Jumatatu, 13 Julai 2026

TIMU ZA MAHAKAMA SPORTS KIGOMA, REDIO JOY ZASAKATA KABUMBU

  • Zaibuka kwa sare ya goli mbili kwa mbili
  • Mahakama Sports Kigoma azindua Jezi mpya

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Kapteni wa Timu ya Mahakama Sports Kigoma, Bw. Omary Magege ameongoza Kikosi cha Mpira wa Miguu kilichochuana vikali na Timu ya Redio Joy ya Mkoani humo katika Mechi ya kirafiki baina ya timu hizo iliyolenga kuzindua Jezi/Sare mpya za Timu ya Mahakama sambamba na kudumisha mahusiano na wadau.

Mechi hiyo ilifanyika tarehe 11 Julai, 2026 katika uwanja wa Kajuna uliopo katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Kocha wa Timu ya Mpira ya Mahakama Kigoma, Bw. Ramadhani Kufakunoga, alisema, “Tunawashukuru Viongozi wetu wa Mahakama Kigoma, kuona Timu hii inastahili jezi mpya pamoja na vifaa vingine kwa ajili ya mechi mbalimbali ambazo zinaendelea. Uwepo wa vifaa hivi vya michezo kwa Wachezaji ni motisha kubwa sana inayoungwa mkono na Timu hii pamoja na Mashabiki wetu.”

Kabla ya Mechi hiyo, Bw. Kufakunoga aliwataka Wachezaji wa Timu ya Mahakama kucheza kwa upendo na kujiamini ili kuonesha weledi katika mpira wao bila kusababisha majeraha kwa Timu pinzani.

Hata hivyo aliwatia shime kuwa, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka, ambaye ndio Mdhamini Mkuu wa timu hiyo ameahidi kufanya makubwa yanayoleta motisha katika michezo, hivyo waendelee kuvitumia vipaji vyao ili kuileta Mahakama pamoja na wananchi.

Na kwa upande wake, Mkurugenzi wa Redio Joy Kigoma, Bw. Mwenge Muyombi, alisema kuwa, “Mechi hii ni ya kuimarisha mahusiano hivyo chezeni kwa furaha, hii ni sehemu ya kujenga afya zaidi, pia kujiandaa na mashindano mengine ya kirafiki yanayokuja, hivyo tunategemea burudani nzuri sana, nawatakia mpira mwema.”

Aidha, mechi hiyo iliendelea kwa mchuano mkali ambapo mpaka dakika ya 65, Timu ya Mahakama ilikuwa inaongoza, hata hivyo, Wachezaji wa Mahakama walionesha uimara mkubwa ambapo baadae kibao ikiligeuka kwa Timu ya Redio Joy kujitutumua na kujibu mapigo kwa wapinzani wao na kuiwezesha mechi hiyo kutoka sare ya mbili kwa mbili.

Ushindi huo kwa timu zote mbili ilikuwa ni kipimo kizuri ambapo Makocha wa Timu zote mbili, walibaini wapi wakaboreshe ili kuendelea kuwa na Timu bora zaidi katika mechi zijazo.

Watumishi wa Mahakama na Redio Joy walijumuika na wananchi waliojitokeza katika mechi hiyo, ambapo walionesha kufurahia mchezo huo kwani ulisheheni utulivu na weledi wa kucheza mpira kwa malengo ya mmoja wapo kuwa mshindi ingawa mizani ililingana kwa matokeo ya sare.


Kikosi cha Timu ya Mahakama Sports Kigoma kikiwa katika uzi mpya wa jezi iliyozinduliwa katika Mechi yao na Timu ya  Redio Joy Kigoma.


Kapteni wa Timu ya Mahakama Sports Kigoma, Bw. Omary Magege akitoa neno baada ya dakika 45 kutamatika, wakiongoza kwa goli moja dhidi ya wapinzani wao Timu ya Redio Joy Kigoma.

Mkurugenzi wa Redio Joy Kigoma, Bw.Mwenge Muyombi akisalimiana na  Wachezaji wa Timu zote mbili ya Mahakama Sports Kigoma na ya Redio Joy mara baada ya kutoa neno kwa Wachezaji wote wa Timu hizo.


Kikosi cha Timu ya Redio Joy Kigoma kikiwa maridadi kwa ajili ya mchezo wa kirafiki na Timu ya Mahakama Kigoma,  mechi iliyopigwa katika uwanja wa Kajuna Kigoma.


Sehemu ya Mashabiki wa Timu ya Redio Joy wakifuatilia Mchezo uliokuwa ukiendelea katika Uwanja wa Kajuna uliopo katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.


Sehemu ya Mashabiki na Watumishi wa Timu ya Mahakama  wakifuatilia Mchezo uliokuwa ukiendelea katika Uwanja wa Kajuna uliopo katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.


Sehemu ya wananchi wakifuatilia mchezo uliokuwa ukiendelea katika Uwanja wa Kajuna uliopo katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.

 

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni