Jumatatu, 13 Julai 2026

MAHAKAMA YA WILAYA UBUNGO YATIMIZA MIAKA MIWILI BILA MLUNDIKANO WA MASHAURI

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Dar es Salaam

Mahakama ya Wilaya Ubungo imefanya kikao cha tathmini ya miaka miwili tangu kufunguliwa kwake ambapo kaulimbiu ya kikao hicho ilikuwa Mahakama ya Wilaya Ubungo bila mashauri ya mlundikano (two years without backlog cases).

Kikao hicho kilifanyika tarehe 10 Julai, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama wa wazi wa Mahakama hiyo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ubungo, Mhe. Tumsifu Barnabas alisema kauli mbiu hiyo ililenga kutokuwepo kabisa kwa Mashauri ya Mlundikano na kwa sasa wametimiza miaka miwili pasipokuwa na mashauri ya Mlundikano.

Mhe. Barnabas alisema kuwa, dhumuni la kikao hicho ni kutathmini utendaji kazi, mafanikio, changamoto na pia kufahamiana na watumishi wapya waliohamia katika Mahakama hiyo kutoka vituo mbalimbali.

Aliwasisitizia Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Ubungo na Mahakama zake za Mwanzo kutimiza lengo la kaulimbiu ya Mahakama na kufanyia kazi kwa kufuata kauli mbiu ya Uadilifu, Weledi na Uwajibikaji.

Aidha, Mfawidhi huo amesema, muitikio wa wananchi katika Mahakama hiyo umekuwa Mkubwa sana na ndio maana mashauri yanayofunguliwa ni mengi. Kwa kipindi cha mwaka 2024 hadi 2026 ni zaidi ya mashauri 5000 yamefunguliwa.

Katika kikao hicho, elimu kuhusu Mahakama SACCOS ilitolewa ambapo Meneja Mikopo wa Mahakama SACCOS, Bw. Godfrey Lulenga aliwaeleza faida za Chama hicho ambazo ni pamoja na kuweka akiba lakini pia kukopesha, ambapo kuna mikopo ya aina nne.

Bw. Lulenga alitaja mikopo hiyo kuwa ni Anza Maisha; ambapo alisema ni aina ya mkopo ambao mtumishi wa ajira mpya anakopeshwa ili kujikimu na Maisha, kuna mkopo wa dharura, mkopo wa maendeleo na mkopo wa sikukuu na kwamba Mahakama SACCOS wana mgawanyo wa riba.

Sambamba na kikao hicho watumishi hao walipata wasaa wa kukata keki ya upendo wa kusherehekea miaka miwili ya Mahakama hiyo.

Kikao hicho kilihudhuriwa na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Ubungo, Mahakama ya Mwanzo Kimara, Mahakama ya Mwanzo Kwembe na Mahakama ya Mwanzo Sinza/Manzese.

Mahakama ya Wilaya Ubungo ilianza kufanya shughuli za kimahakama tarehe 17 Mei, 2024.


Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Ubungo, Mhe. Tumsifu Barnabas  akizungumza jambo wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Tathmini ya miaka miwili ya Mahakama ya Wilaya Ubungo kilichofanyika tarehe 10 Julai, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama hiyo.

 Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Ubungo wakifungua kikao kwa dua.

Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Ubungo wakiwa katika picha ya pamoja na wakijiandaa kukata keki ya upendo na ishara ya kuadhimisha miaka miwili ya Mahakama hiyo.

Meneja Mikopo wa Mahakama SACCOS, 
Bw. Godfrey Lulenga akielezea faida na mikopo inayopatikana Mahakama SACCOS wakati wa Kikao cha Tathmini ya miaka miwili ya Mahakama ya Wilaya Ubungo.

Keki ya kusherehekea Maadhimisho ya miaka miwili ya Mahakama ya Wilaya Ubungo.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni