Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Kibaha
Kikao cha Kusukuma Mashauri ya Jinai kwa Mahakama ya Wilaya na Mahakama za Mwanzo katika Wilaya ya Kibaha kimejadili na kuomba Askari wanaokaa Mahakama za Mwanzo kutekeleza amri mbalimbali za Mahakama kupatiwa mafunzo ya namna ya kuendesha mashauri ya jinai.
Hayo yamesemwa jana tarehe 10 Julai, 2026 katika kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha.
Akizungumza katika kikao hicho, namna ambavyo washtakiwa na walalamikaji katika mashauri ya jinai, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Mkuza, Mhe. Leah Mkono amesema kuna ugumu unatokea pale Askari wanafika Mahakamani na vielelezo hawavitoi wakati wa usikilizaji wa shauri badala yake wanavitelekeza tu Mahakamani na baada ya shauri kuisha ndipo mlalamikaji anadai vielelezo alikuwa navyo askari wakati huo shauri limeshaisha hali inayosababisha haki za wadaa kupotea.
Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mailimoja, Mhe. Honorina Kambadu ameeleza masikitiko yake kuhusiana na hati za mashtaka kukosewa kila mara kutokana na kubadilishwa kila mara kwa Askari wanaofika Mahakamani hapo kiasi kwamba akielekezwa Askari huyu akaelewa, kesho anakuja Askari mwingine hivyo kumekuwa na ugumu wa kufanya kazi na Askari tofauti tofauti.
Wakati, huohuo amesema kumekuwa na uhaba wa Askari Polisi ambapo Mahakimu watano lakini Askari mmoja jambo hilo linasababisha kusubiriana wakati wa kusoma hati za mashtaka na kama kuna hukumu ya kumtia mtu hatiani inabidi wasubiri.
Akizungumzia katika masuala hayo, Katibu wa Kikao hicho ambaye ni Wakili wa Serikali Said Seif amesema, kutokana na changamoto hizo anayapokea hayo yote na kwamba atayafikisha kwa Viongozi wake na kuwashauri wafanye mafunzo ya namna bora ya kuandaa hati za mashtaka kwa Askari Polisi wa Mahakama za Mwanzo kuhusu namna bora ya kuwasilisha vielelezo Mahakamani na pia uwepo wa Askari Mahakamani bila kubadilishwa badilishwa kila siku.
Naye Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kibaha, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Victor Kashai amesema kuna uhaba wa Askari Polisi na hivyo kusababisha kuwepo kwa Askari mmoja Mahakamani lakini kutokana na changamoto hizo atazungumza na Viongozi wake kuongeza Askari ili kuepusha ucheleweshaji wa mashauri kuisha Mahakamani.
Katika kikao hicho Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Lukumai ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho amebainisha kwamba, katika Mahakama ya Wilaya kuna mashauri mawili tu yaliyovuka miezi sita na miongoni mwa mashauri hayo moja liko kwenye hatua ya maamuzi madogo na jingine liko kwenye mashauri ya majadiliano (Pre Bargain).
Aidha, Mhe.Lukumai amewataka upande wa mashtaka kwa mashauri ya majadiliano (Pre Bargain) yasizidi siku sitini (60) yakitajwa Mahakamani bila kukamilika.
Katika kikao hicho Wadau wa Haki Jinai wameweka maazimio kadhaa ili kikao kijacho waone kama yametekelezeka. Maazimio hayo ni pamoja na Mahakama za Mwanzo ziko karibu na wananchi hivyo Mahakimu wasifungwe kupita kiasi na masharti ya kiufundi (technicalities), Hati za Mashtaka zenye Mapungufu zisipokelewe Mahakamani.
Pia umetolewa ushauri kwa Mahakimu kutokana na mabadiliko ya Sheria ya Kieletroniki kuruhusu Ushahidi kupokelewa Mahakama za Mwanzo wajitahidi kusoma na kuelewa vizuri na kutofautisha kati ya maudhui ya kidijitali (Digital Content) na maudhui ya Makala (Documentary Content) na taratibu za upokeaji wake na pia kufanya kozi fupi zinazotolewa na Vyuo Vikuu kuhusu Akili Unde (AI) ili kuendana na wakati na hali halisi maana uhalifu mwingi umehamia kwenye mambo ya kimtandao zaidi kuliko uhalifu wa kawaida.
Sambamba na kikao hicho cha kusukuma mashauri ya jinai pia kimefanyika kikao cha kusukuma mashauri ya madai (Bench Bar) ambapo wito umetolewa kwa Mawakili kuweza kusimamia vema shajara zao ili kuepuka muingiliano wa mashauri kati ya Mahakama moja na nyingine.
Wadau wa Haki Jinai wakiwa katika picha ya pamoja baada ya Kikao cha Kusukuma Mashauri ya Jinai. Walioketi kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha na Mwenyekiti wa Kikao hicho, Mhe. Emmael Lukumai na kulia ni Katibu wa kikao hicho, Wakili wa Serikali Said Seif.
Wadau wa Haki Jinai wakiendelea na kikao.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni