, Mhe. Dkt. Adam Mambi leo tarehe 24 Juni, 2026 ikiwa ni baada ya Mhe. Mugeta kuhamishwa kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Tabora.

Mhe. Dkt. Mambi ambaye kabla ya kuja Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara, alikuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Tabora. Katika hafla ya makabidhiano, Majaji hao walipata wasaa wa kuzungumza na watumishi pamoja na wadau wa Mahakama, ambapo Mhe. Mugeta alitumia nafasi hiyo kuagana na wanamanyara, huku Mhe. Dkt Mambi akitumia wasaa huo kujitambulisha na kuwatambua watumishi wa Mahakama katika Masjala hiyo.

Akitoa shukrani wakati wa kuagana na watumishi Mhe. Mugeta alisema kuwa, ushirikiano alioupata toka Masjala Ndogo ya Manyara usiishie hapo mara baada ya kuondoka kwake bali uendelee kwa Kiongozi huyo mpya na hata Viongozi wengine watakaoendelea kuja kwenye Masjala hiyo.

“Leo ni siku yangu ya pekee ambayo imechanganyikana na hisia za furaha pamoja na huzuni, nalazimika kuagana na watumishi niliokuwa nao tangu mwaka 2025 nilipohamia Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara nikitokea Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Arusha, watumishi hawa wamenipa heshima kubwa sana…

 …Viongozi hawawezi kufanya kazi peke yao isipokuwa kwa ushirikiano na umoja wetu. Mhe Jaji Mambi, ninakuachia watumishi hodari ambao wana moyo wa kufanya kazi kwa bidii pasipo kushurutishwa au kusimamiwa kwa nguvu,” alisema Mhe. Mugeta.

Naye, Mhe. Dkt. Mambi alipokea kwa mikono miwili ukaribisho aliyoupata kwa watumishi wa Masjala hiyo, huku akisisitiza kuwa ofisi yake ipo wazi kwa yeyote mwenye mawazo ya kuboresha. Alisisitiza kuwa yeye ni mtu wa kazi na anavutiwa zaidi na wachapa kazi.

“Nashukuru kwa uongozi wa Mahakama kwa kuona kuwa mimi naweza kuendeleza kazi njema ambayo ameifanya Mhe Jaji Mugeta katika Masjala hii ya Manyara, kasi ya utendaji kazi iliyokuwepo naamini tutaiendeleza na kushirikiana vema ili tuweze kuwahudumia wananchi kwa namna ambayo inastahili,” alisema Mhe. Dkt. Mambi.

Katika hafla hiyo, watumishi wa Kada mbalimbali waliweza kutoa maneno ya kumkaribisha na kumpokea Mhe. Dkt. Mambi anayehamia Manyara na pia kumuaga Mhe. Mugeta.

Miongoni mwao alikuwa ni Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Thobias Kavishe John alisema kuwa, wataendelea kutoa ushirikiano kwa Mhe. Dkt. Mambi ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa. Pia Mhe. John alimtakia majukumu mema Mhe. Mugeta katika majukumu yake mapya anayokwenda kuyaanza katika Kituo chake Kipya cha Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Tabora.

Naye, Msaidizi wa Hesabu wa Mahakama ya Wilaya ya Babati Bw. Sixbert Hongoli aliahidi kuendeleza ushirikiano kutoka kwa watumishi wa Kada nyingine ambao wote kwa ujumla wao wameonesha nia na utayari wa kuyapokea maelekezo toka kwa Kiongozi huyo mgeni aliyeripoti Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara.

Kwa namna ya pekee wanamanyara watamkumbuka Mhe. Mugeta kwa kuwa ndiye Jaji Mfawidhi wa pili tangu kuanzishwa kwa huduma za Mahakama Kuu katika Masjala Ndogo ya Manyara mnamo Mwezi Novemba mwaka 2022.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara anayehamia Mahakama Kuu Tabora Mhe. Ilvin Mugeta (kulia) na Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara Mhe Jaji Dkt. Adam Mambi wakiwa katika tukio la kupeana hati ya makabidhiano ya Ofisi ya Ufawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara.

Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi akitoa neno la shukrani kwa watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara kwa mapokezi waliyompatia mara baada ya kuwasili kituoni hapo. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara anayehamia Masjala Ndogo ya Tabora Mhe. Ilvin Mugeta akitoa neno la shukrani kwa watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara kwa kumuuga vizuri.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara anayehamia Masjala Ndogo ya Tabora Mhe. Ilvin Mugeta (kulia) na Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi (katikati) wakionesha hati za makabidhiano kwa watumishi waliofika kushuhudia tukio hilo.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara Bi. Nyanzobe Hemedi akimkabidhi Zawadi ya ua Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara anayehamia Masjala Ndogo ya Tabora, Mhe. Ilvin Mugeta ikiwa ni Ishara ya kumuaga kutoka kwa watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara.

Watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara wakiendelea na zoezi la kujitambulisha wakati wa zoezi la Makabidhiano ya Ofisi kati ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara anayeondoka Mhe. Ilvin Mugeta na Jaji Mfawidhi mpya Mhe Dkt Adam Mambi.

Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi akisaini vitabu vya wageni katika Ofisi yake mpya mara baada ya kuripoti kituoni hapo.


Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi akisalimiana na baadhi ya watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara mara baada ya kuripoti kituoni hapo.

Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Manyara Mhe. Dkt. Adam Mambi akipokea Zawadi ya ua ikiwa ni Ishara ya Ukaribisho kutoka kwa Watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Manyara.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni