Na MICHAEL RITTE, Mahakama-Bukoba
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba, Mhe. David Nyanguye amewasihi
watumishi wa Masjala hiyo kuhakikisha kazi za usikilizwaji wa mashauri
zinaendeshwa vema pasipo kukwama na jukumu hilo liambatane na juhudi katika
utendaji wa majukumu ya kila siku kwa kuzingatia Maadili na kanuni za nafasi
husika wanazozitumikia.
Mhe. Ngunyale aliyasema
hayo jana tarehe 17 Juni, 2026 katika Ofisi ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba wakati wa makabidhiano ya Ofisi kati yake na aliyekuwa
Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Immaculata Kajetan Banzi ambaye ameteuliwa
hivi karibuni kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.
Kabla ya makabidhiano ya
ofisi, kulikuwa na mapokezi ya awali
katika viwanja vya Mahakama hiyo.
Jaji Ngunyale alisema kuwa,
kila mtumishi ana wajibu wa kuhakikisha huduma za utoaji haki zinafanyika kwa
uadilifu na weledi. Huku akisisitiza kuwa, “tujivunie nafasi tulizopewa na
kuzisimamia ipasavyo.”
“Tukifanikiwa kusimamia
majukumu yetu na kuwekeza nguvu na muda katika kazi, itatuletea nafasi thabiti
ya kujengeana uwezo katika kazi na katika majukumu mbalimbali,” amesisitiza
Mhe. Ngunyale.
Ameongeza kuwa, katika
utekelezaji wa majukumu ni muhimu kujali afya, familia zetu na jamii sambamba
na kuwa na ukaribu na kutenga muda na nafasi
kushiriki shughuli za kijamii ambazo kwa namna moja hudumisha afya ya kiakili
na kiutendaji kwa mtumishi.
Alisisistiza kwa kunukuu,
“To be trusted is a greater Compliment than to be loved,” Usemi kutoka kwa
Mwandishi George MacDonald ambao unamaanisha kuwa, ‘Kuaminiwa ni sifa kubwa
kuliko kupendwa.’
Kwa upande wake, aliyekuwa
Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Immaculata Kajetan Banzi ambaye kwa sasa
ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, aliwasihi watumishi hao kuendelea
kuishi kwa upendo kama walivyoishi naye kipindi akiwa katika nafasi hiyo.
Kadhalika, Mhe. Banzi
amewasihi watumishi hao kuendeleza ushirikiano. Na kuhitimisha kwa kumtakia Mhe.
Ngunyale kila la kheri katika utekelezaji wa majukumu mapya katika Kituo hicho.
Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba, Mhe. David Ngunyale akisalimiana na Watumishi wa Mahakama hiyo alipowasili katika Kituo chake kipya cha kazi jana tarehe 17 Juni, 2026.
Jaji wa Mahakama ya Rufani na aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Bukoba, Mhe. Immaculata Kajetan Banzi (kulia) akimkabidhi taarifa ya makabidhiano ya ofisi Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba, Mhe. David Ngunyale.
Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Immaculata Kajetan Banzi (wa pili kushoto) akizungumza jambo wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Bukoba kwa Mhe. David Ngunyale. Wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Bukoba, Mhe. Lillian Itemba na wa kwanza kulia ni Mhe. Ferdinand Kiwonde, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba, wakiwa kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Bukoba.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba, Mhe. Said Mkasiwa akitoa neno la kumkaribisha Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama hiyo, Mhe. David Ngunyale (wa kwanza kushoto).
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni