· Yanawaandaa pia Majaji wapya kutekeleza majukumu yao kwa
weledi, kujiamini na kuzingatia misingi ya utoaji haki
Na HALIMA MNETE, Mahakama-Dodoma.
Majaji wa Mahakama ya Rufani wametakiwa kutumia mafunzo
elekezi wanayopatiwa kama fursa ya kujenga uwezo, kuongeza ufanisi katika
utekelezaji wa majukumu yao na kuimarisha utoaji haki unaozingatia misingi ya
Katiba, sheria na maslahi ya wananchi.
Hayo yameelezwa leo tarehe 06 Julai, 2026 na Jaji wa
Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)-Lushoto,
Mhe. Dkt. Paul Kihwelo alipokuwa akitoa neno la utangulizi wakati wa ufunguzi
wa Mafunzo Elekezi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani yanayofanyika kwenye Ukumbi
wa miktano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Mafunzo hayo yamefunguliwa rasmi na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju na yamewaleta pamoja Majaji wapya wa
Mahakama ya Rufani kwa lengo la kuwaandaa kuanza kutekeleza majukumu yao katika
ngazi hiyo ya juu ya utoaji haki.
Akitoa salamu zake, Mhe.Dkt. Kihwelo amemshukuru Mungu kwa
kuwezesha kufanyika kwa mafunzo hayo na Jaji Mkuu kwa kuridhia kufanyika kwa mafunzo
hayo, kushiriki katika ufunguzi wake pamoja na kukubali kuwa mmoja wa Wawezeshaji
wa mafunzo hayo licha ya majukumu yake mengi ya kiuongozi.
Amesema ushiriki wa Jaji Mkuu kama Mwezeshaji ni ishara ya
namna ambavyo Uongozi wa Mahakama ya Tanzania unavyoweka kipaumbele katika
maendeleo ya taaluma na kuwajengea uwezo Majaji ili waendelee kutekeleza
majukumu yao kwa viwango vya juu vya weledi.
Mhe.Dkt. Kihwelo pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuiamini Mahakama ya
Tanzania kupitia uteuzi wa Majaji wa Mahakama ya Rufani, akisema kwamba, hatua
hiyo imeendelea kuimarisha uwezo wa Taasisi hiyo katika utoaji haki.
Sambamba na hilo, amewapongeza Majaji tisa walioteuliwa hivi
karibuni kujiunga na Mahakama ya Rufani, akiwakaribisha rasmi katika ngazi hiyo
ya juu ya Mhimili wa utoaji haki na kuwahimiza kutumia mafunzo hayo kama msingi
wa safari yao mpya ya utumishi.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa mafunzo hayo, Mhe. Dkt.
Kihwelo amesema jukumu kuu la Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ni
kuwajengea uwezo watumishi wa Mahakama ili kuboresha utendaji wao katika utoaji
haki, akibainisha kuwa, mafunzo hayo yanatekeleza Sera ya Mafunzo ya Mahakama
ya mwaka 2019 pamoja na Sera ya Mafunzo ya Taifa.
Ameongeza kuwa, Mahakama imeendelea kujenga utamaduni wa
kuhakikisha Viongozi wote wanaoteuliwa katika nafasi mpya wanapatiwa mafunzo
elekezi kabla ya kuanza rasmi majukumu yao, hatua ambayo imechangia kuongeza
ufanisi katika utekelezaji wa kazi za Mahakama.
"Dhamira yetu ni kuhakikisha kila Kiongozi anayepata
nafasi mpya anaingia akiwa ameandaliwa ipasavyo ili aweze kutekeleza majukumu
yake kwa weledi na kujiamini," amesema.
Aidha, ameeleza kuwa, mafunzo hayo ni ya tano kufanyika kwa Majaji
wa Mahakama ya Rufani tangu programu hiyo ilipoanzishwa mwaka 2019, jambo
linaloonesha dhamira ya Mahakama ya Tanzania ya kuendelea kuwekeza katika
maendeleo ya rasilimali watu.
Kwa mujibu wa Mhe. Dkt. Kihwelo, washiriki watapata mafunzo
kutoka kwa Wawezeshaji wenye uzoefu mkubwa katika masuala ya Mahakama ya
Rufani, wakiwemo Majaji Waandamizi na Wastaafu, ambao watashirikiana nao
kupitia majadiliano ya kitaaluma yanayojikita katika uzoefu wa kazi za kila
siku.
Amesema, mada zitakazowasilishwa zimeandaliwa mahsusi
kuwasaidia Majaji hao kuelewa kwa kina majukumu yao mapya, ikiwemo misingi ya
utoaji haki, masuala ya utawala wa Mahakama ya Rufani, mwenendo wa mashauri
yanayosikilizwa mbele ya Jaji mmoja na yale yanayosikilizwa na jopo la Majaji,
maombi ya mapitio (Revision) pamoja na tofauti za kiutendaji kati ya Mahakama
Kuu na Mahakama ya Rufani.
Aidha, Jaji Kihwelo amesisitiza kuwa, mafunzo hayo pia
yatawakumbusha Majaji umuhimu wa kuzingatia lengo kuu la Mahakama ambalo ni
kutenda haki kwa wananchi, akieleza kuwa masharti ya kiufundi hayapaswi kuwa
sababu ya kuchelewesha au kunyima haki pale mazingira ya kisheria yanaporuhusu
haki kutendeka.
"Lengo kubwa la Mahakama ni kuamua migogoro na
kuhakikisha haki inapatikana kwa mujibu wa Katiba na sheria. Tunapaswa kujikita
zaidi katika kutatua migogoro kuliko kushikilia masharti ya kiufundi yanayoweza
kuathiri upatikanaji wa haki," amesema.
Mbali na mada za kisheria, amesema washiriki watapata
mafunzo kuhusu afya ya akili na namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo,
akibainisha kuwa afya njema ya Jaji ni msingi muhimu wa utoaji wa maamuzi yenye
ubora.
Aidha, amesema mafunzo hayo yataendeshwa kwa kuzingatia
matumizi ya teknolojia, ambapo washiriki watapatiwa nyenzo zote za mafunzo
kupitia mfumo wa ‘QR Code’, utakaowawezesha kupata maudhui yote ya sasa pamoja
na mafunzo yaliyotolewa katika programu zilizopita kwa urahisi.
Mhe.Dkt. Kihwelo ameeleza kuwa, mfumo huo wa kidijitali
unapunguza matumizi ya karatasi huku ukiwapa washiriki fursa ya kurejea nyenzo
hizo wakati wowote wanapozihitaji katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumzia mbinu ya ufundishaji, amesema mafunzo hayo
yameandaliwa kwa mfumo wa majadiliano na kubadilishana uzoefu badala ya
mihadhara ya kawaida, ili kuwawezesha washiriki kujifunza kupitia uzoefu wa
vitendo kutoka kwa Majaji waliobobea katika kazi za Mahakama ya Rufani.
Alisema uzoefu wa mafunzo yaliyopita umeonesha kuwa mfumo
huo umekuwa na mchango mkubwa katika kuwaandaa majaji wapya na kuongeza
kujiamini kwao wanapoanza kutekeleza majukumu yao.
Akihitimisha hotuba yake, Mhe.Dkt. Kihwelo aliishukuru
Sekretarieti ya Mahakama ya Tanzania, hususan Idara ya Utawala na Usimamizi wa
Rasilimali Watu, pamoja na Sekretarieti ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
(IJA), kwa maandalizi na ushirikiano uliowezesha kufanyika kwa mafunzo hayo.
Amesema ushirikiano huo unaendelea kuimarisha juhudi za
Mahakama ya Tanzania katika kujenga mfumo endelevu wa maendeleo ya kitaaluma
kwa Majaji na watumishi wake, hatua inayochangia kuimarisha utoaji haki nchini.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni