Mhe. Kakusulo Mwakipome Mbutolwe Sambo enzi za uhai wake.
TANZIA
Mahakama
ya Tanzania inasikitika kutangaza kifo cha Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Kakusulo Mwakipome Mbutolwe Sambo, kilichotokea tarehe 26 Julai, 2026 jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa, marehemu Jaji Kakusulo anatarajiwa kuzikwa tarehe 31 Julai, 2026 Kiwila Tukuyu mkoani Mbeya.
Marehemu Jaji Kakusulo aliajiriwa na Mahakama ya Tanzania tarehe 04 Februari, 1989 kama Hakimu Mkazi Daraja III na kuapishwa tarehe 04 Februari 1989 mbele ya aliyekuwa Jaji Mkuu, Marehemu Francis Nyalali.
Katika maisha yake Jaji Sambo aliitumikia Mahakama
ya Tanzania kama Hakimu Mkazi kwenye Mikoa ya Iringa, Mbeya, na pia aliteuliwa
mnamo tarehe 04 Mei, 1994 kuwa Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Nyumba, Mkoa wa
Mbeya ambapo alitumikia kwa miaka zaidi ya mitatu.
Hata hivyo, aliteuliwa kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mkoa wa Ruvuma mnamo tarehe 05 Julai, 1993 na kutumikia cheo hicho katika Mkoa
wa Arusha baada ya kuteuliwa mnamo tarehe 01 Januari, 2000.
Marehemu Jaji Sambo aliteuliwa kukaimu Ofisi ya Msajili wa wilaya Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha na baadae mnamo tarehe 02 Novemba, 2001 aliteuliwa kuwa Msajili wa Wilaya (District Registrar) na kupangiwa kutumika katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Tanga.
Aidha, alitumikia kituo hicho kwa
weledi mkubwa na kujitolea kwa moyo wake wote na mamlaka za uteuzi ziliona kazi
yake iliyotukuka akiwa Hakimu Mkazi Mwandamizi na ndipo mnamo tarehe 28 Novemba, 2006 aliteuliwa kuwa Naibu Mwenyekiti wa Mahakama ya Kazi (Deputy Chairman,
Industrial Court).
Jaji Sambo aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania tarehe 18 Desemba, 2006 na alihudumu kwa uadilifu na weledi
mkubwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo za Bukoba, Arusha nafasi hiyo na mnamo tarehe 18 Februari, 2013 aliteuliwa kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga na hadi
alipostaafu mnamo 01 Mei, 2016. Na hata baada ya kustaafu kama Jaji wa Mahakama
Kuu, bado tuliendelea kushirikiana nae katika masuala mbalimbali ya kitaasisi
na kitaifa kwa ujumla.
Kufuatia msiba huo mzito, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemtumia salamu za rambirambi Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano-Ikulu leo tarehe 27 Julai, 2026.
Aidha, Mahakama ya Tanzania inaungana na Ndugu, Jamaa na Marafiki kuomboleza msiba huo mzito wa kuondokewa na Mpendwa wetu.
BWANA
ALITOA, BWANA AMETWAA JINA LAKE LIHIMIDIWE.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni