Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Kibaha
Mahakama ya Wilaya Kibaha imetoa mafunzo ya Mirathi kwa Mahakimu wa Mahakama ya Wilaya na Mahakama za Mwanzo za Wilaya hiyo yakilenga katika maeneo muhimu kuanzia ufunguaji hadi ufungaji wa mashauri ya aina hiyo.
Mafunzo hayo ya siku moja yalifanyika tarehe 03 Julai, 2026 kwenye ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha.
Akizungumza wakati akimkaribisha Mwezeshaji wa Mafunzo hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha Mhe Emmael Lukumai amesema kutokana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo Mahakimu katika usikilizaji wa mashauri ya mirathi,wameona ni vyema wapate mafunzo ambayo yatawaweka sawa ili kutatua changamoto wanazokutana nazo.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye ni Hakimu Mkazi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Mhe.Simon Swai amewaeleza Mahakimu hao kuwa, anapoteuliwa Msimamizi wa Mirathi wamueleze taratibu zote kuepuka usumbufu huku akiwataka Mahakimu kuangalia uhalisia wa mali za marehemu ili waweze kutoa muda wa kufanya hesabu kutokana na wingi au uchache wa mali hizo.
"Mfano marehemu alikuwa na mali NSSF tu haihitaji muda mrefu sana wiki tatu tu zinatosha," alisema Mhe. Swai huku akiongeza kuwa, miongoni mwa maeneo hayo ni pamoja na kutambua kama hayo ni maombi ya Mirathi au ni maombi ya barua ya kusimamaia mirathi pamoja fomu zake, Mamlaka ya Mahakama kusikiliza shauri hilo, mchakato wa mapingamizi wakati wa uteuzi wa Msimamizi wa mirathi, uteuzi, uwasilishaji wa hesabu za mali za marehemu, usikilizwaji wa mapingamizi, akaunti maalum ya mirathi, kuhamisha umiliki wa mali za marehemu kwenda kwa warithi na ufungaji wa mirathi.
Aidha, Mhe. Lukumai amemshukuru Mhe. Swai kwa kukubali mwaliko huo wa kufika Mahakamani hapo kutoa mafunzo hayo na kukiri kwamba wamefurahi kwakuwa kulikuwa na changamoto wanazokumbana nazo na wameweza kupata ufumbuzi.
Hakimu Mkazi kutoka Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Mhe. Simon Swai akiwafundisha Mahakimu wa Mahakama ya Wilaya na wa Mwanzo Kibaha namna bora ya usikilizwaji wa mashauri ya mirathi tarehe 03 Julai, 2026 kwenye ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni