Jumamosi, 11 Julai 2026

JENGENI UTAMADUNI WA UWAJIBIKAJI NA UWAZI KAZINI; JAJI FRANK MAHIMBALI

Na SETH KAZIMOTO – Mahakama Kuu Arusha

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali amewaagiza Viongozi wa ngazi mbalimbali za Mahakama mkoani humo kuwa ni lazima wajenge utamaduni wa uwajibikaji na uwazi kazini katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kwakuwa ndio njia bora ya kutoa huduma na kuondoa malalamiko ya wananchi wanaohudumiwa.

Mhe. Mahimbali aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa Kikao cha Menejimenti cha Masjala hiyo kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Sparrow iliyopo wilayani Karatu.

Akizungumza na wajumbe wa kikao hicho, Jaji huyo Mfawidhi alisisitiza kuwa ni lazima Hakimu anaposoma hukumu ahakikishe anatoa na nakala yake siku hiyo ya kusoma hukumu.

Amesisitiza kwa kusema kuwa, kushindwa kutoa nakala ya hukumu kwa wakati ni ukiukwaji wa miongozo iliyopo na kusababisha malalamiko yasiyo ya lazima kutoka kwa wateja na wadau wa Mahakama.

Mhe. Mahimbali ametoa maagizo kwa Mahakimu wote Wafawidhi kufuatilia kwa karibu Mahakimu walio chini yao kuhakikisha kuwa, taarifa muhimu kama nakala za hukumu na mienendo ya mashauri wateja wanazipata kwa urahisi na kwa wakati na hivyo kujiepusha na malalamiko yasiyo ya lazima.

Vilevile, Jaji Mahimbali ametoa maelekezo kwa kila Mahakama kuboresha utoaji huduma kwa wateja. Amesisitiza kwa kusema, “Sisi tunafanya kazi kwa Umma, tunahudumia wananchi, Mahakama zetu ni kwa ajili ya wananchi, kwa hiyo maslahi ya wananchi yawe kipaumbele cha kwanza. Tunao wajibu wa kuwahudumia wananchi kwa heshima, utu na usafi.”

Hali kadhalika, Mhe. Mahimbali amewaasa wajumbe kuzingatia maadili ya kazi katika kusimamia Mahakama zao ikiwemo matumizi sahihi ya fedha za ofisi na kujiepusha na tamaa hatarishi.

Aliongeza kuwa, ni wajibu wa Viongozi wa Mahakama husika kuhakikisha kuwa, watumishi walio chini yao wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa miongozo ya kazi kama sehemu ya kuwaepusha watumishi kufanya matendo yanayokiuka taratibu za kazi na hatimaye kuwekwa nguvuni na vyombo vya sheria.

Pia, Jaji Mahimbali ameelekeza mambo mbalimbali yanayolenga kuongeza ufanisi kazini, ikiwemo Mahakimu kuzingatia muda uliowekwa wa mashauri kuisha, kuepuka kuahirisha mashauri bila sababu za msingi, kusimamia ubora wa hukumu, maamuzi na amri za Mahakama; watumishi kuwa waadilifu na waaminifu kazini, usimamizi bora wa fedha na rasilimaliwatu, kuimarisha ushirikiano kati ya Viongozi na watumishi wa ngazi za chini na watumishi kujiepusha na vitendo vinavyoharibu taswira nzuri ya Mahakama.

Aidha, amewaagiza Mahakimu Wafawidhi kufanya tathmini ya kaguzi wanazofanya na kubaini maeneo yanayohitaji mafunzo na kuchukua hatua ya kuandaa mafunzo ya ndani kwa lengo la kuwaelimisha watumishi walio chini yao na hatimae kuongeza ufanisi wa kazi.

Amezitaka Mahakama mkoani Arusha kuboresha utunzaji wa kumbukumbu na kuendelea kutumia mifumo ya Kitehama iliyopo Mahakamani hususan Mifumo ya kuratibu mashauri (e-CMS na Primary Court Mobile App).

Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye ni Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Mhe. Erasto Philly, aliwasilisha taarifa ambayo ilionesha kuwa hadi kufikia tarehe 18 Machi, 2026, Mahakama Kuu Arusha ilikuwa na mashauri yanayoendelea 593, ambapo kwa kipindi cha kuanzia tarehe 18 Machi, 2026 hadi tarehe 30 Juni, 2026 yalisajiliwa mashauri 324, yalimalizika mashauri 448 na kubaki mashauri 469.

Katika mashauri hayo (469) yaliyobaki, mashauri ya mlundikano ni matatu ambayo yote ni mashauri ya utekelezaji.

Mhe. Philly aliendelea kusema kuwa, hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2026 Mahakama ya Hakimu Mkazi ilikuwa na mashauri 72 yaliyokuwa yakiendelea Mahakamani na kwa kipindi cha kuanzia Mwezi Aprili hadi Juni 2026, Jumla ya mashauri 45 yalisajiliwa na mashauri 61 yakasikilizwa. Idadi ya mashauri yaliyobaki kufikia tarehe 30 Juni, 2026 yalikuwa 56.

Naibu Msajili huyo alizitaja pia takwimu za Mahakama za Wilaya mkoani Arusha kuwa, hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2026, Mahakama hizo zilikuwa na mashauri 334 yaliyokuwa yanaendelea Mahakamani, na kwa kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni 2026, jumla ya mashauri 514 yalisajiliwa na 470 yalisikilizwa. Idadi ya mashauri yaliyobaki kufikia tarehe 30 Juni, 2026 yalikuwa 378.

Kwa upande wa Mahakama za Mwanzo Mkoa wa Arusha, Mhe. Philly alisema kuwa, zilikuwa na jumla ya mashauri 207 yaliyokuwa yakiendelea Mahakamani hadi kufikia tarehe 30 Machi, 2026, na kwa kipindi cha kuanzia mwezi Aprili hadi Juni yalisajiliwa mashauri 4,169 na yalisikilizwa mashauri 4,121. Mashauri yaliyobaki tarehe 30 Juni, 2026 yalikuwa 255.

Aliongeza kuwa, kumekuwa na changamoto mbalimbali katika usikilizaji wa mashauri hayo, ikiwa ni pamoja na majalada yanayoitishwa kutoka Mabaraza ya Ardhi na Usuluhishi kutokuletwa kwa wakati, Majalada yaliyorudishwa katika Mabaraza ya Ardhi na Tume ya Usuluhishi kwa ajili ya kufanyiwa masahihisho kutorejeshwa kwa wakati, mashahidi kutoletwa kwa wakati katika mashauri ya jinai na kusababisha mashauri kuchelewa kuisha mahakamani na wakati mwingine hata kusababisha vikao maalum vya mashauri ya Jinai kusogezwa mbele.

Naye Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Arusha, Bi. Grace Kapama amebainisha katika wasilisho lake kuwa, kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 Mahakama Arusha imepiga hatua kubwa katika mambo mbalimbali yanayoweka mazingira mazuri katika utekelezaji wa shughuli za Mahakama ikiwemo mafunzo kwa watumishi, kubadilishwa kada watumishi wenye sifa, kulipa stahili za Viongozi kwa wakati.

Mengine ni kuwezesha sare za watumishi wasio Mahakimu, kufanya ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya Mahakama, kuanzisha Mahakama mpya na kufufua Mahakama zilizokuwa zimefungwa kwa muda mrefu.

Pia, Bi. Kapama aliongeza kwa kusema kuwa, Mahakama hiyo imepiga hatua kubwa katika malipo ya fedha za mirathi ambapo katika Mwaka wa Fedha uliopita 2025/2026, Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Arusha imefanya malipo ya shilingi za Kitanzania takribani bilioni tatu (3,069,003,707.53/=), sawa na asilimia 86.92. Kiasi kilichobaki kwenye akaunti ya Mirathi kufikia tarehe 30 Juni, 2026 kilikuwa takribani shilingi milioni mia nne na sitini na moja (461,609,115.19/=), ambapo juhudi zinaendelea kumalizia malipo ya fedha hizo za mirathi zilizosalia.

Kikao hicho kimehudhuriwa na wajumbe mbalimbali kutoka Mahakama za Mkoa wa Arusha hususan Mahakimu Wakazi Wafawidhi na Maofisa mbalimbali waliowakilisha Mahakama zao.

Wajumbe hao wamejadili mambo mbalimbali ikiwemo mafanikio na changamoto wanazokumbana nazo katika kazi na kubadilishana uzoefu wa namna ya kuboresha utendaji kazi katika maeneo yao.

Vikao hivyo vya menejimenti ni moja ya fursa inayouwezesha Uongozi wa Mahakama Arusha kufanya tathmini na kujadili kwa pamoja juu ya namna bora ya kutekeleza shughuli za Mahakama na hatimaye kuongeza ufanisi katika kazi.

Vikao hivyo hufanyika katika Mahakama tofauti tofauti kwa mzunguko ambapo kikao hicho kimefanyika Wilayani Karatu, Mahakama ya Wilaya Karatu wakiwa ni wenyeji. Kikao kitakachofuata kitafanyika mwezi Oktoba, 2026 Wilayani Longido.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali akifungua Kikao cha Menejimenti cha Mahakama Arusha kilichofanyika hivi karibuni kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Sparrow iliyopo Wilayani Karatu. Kushoto ni Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Arusha, Bi. Grace Kapama. 


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Mhe. Erasto Philly akifafanua jambo wakati wa Kikao cha Menejimenti ya Mahakama Arusha kilichofanyika hivi karibuni kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Sparrow mjini Karatu. Kushoto ni Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Arusha, Mhe. Sheila Manento.


Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Arusha, Bi. Grace Kapama (aliyesimama) akifafanua jambo wakati wa Kikao cha Menejimenti kilichofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Sparrow iliyopo Wilaya Karatu. Kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali. 

Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya Monduli na Karatu, Mhe. Pamela Meena (kushoto) na Mhe. Samwel Mushumbusi (kulia) wakishiriki kikamilifu Kikao cha Menejimenti ya Mahakama Arusha kilichofanyika hivi karibuni kwenye Hoteli ya Sparrow Karatu Mjini.

Wajumbe mbalimbali walioshiriki katika Kikao cha Menejimenti ya Mahakama Arusha kilichofanyika hivi karibuni kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Sparrow Wilayani Karatu.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni