Na KEVIN HEZRON-Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Dar es Salaam
Watumishi
kutoka Chuo cha Ufundi Arusha (Arusha Technical
College), jana tarehe 18 Juni, 2026, walitembelea Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara kwa
lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu matumizi ya mifumo ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika usimamizi na utunzaji wa
kumbukumbu.
Akizungumza wakati wa
ziara hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu – Divisheni ya Biashara, Mhe. Kevin Mhina, aliwashauri wageni hao kufanya juhudi za kuhamia
katika mfumo wa utendaji usiotegemea karatasi.
Alieleza kuwa matumizi ya
mifumo ya kidijitali hurahisisha utekelezaji wa shughuli za Taasisi, huongeza ufanisi wa utendaji
kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wakati.
Katika ziara hiyo, Afisa TEHAMA Mwandamizi wa Mahakama Kuu –
Divisheni ya Biashara, Bi. Amina Said, aliwasilisha
mada kuhusu Kanzidata ya Hifadhi na Usimamizi wa Nyaraka (Record Centre
Database) iliyobuniwa kwa lengo la kuboresha usimamizi wa majalada
yaliyofungwa.
Aliwaeleza wageni hao
changamoto zilizokuwepo kabla ya kuanzishwa kwa kanzidata hiyo, ikiwemo ugumu
wa kufuatilia maeneo yalipohifadhiwa majalada na ucheleweshaji wa upatikanaji
wa taarifa muhimu.
Aidha, aliwasilisha namna
kanzidata hiyo inavyowezesha usajili wa majalada, utambuzi wa maeneo
yanapohifadhiwa, ufuatiliaji wa Watumishi
wanaochukua majalada kwa matumizi ya muda pamoja na utoaji wa taarifa na ripoti
mbalimbali.
Kanzidata hiyo imeleta
maboresho makubwa katika kuokoa muda, kuongeza ufanisi wa kazi, kupunguza
upotevu wa majalada na kuboresha utoaji wa huduma.
Baada ya kupata
mawasilisho na kushuhudia onesho la matumizi ya kanzidata hiyo, wageni hao walionesha kuvutiwa na ubunifu huo na
kutoa pongezi kwa Mahakama Kuu – Divisheni ya Biashara kwa kutumia TEHAMA
kutatua changamoto za kiutendaji.
Kwa pamoja walieleza kuwa wamejifunza mambo mengi yatakayowasaidia katika kuboresha mifumo ya usimamizi wa kumbukumbu katika Taasisi yao.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Kevin Mhina akiwakaribisha Watumishi kutoka Chuo cha Ufundi Arusha.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Kevin Mhina akizungumza na wageni kutoka Chuo cha ufundi Arusha. Kushoto kwake, ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Susan Kihawa, na Kulia kwake ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Bw. Anatory Kagaruki.
Bi.
Amina Said, Afisa TEHAMA wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, akitoa
wasilisho juu ya matumizi ya kanzidata ya usajili, usimamizi na utunzaji wa
kumbukumbu.
Wageni kutoka Chuo cha ufundi Arusha, wakisikiliza kwa makini mawasilisho yaliyoandaliwa.
Picha
na Iman Kasian, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni