Alhamisi, 2 Julai 2026

ILO DAR ES SALAAM YAMUAGA JAJI MLYAMBINA

  • Yaahidi kuendeleza ushirikiano na Jaji Mfawidhi mpya

Na LIGHTNESS KABAJU-Mahakama, Divisheni ya Kazi

Viongozi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Ofisi ya Dar es Salaam, jana tarehe 1 Julai, 2026 walikutana na Viongozi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kwa ajili ya kumuaga aliyekuwa Jaji Mfawidhi, Mhe.  Dkt. Yose Mlyambina, ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano ILO Kazi House, Viongozi hao walimkaribisha pia Jaji Mfawidhi mpya, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wawakilishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, ILO na Wadau wengine wa haki kazi na ajira.

Mhe. Dkt. Mlyambina aliwasilisha shukrani zake kwa ILO kwa kuwa bega kwa bega na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi katika kufanikisha shughuli mbalimbali kwa kipindi chote alichohudumu katika ofisi hiyo. 

Alieleza kuwa ILO imekuwa ikishirikiana na Mahakama hiyo katika kuimarisha haki kazi nchini. Ushirikiano huo ni pamoja na kuwezesha machapisho ya (Labour Case Reports) ambazo zimekuwa msaada mkubwa katika kuimarisha utoaji wa haki kazi.

Aidha, alieleza kuwa ILO imekuwa ikiwezesha mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi ambapo watumishi na Wadau wengine wamekuwa wakinufaika kwa kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Ofisi ya ILO, anayehudumia Tanzania, Kenya, Rwanda na Uganda, Bi. Caroline Mugalla, alisema kuwa mfumo madhubuti wa haki za kazi ni msingi muhimu wa kuendeleza ajira zenye staha na haki za kijamii.  

Vilevile, alisisitiza kuwa ushirikiano wa muda mrefu kati ya ILO na Mahakama ya Tanzania umechangia kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wafanyakazi na waajiri kupitia mfumo wenye ufanisi wa utoaji haki.

Bi. Caroline, kwa niaba ya ILO, alitumia nafasi hiyo kumshukuru Jaji Mlyambina kwa utendaji kazi wake katika kipindi chote alichohudumu, huku akimpongeza kwa  kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Katika kumkaribisha Jaji Mfawidhi mpya, Bi. Caroline alieleza kuwa ILO itaendelea kushirikiana na Mahakama ya Tanzania katika kuimarisha mfumo wa haki kazi nchini kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.

Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe.  Dkt. Yose Mlyambina, ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, akimkabidhi zawadi Mkurugenzi wa Ofisi ya ILO, anayehudumia Tanzania, Kenya, Rwanda na Uganda, Bi. Caroline Mugalla.

Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe.  Dkt. Yose Mlyambina, ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Ofisi ya ILO, anayehudumia Tanzania, Kenya, Rwanda na Uganda, Bi. Caroline Mugalla.

Viongozi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi na wale kutoka  Ofisi ya ILO Dar es Salaam wakiwa kwenye mazungumzo. 

Mkurugenzi wa Ofisi ya ILO, anayehudumia Tanzania, Kenya, Rwanda na Uganda, Bi. Caroline Mugalla (kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga.

Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe.  Dkt. Yose Mlyambina, ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama ya Rufani (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na mkabidhi Mkurugenzi wa Ofisi ya ILO, anayehudumia Tanzania, Kenya, Rwanda na Uganda, Bi. Caroline Mugalla (kulia) na Jaji Mfawidhi mpya, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga.


Picha ya pamoja kati ya Viongozi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi na wale kutoka  Ofisi ya ILO Dar es Salaam.

 Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Singida.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni