Na. MUKSINI NAKUVAMBA - Mahakama, Mbeya
Mahakama
ya Wilaya ya Mbeya imefanya kikao kazi kilichowakutanisha Mahakimu wa Mahakama
za Mwanzo zilizopo jijini Mbeya kwa lengo la kusisitiza uimarishaji wa maadili,
uwajibikaji na kuzingatia ubora wa utoaji wa huduma za Mahakama sambamba na
kujadili changamoto zinazojitokeza katika ushughulikiaji wa malalamiko na
uandaaji wa kumbukumbu za mashauri ya rufaa.
Kikao
hicho kiliitishwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya Mhe.
Tedy Mlimba na kuwashirikisha viongozi kutoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya
Mbeya, walitoa maelekezo na miongozo kadhaa ya utendaji kazi kwa Maafisa
Mahakama wakiwa katika vituo vyao.
Viongozi
walioshiriki kikao kazi hicho ni Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala
Ndogo ya Mbeya, Mhe. Benard Mpepo, Naibu Msajili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya,
Mhe. Zawadi Laizer na Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Bw.
Festo Chonya.
Akizungumza
katika kikao hicho, Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya
Mbeya, Mhe. Benard Mpepo aliwataka Mahakimu kuendelea kudumisha nidhamu,
uadilifu na uzingatiaji wa sheria katika kila hatua ya utekelezaji wa majukumu
yao. Alisisitiza kuwa utoaji wa haki unapaswa kuongozwa na misingi ya haki,
uwazi na weledi ili kulinda hadhi ya Mahakama.
“Mahakama
ina jukumu la kumfuta machozi mtu aliyedhurumiwa haki zake na nasisitiza kuwa
kila shauri linapaswa kushughulikiwa kwa umakini, usawa na kwa kuzingatia
sheria ili kuhakikisha haki inatendeka na kuonekana kutendeka,” alisema Mhe.
Mpepo.
Kwa
upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Mhe. Zawadi
Laizer, aliwahimiza Mahakimu kuendelea kuzingatia maadili ya kazi, kuwahudumia
wananchi kwa weledi na kwa lugha yenye staha, pamoja na kutekeleza kwa vitendo
maelekezo yanayotolewa na viongozi kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma za Mahakama.
Naye, Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Bw. Festo Chonya, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano, kuheshimiana na kujenga mahusiano mazuri mahali pa kazi. Pia aliwakumbusha Maofisa hao kutunza afya zao, akieleza kuwa afya njema ni msingi wa utendaji bora na huchangia katika kulinda na kutunza rasilimali za Mahakama na kuongeza ufanisi wa taasisi kwa ujumla.
Maofisa
Mahakama katika kikao hicho, walikumbushwa umuhimu wa kuzingatia maadili ya
utumishi wa umma, missing ya taaluma inayoongoza kazi zao na kuhakikisha kuwa
majukumu yao yanatekelezwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu
zilizowekwa.
Pamoja
na hayo, washiriki walijadili mbinu za kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi
ili kuongeza ufanisi na kuimarisha imani ya jamii kwa Mhimili wa Mahakama.
Aidha,
Viongozi hao walisisitiza na kuhimiza Maofisa hao kuhakikisha wananchi
wanapatiwa nakala za hukumu na mwenendo wa mashauri kwa wakati, matumizi sahihi
ya mifumo ya TEHAMA katika utekelezaji wa majukumu ya kimahakama, kuzingatia
mipaka ya mamlaka hayo wakati wa kusikiliza mashauri na kufuata sheria na
kanuni katika utekelezaji wa tuzo na amri za Mahakama.
Mahakama
ya Tanzania inaendelea kuimarisha uwezo wa watumishi wake kupitia mafunzo ya
ndani na vikao vya kitaalamu vinavyolenga kuboresha utendaji kazi, kuimarisha
maadili na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za haki zenye ubora, kwa wakati
na kwa kuzingatia misingi ya sheria na haki.
Meza Kuu ikiongozwa na Naibu Msajili Mfawidhi wa
Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Benard Mpepo (wa pili kushoto) na Viongozi
wengine kutoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya wakiwa kwenye picha ya
pamoja na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo jijini Mbeya.
Meza Kuu ikiongozwa na Naibu Msajili Mfawidhi wa
Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Benard Mpepo (wa pili kushoto) na Viongozi
wengine kutoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya wakiwa kwenye picha ya
pamoja na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo jijini Mbeya.
Viongozi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya wakiwa
kwenye picha ya pamoja wakati wa kikao hicho, kulia ni Naibu Msajili wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Mhe. Zawadi Laizer, (wa pili kulia) ni Naibu Msajili
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Benard Mpepo, (wa pili
kushoto) ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Bw. Festo Chonya
na kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya Mhe. Tedy
Mlimba.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni