Jumanne, 28 Julai 2026

MASJALA NDOGO GEITA YAFANYA KIKAO CHA MENEJIMENTI

Na. DOTTO NKAJA – Mahakama, Geita

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Geita, Mhe. Projestus Kahyoza, amewataka watumishi wa Mahakama kuongeza ubunifu na uwajibikaji ili kuleta tija katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za utoaji haki kwa wakati.

Wito huo ametolewa wakati akifungua kikao cha Menejimenti cha Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Geita, kilichofanyika hivi karibuni, katika ukumbi wa mafunzo uliopo Kituo Jumuishi cha utoaji haki mjini Geita.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kahyoza alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha viongozi na watumishi kukutana kwa lengo la kutathmini utendaji wa kazi wa Mahakama na kujadili mbinu bora za kuendelea kuboresha utoaji wa haki kwa wananchi.

Mhe. Kahyoza alisema kuwa, kikao hicho ni muhimu kwa kuwa kinatoa fursa ya kutathmini utekelezaji wa majukumu, kubaini mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya kuongeza ufanisi katika maeneo yanayohitaji maboresho.

Alieleza kuwa, pamoja na kikao hicho kuwa sehemu ya utaratibu wa kisheria wa Mahakama, umuhimu wake unakwenda mbali zaidi ya kutekeleza matakwa ya kisheria, kwani kinatoa nafasi ya kutafakari namna ya kuifanya Mahakama iendelee kupiga hatua katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Jaji Kahyoza alisisitiza kuwa, utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama unapaswa kuzingatia maslahi mapana ya wananchi wa Mkoa wa Geita na Tanzania kwa ujumla. Alibainisha kuwa kila mtumishi anapaswa kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi na viwango vya juu vya weledi.

“Ni muhimu kila mmoja wetu kutathmini tumefanikiwa kwa kiwango gani, ni maeneo yapi tunasuasua na ni hatua zipi tunapaswa kuchukua ili kuhakikisha shughuli zetu zinaendelea kufanyika kwa ufanisi zaidi,” alisema Jaji Kahyoza.

Nao, Wakuu wa vitengo pamoja na Viongozi wa Utawala kutoka Mahakama za Wilaya na Mahakama Kuu waliwasilisha taarifa za maeneo yao ya kiutendaji.

Wajumbe walipata nafasi ya kujadili taarifa mbalimbali zilizowasilishwa, huku mijadala ikijikita katika namna ya kuongeza ubunifu na tija katika uendeshaji wa shughuli za Mahakama, hususan kuimarisha usikilizaji na utoaji wa maamuzi ya mashauri kwa wakati.

Miongoni mwa changamoto zilizojadiliwa ni uchakavu wa baadhi ya majengo ya Mahakama pamoja na kuwepo kwa fedha za mirathi ambazo hazijachukuliwa na wanufaika wake.

Taarifa ya Mashauri ilionesha Mahakama zote kufanya vizuri kwa kipindi cha Machi mpaka Juni 30, 2026. Mashauri ya Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi, na Wilaya zote hazikuwa na shauri la mlundikano kwa mashauri yaliyofunguliwa mwaka 2025.

Pongezi pia zilienda Mahakama za Mwanzo kwa kuendelea kuondosha Mashauri kwa wakati kwani Mahakama zote zina wastani wa siku 9 wa umri wa shauri kukaa mahakamani.

Hata hivyo, kikao kilibaini kuwa bado kuna changamoto kuhusu fedha za mirathi, ambapo baadhi ya fedha hizo zimeendelea kubaki bila kuchukuliwa kutokana na kutopatikana kwa wanufaika au baadhi yao kukataa kuzichukua kwa madai kuwa kiasi kilichopo ni kidogo.

Wajumbe kutoka Mahakama za Wilaya za Chato, Geita, Bukombe, Mbogwe na Nyang'hwale walieleza kuwa changamoto hiyo imeendelea kujitokeza katika maeneo yao. Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti alisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za haraka ili kupata suluhisho la kudumu.   

Katika kikao hicho, wajumbe walichangia umuhimu wa kuendelea kutafuta viwanja na kuvipatia hati angalau viwanja viwili kwa kila Halmashauri. Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Geita Bi. Masalu Kisasila asisitiza kuwa, hatua hiyo ni muhimu katika kuwezesha upatikanaji wa miradi ya maendeleo na kulinda mali za Mahakama.

Kutokana na umuhimu wa suala hilo, Mwenyekiti wa kikao hicho alielekeza kuwa, ifikapo Septemba 30, 2026, viwanja na majengo yote ya Mahakama ambayo bado hayana hati miliki viwe vimekamilisha taratibu za umiliki.

Aidha, viongozi wa Mahakama waliagizwa kushirikiana kwa karibu na Wakurugenzi wa Halmashauri katika maeneo yao ili kutatua kwa wakati changamoto zinazohusu miundombinu pamoja na masuala mengine ya kiutendaji.

Mhe. Kahyoza alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Mahakama na taasisi nyingine za Serikali, akieleza kuwa ushirikiano huo ni nguzo muhimu katika kuhakikisha mipango ya maendeleo ya Mahakama inatekelezwa kwa ufanisi na huduma kwa wananchi zinaendelea kuimarika.

Mhe. Kahyoza alisisitiza kuwa, ubunifu, uwajibikaji, matumizi bora ya rasilimali na tathmini ya mara kwa mara ya utekelezaji wa mipango ni nguzo muhimu za kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za Mahakama. Alieleza kuwa hatua hizo zitawezesha Mahakama kuendelea kuboresha mazingira ya utendaji, kuharakisha usikilizaji wa mashauri na kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kwa ufanisi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Geita, Mhe. Projestus Kahyoza (kulia) akiwa anaongoza kikao cha menejimenti Mahakama Kuu Masjala Ndogo Geita.

Mhasibu wa Mahakama Kuu Geita, Bw. Goodluck Machange akiwasilisha Taarifa ya utekelezaji wa Fedha.

Sehemu ya washiriki wa kikao cha menejiment Masjala Ndogo ya Geita.

Afisa Ugavi wa Mahakama Kuu Geita, Bw. Abel Bunzali akiwasilisha Taarifa ya utekelezaji wa robo ya nne ya mwaka 2025/2026.

Meza Kuu katika kikao cha menejimenti, aliyesimama ni Katibu wa kikao, Bi. Masalu kisasila, katikati ni Mwenyekiti wa Kikao, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Geita, Mhe. Projestus Kahyoza na kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Mhe. Fredrick Lukuna.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni