Jumatatu, 6 Julai 2026

MAHAKAMA KUU MASJALA NDOGO DODOMA YAWEKA MIKAKATI KUZUIA MLUNDIKANO WA MASHAURI

Na ARAPHA- RUSHEKE, Mahakama Kuu Dodoma.

Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma imeendelea kuimarisha usimamizi wa mashauri ya jinai na kuhakikisha haki inatolewa kwa wakati, ambapo hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2026 haikuwa na shauri lolote la mlundikano.

Hali hiyo ilibainishwa tarehe 03 Julai,2026 katika kikao cha Usimamizi wa Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (Case Flow Management) kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC).

Kikao hicho kilifunguliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga, ambaye alikuwa mgeni rasmi  na kuhudhuriwa na Viongozi na wawakilishi wa Taasisi mbalimbali za mnyororo wa haki jinai, wakiwemo  Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), TAKUKURU, Idara ya Uhamiaji Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Ofisi ya Ustawi wa Jamii na Idara ya Uangalizi.

Viongozi wa Mahakama pamoja na Wadau wa mnyororo wa haki jinai walikutana kwenye kikao hicho kwa lengo la kutathmini mwenendo wa mashauri, kujadili changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya kuharakisha utoaji wa haki.

Akiwasilisha taarifa ya mashauri, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Upendo Ngitiri, alisema katika kipindi cha Januari hadi Juni 2026, Mahakama ilisajili mashauri mapya 499 na kusikiliza mashauri 519.

Kwa upande wa mashauri ya jinai, mashauri mapya 203 yalipokelewa na 187 yakisikilizwa, huku kiwango cha kumaliza mashauri kikiongezeka.

Alisema mafanikio ya kutokuwa na mashauri ya jinai ya mlundikano yametokana na utekelezaji wa mikakati mbalimbali ambayo Mahakama Kuu imejiwekea, ikiwemo kufanya mapitio ya mashauri na kubaini yale yanayoweza kukamilika katika hatua za awali.

Mikakati mingine ni kufanya vikao vya mara kwa mara vya mashauri ya jinai  na vikao Maalum”Clean up Sessions” na kuongeza  matumizi ya Mahakama Mtandao katika usikilizaji wa rufaa na maombi ya jinai.

Mhe. Ngitiri alieleza kuwa, pamoja na mafanikio hayo, Mahakama imebaini mashauri   nane ya jinai yanayoweza kuwa ya mlundikano  ifikapo Desemba 2026, huku mikakati mahsusi ikiwa tayari imewekwa ili kuhakikisha yanakamilishwa mapema iwezekanavyo.

Katika kikao hicho, Wadau walichangia hoja mbalimbali na walipitisha maazimio kadhaa, yakiwemo kuendelea kutekeleza mikakati ya Jaji Mkuu ya kuharakisha utoaji wa haki, kuyapa kipaumbele mashauri yanayokaribia kuwa ya mlundikano na kuimarisha ushirikiano katika kushughulikia mashauri yanayoweza kumalizika katika hatua za awali.

Aidha, Wadau hao walikubaliana kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya makosa ya mauaji kwa kushirikiana na Viongozi wa dini na Serikali ili kuimarisha kinga dhidi ya uhalifu.

Mhe. Tiganga alisisitiza  kuwa usimamizi madhubuti wa mashauri na ushirikiano wa Wadau wa sekta ya haki jinai ni msingi muhimu wa kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati na kuimarisha imani ya wananchi kwa Mhimili  wa Mahakama.

Meza kuu waliokaa ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga, kulia kwake ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Upendo Ngitiri na kushoto kwake ni Kaimu Mkuu wa Mashtaka kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Dodoma, Bi Bertha Kulwa wakiwa katika kikako.

 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga, ambae pia ni mgeni rasmi akifurahia jambo wakati wa kikao hicho.


 

Meza kuu waliokaa ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Dodoma, Mhe Joachim Tiganga, (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa kikao hicho kutoka ofisi mbalimbali. Kulia kwake waliokaa ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Upendo Ngitiri na kulia kwake ni Kaimu Mkuu wa Mashtaka,Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Dodoma, Bi. Bertha Benedict.


 Meza kuu waliokaa ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Dodoma, Mhe Joachim Tiganga, (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa kikao hicho kutoka ofisi mbalimbali. Kulia kwake waliokaa ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Upendo Ngitiri na kulia kwake ni Kaimu Mkuu wa Mashtaka, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Dodoma, Bi. Bertha Benedict.

 Sehemu ya wajumbe wa kikao hicho wakifuatilia kwa umakini kikao hicho.

 Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni