Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Jaji wa Mahakama ya
Rufani Tanzania, Mhe. Dkt.Yose Mlyambina amesema kuwa, masuala ya usalama na afya
si jambo la hiyari bali ni sehemu muhimu ya utawala bora na utoaji haki wenye
ufanisi.
Jaji Mlyambina ambaye
alikuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi kabla ya
kuteuliwa kuwa Jaji wa Rufani ameyasema hayo leo tarehe 02 Julai, 2026 alipokuwa
akitoa neno wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya siku mbili Usalama na Afya Mahali
pa Kazi kwa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani yanayofanyika kwenye ukumbi wa
mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
"Tumekuza utamaduni
wa usalama na afya mahala pa kazi ndani ya Mhimili wa Mahakama. Kupitia
ushirikiano huu thabiti na OSHA, tumeshaendesha mafunzo kwa Majaji, Wasajili,
Mahakimu, watumishi wa kada za utendaji, na hata watumishi wenye ulemavu.
Msisitizo wetu ni kwamba usalama na afya ni haki ya kila mfanyakazi bila ubaguzi,"
amesema Jaji Mlyambina.
Mratibu huyo ameeleza juu
ya mafanikio ya mafunzo ya aina yake yaliyofanyika mwaka jana (2025) jijini
Mwanza (Malaika Hoteli) ambapo teknolojia ya kisasa ilitumika kuunganisha kumbi
mbili tofauti ili Viongozi na Kada saidizi (Majaji na Madereva) wapate mafunzo
yanayoendana na majukumu yao kwa wakati mmoja.
Mhe. Dkt. Mlyambina
amesema baada ya mafunzo hayo, walitembelea katika Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti, ambapo waliendelea kujifunza kuhusu haki kazi katika mazingira ya
mbugani, ambapo walidhihirisha kwamba usalama na afya mahala pa kazi ni suala
ambalo linahusu kila eneo la kazi na kila mazingira ya utendaji.
Aidha, Mhe. Dkt. Mlyambina amesema kwa awamu hii, mafunzo yanalenga kujenga uwezo wa Majaji wa Rufani wapya na viongozi waandamizi, kutekeleza Sheria ya OSHA, inayomtaka kila mwajiri kuweka mazingira salama ya kazi, kuhimili changamoto za kisaikolojia, hasa kukabiliana na msongo wa mawazo (stress) na madhara ya kisaikolojia yanayotokana na kazi za utoaji haki (vicarious trauma) na kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Mwaka, 2050 kupitia watumishi wenye afya bora na tija kubwa.
Ameongeza kwamba, lengo ni kuwafikia Viongozi na Watumishi wote wa Mahakama kwa awamu ili kila mmoja, popote alipo, apate uelewa na ujuzi wa kujilinda na kulinda wenzake mahala pa kazi.
“Tunamini kwamba
Mahakama yenye Viongozi na Watumishi wanaozingatia usalama na afya mahala pa
kazi ndio inayoweza kutoa haki kwa ufanisi zaidi na kuchangia maendeleo
endelevu ya taifa, na hasa katika kutekeleza Dira ya Taifa ya mwaka 2050,” ameeleza
Jaji Mlyambina.
Kadhalika, Jaji Mlyambina ameongeza kuwa, ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na OSHA unaendelea kuwa mfano wa kuigwa katika Taasisi za umma, ukionesha namna utekelezaji wa Sheria za Usalama kazini unavyoweza kuongeza ufanisi, kulinda nguvu kazi ya Taifa na kuhakikisha haki inatendeka katika mazingira salama na yenye staha.
“Mhe. Jaji Mkuu, kwangu binafsi, mafunzo haya yana maana ya kipekee. Mbali na kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, ninayo heshima ya kuwa Mratibu wa mafunzo haya. Katika kipindi nilichohudumu kama Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mahakama imejenga na kuimarisha ushirikiano wa karibu na Wadau wa haki kazi, ikiwemo pamoja na OSHA Tanzania,” ameeleza Mhe. Dkt. Mlyambina.
Aidha, Jaji Mlyambina amempongeza
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, kwa utendaji kazi wake uliotukuka na
wa kizalendo, ikiwa ni pamoja na kufadhili mafunzo hayo na kutoa vifaa kinga ili
kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa Majaji.
Katika hatua nyingine,
Mhe. Dkt. Mlyambina ametumia jukwaa hilo kumpongeza Dkt. John Anthony Jingu
kufuatia kuteuliwa kwake na Rais wa Jamhuri ya Munungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan kuwa Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama ya Tanzania.
Mafunzo hayo yamebeba Kaulimbiu isemayo, "Nafasi ya Haki Kazi, Afya na Usalama Mahala pa Kazi kwa Maendeleo Endelevu."
Washiriki wa mafunzo pamoja na baadhi ya Viongozi waalikwaJaji kutoka Mahakama wakimsikiliza Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt.Yose Mlyambina alipokuwa akitoa neno leo tarehe 02 Julai, 2026 wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya siku mbili Usalama na Afya Mahali pa Kazi kwa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani yanayofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni