Jumatatu, 27 Julai 2026

WATUMISHI MBEYA WANOLEWA NAMNA BORA YA UANDAAJI KUMBUKUMBU ZA RUFAA MASHAURI YA JINAI

Na. MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya

Watumishi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya wamehitimisha mafunzo ya siku mbili ya namna bora ya kuandaa kumbukumbu za rufaa za mashauri ya jinai, yaliyofanyika hivi karibuni jijini Mbeya yakilenga kuimarisha ufanisi katika uandaaji wa nyaraka na kumbukumbu za Mahakama ya Rufani.

Mafunzo hayo yalifunguliwa na Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Benard Mpepo, ambaye alisisitiza umuhimu wa watumishi wa kada zote kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu taratibu za uandaaji wa kumbukumbu za rufaa na kuongeza kuwa, ubora wa uandaaji wa nyaraka za Mahakama ni msingi muhimu wa utoaji wa haki kwa wakati.

Washiriki wa mafunzo hayo walitoka kada mbalimbali ikiwemo Mahakimu, wasaidizi wa kumbukumbu, waandishi waendesha ofisi, wasaidizi wa ofisi na walinzi, hatua inaonesha dhamira ya Mahakama ya kuwajengea uwezo watumishi wote ili kuboresha utendaji kazi wa taasisi.

Akitoa mada katika mafunzo hayo, Hakimu Mkazi wa Mahakama Kuu Mbeya, Mhe. Hassan Yahaya Mbojellah, aliwaelekeza washiriki kuhusu taratibu na mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kuandaa kumbukumbu za Mahakama ya Rufani kwa mashauri ya jinai.

Alifafanua tofauti za uandaaji wa kumbukumbu kwa mashauri yanayotoka Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi, pamoja na mashauri yenye asili ya Mahakama Kuu.

Mbali na mafunzo ya nadharia, washiriki walipata fursa ya kujifunza kwa vitendo kupitia kazi za makundi, ambapo waliandaa kumbukumbu za rufaa na vitabu mbalimbali vya Mahakama ya Rufani kwa kutumia mifano halisi. Mbinu hiyo iliwawezesha kuongeza uelewa na umahiri katika kuandaa nyaraka kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.

Kwa upande wao, washiriki walieleza kuridhishwa na mafunzo hayo na kuomba yawe endelevu, wakisema yatawasaidia kuongeza uelewa kuhusu masuala ya mashauri, uandaaji na utunzaji wa kumbukumbu za mahakama.

Washiriki wa mafuzo hayo walisisitiza kuwa, kwa kuwa mashauri ndiyo kiini cha shughuli za Mahakama, mafunzo ya mara kwa mara yataongeza ubora wa huduma na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya za kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wake, kuboresha usimamizi wa mashauri na kuhakikisha nyaraka na kumbukumbu za Mahakama ya Rufani zinaandaliwa kwa usahihi kwa kuzingatia weledi, taratibu na viwango vinavyotakiwa.

Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Benard Mpepo akifungua mafunzo ya siku mbili ya namna bora ya kuandaa kumbukumbu za rufaa za mashauri ya jinai kwa watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeyav (hawapo pichani).

Mtoa mada katika mafunzo hayo Hakimu Mkazi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Hassan Yahaya Mbojellah (aliyesimama) akitoa madini katika mafunzo hayo.

Mtoa mada katika mafunzo hayo Hakimu Mkazi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Hassan Yahaya Mbojellah (aliyesimama) akitoa madini katika mafunzo hayo.

Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Bw. Alintula Watson Ngalile (aliyesimama) akizungumza katika mafunzo hayo, kulia ni Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Benard Mpepo.

Msaidizi wa Ofisi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Bi. Editha Exavery Mhiliwa (aliyesimama) akieleza kwa muhtasari mada zilizofundishwa katika siku ya kwanza ya mafunzo hayo.

Sehemu ya Watumishi walioshiriki katika Mafunzo hayo. 

Sehemu ya Watumishi walioshiriki katika Mafunzo hayo. 

Sehemu ya Watumishi walioshiriki katika Mafunzo hayo. 

Sehemmu ya washiriki katika mafunzo hayo wakiwa kwenye makundi wakifanya kwa vitendo yale waliyojifunza ambapo ilikuwa ni sehemu ya mafunzo hayo.



 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni