Na ARAPHA- RUSHEKE, Mahakama Kuu Dodoma.
Mahakama
Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dodoma, hivi karibuni ilifanya Kikao cha
Kusukuma Mashauri ya Madai (Bench Bar) kilichowakutanisha wadau mbalimbali wa
sekta ya sheria na haki, kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa mashauri ya
madai, kupunguza mlundikano na kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki kwa
wakati.
Kikao
hicho kiliongozwa na Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga, na kuhudhuriwa
na wawakilishi kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Ofisi ya Msajili wa Hati
pamoja na Baraza la Usuluhishi na Uamuzi (CMA).
Akifungua
kikao hicho, Jaji Mfawidhi alisisitiza umuhimu wa wadau wote wa sekta ya sheria
na haki kuendelea kutekeleza na kufuatilia kwa vitendo mikakati iliyoelekezwa
na Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. George Masaju, yenye lengo la kuhakikisha mashauri yanasikilizwa na
kuamuliwa mapema ipasavyo, kupunguza mlundikano na kuimarisha utoaji wa haki
nchini.
Akiwasilisha
taarifa ya hali ya mashauri ya madai, Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dodoma, Mhe. Upendo Ngitiri,
alisema Mahakama inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuhakikisha
mashauri yanasikilizwa na kuamuliwa kwa wakati, sambamba na kudhibiti mashauri
ya mlundikano.
Alieleza kuwa Mahakama imeendelea
kufanya vikao maalum vya kusafisha mashauri (clean-up sessions), kutoa
kipaumbele kwa mashauri ya kimkakati na
matumizi ya hati ya maelezo ya shahidi (Witness statement) kwa dhumuni la kumaliza mashauri haraka na
kupata kumbukumbu nzuri ya kile alichokikusudia mteja.
Mikakati mingine ni kusikiliza
mashauri kadri inavyokuwa yamekamilika au yameiva bila kujali yamepokelewa
lini, kuhimiza matumizi ya usuluhishi
pale inapowezekana, kukamilisha hatua za awali ya mashauri ya awali ndani ya siku 30, kutoa
ahirisho lisilozidi wiki mbili na
kuimarisha ushirikiano na wadau wa mnyororo wa haki ili kuondoa vikwazo
vinavyochelewesha usikilizaji wa mashauri.
Kikao
hicho pia kilibaini mashauri yanayokaribia kuwa ya mlundikano na kuweka
mikakati ya kuyashughulikia mapema. Aidha, wadau walisisitiza umuhimu wa
kushughulikia migogoro katika ngazi zinazotakiwa kisheria kabla ya kufikishwa mahakamani,
hususan mashauri ya ardhi, pamoja na kuhakikisha mashauri yanaamuliwa kwa
kuzingatia ushahidi na hoja za msingi badala ya kasoro za kiufundi.
Miongoni
mwa mikakatii iliyofikiwa ni kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Mahakama
na Taasisi za mnyororo wa haki, kuongeza matumizi ya usuluhishi katika kutatua
migogoro, kuharakisha utekelezaji wa hukumu na kuhakikisha mashauri
yanayosikilizwa yanakamilika kwa wakati kwa kuzingatia sheria na kanuni.
Mikakati
mingine iliyofikiwa ni kutosajili mashauri ya ardhi ambayo yalipaswa
kuanzia kwa Msajili wa Hati kwa mjibu wa
sheria pamoja na kufuatilia utekelezaji wa mikakati ya kikao cha Jaji Mkuun na
Wadau wa Haki Madai inayolenga kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki.
Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dodoma, imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wote wa sekta ya sheria na haki ili kuboresha utoaji wa huduma za Mahakama, kupunguza mlundikano wa mashauri na kuhakikisha wananchi wanapata haki mapema ipasavyo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga, akiongoza kikao cha
kusukuma mashauri ya madai.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim
Tiganga, (aliyepo katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe na
wadau wa kikao hicho. Kulia kwake waliokaa ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Dodoma,
Mhe. Upendo Ngitiri na kushoto kwake ni Naibu Msajili, Mhe.Zabibu Mpangule.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni