- Kukagua Mahakama, Magereza
- Kuteta na Mkuu wa Mkoa, kuzungumza na Watumishi
Na FAUSTINE KAPAMA na Noel Daud-Mahakama, Songea
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed
Siyani, amewasili mkoani Ruvuma leo tarehe 21 Juni, 2026, kufanya ziara ya
kimahakama ya siku tano, kukagua Mahakama na Magereza.
Mhe. Dkt. Siyani amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Songea majira ya
saa 5.00 asubuhi akiwa ameambatana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Masjala Ndogo Songea, Mhe. James Karayemaha, na kupokelewa na Viongozi
wa Mahakama.
Viongozi waliokuwa Uwanja wa Ndege kumpokea Jaji Kiongozi ni Jaji wa
Mahakama Kuu Songea, Mhe. Dkt. Emmanuel Kawishe, Msajili wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa, Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu Songea, Mhe.
Elizabeth Nyembele na Mhe. Asha Waziri.
Wengine ni Mtendaji wa Mahakama Songea, Bw. Allan Mwela, Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Songea, Mhe. Lilian Rugarabamu, Mahakimu na
Watumishi wengine wa Mahakama Songea.
Ratiba iliyotolewa mjini hapa inaonesha kuwa JaJi Kiongozi ataanza ziara
yake kwa kutembelea Mahakama ya Wilaya Nyasa na kufanya kikao na Watumishi,
kabla ya kuelekea Wilaya ya Mbinga na kuongea na Watumishi na kukagua Gereza la
Wilaya ya Mbinga.
Kesho yake, kwa mujibu wa ratiba hiyo, Mhe. Dkt. Siyani ataelekea kwenye
Gereza la Mkwaya kufanya ukaguzi na baadaye kugagua Gereza lingine la Kitai,
yote yakiwa katika Wilaya ya Mbinga.
Siku ya tatu, Jaji Kiongozi atamtembelea Mkuu wa Mkoa, Mhe. Brigedia
Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, na kufanya naye mazungumzo mafupi na baadaye
kufanya ukaguzi katika Gereza Kuu Songea.
Siku hiyo hiyo, Mhe. Dkt. Siyani atatembelea Mahakama Kuu Songea na
kufanya mazungumzo mafupi na Jaji Mfawidhi na kisha kuongea na Watumishi wa
Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama ya Wilaya pamoja na Mahakama
zote za Mwanzo Songea mjini.
Siku ya nne, Jaji Kiongozi atatemebelea Mahakama ya Wilaya Namtumbo na
kuzungumza na Watumishi na kisha kuelekea Wilaya ya Tunduru kufanya ukaguzi
kwenye Gereza la Tundura, kabla ya kufanya kikao na Watumishi wa Mahakama ya
Wilaya Tunduru na Mahakama za Mwanzo katika Wilaya hiyo.
Siku ya tano, Mhe. Dkt. Siyani atafanya kikao cha majumuisho ya ziara
katika Mahakama ya Wilaya Tunduru, kikihusisha Watumishi wote kutoka maeneo
tofauti mkoani Ruvuma.








Hakuna maoni:
Chapisha Maoni