Na. SHARIFU MOKIWA - Mahakama, Sumbawanga
Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya
Sumbawanga imetoa Mafunzo maalum kwa Mahakimu yaliyolenga kuimarisha uwezo wao katika kushughulikia mashauri
yanayohusisha ushahidi wa kielektroniki pamoja na kuwakumbusha kuendelea kuzingatia
maadili ya kimahakama katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mafunzo hayo yalifunguliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Frederick Kapela Manyanda na kujumuisha
Mahakimu Wakazi 27 kutoka Wilaya za Kalambo, Sumbawanga na Nkasi ili kuwajengea washiriki hao uelewa wa pamoja
kuhusu uchukuaji wa ushahidi wa kielektroniki, kanuni zinazosimamia upokeaji na tathmini ya
ushahidi huo mahakamani.
Aidha, Mafunzo hayo yalijikita katika kuondoa
dosari na makosa ya
kawaida yanayoweza kujitokeza wakati wa kushughulikia ushahidi wa kidijiti, pamoja na mbinu bora za kuhakikisha ushahidi
huo unatumika kwa usahihi na kwa kuzingatia sheria wakati wote wa
uendeshaji mashauri yanayohusu matumizi hayo.
Kupitia Mada mbalimbali, washiriki walijadili changamoto
zinazotokana na maendeleo ya teknolojia katika utoaji wa haki na namna Mahakama zinavyoweza kuendana na mabadiliko
hayo. Washiriki walisisitizwa umuhimu wa kuendelea kujenga uwezo
wa Mahakimu katika masuala ya TEHAMA ili kuongeza
ufanisi katika utoaji wa maamuzi yenye haki na yanayozingatia ushahidi wa
kisasa.
Mbali na mada za
ushahidi wa kielektroniki, mafunzo hayo pia yaliendeshwa kwa njia ya mkutano mtandao
kwenye mada iliyowasilishwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania, Masjala Ndogo ya Simiyu Mhe. Wilbert Martin
Chuma ambaye
alitoa mada kuhusu Utamaduni na Maadili ya Mahakama kwa Mahakimu hao (Judicial Ethics and
Culture). Katika
wasilisho hilo, alielezea umuhimu wa maadili ya kimahakama katika kujenga na
kuimarisha imani ya wananchi/umma kwa Mhimili wa Mahakama.
Aidha, Mhe. Chuma alisisitiza kuwa, maadili ya kimahakama yanapaswa kuonekana si tu katika maamuzi
yanayotolewa bali pia katika mwenendo, mawasiliano na utendaji kazi wa kila siku wa Hakimu.
Mhe. Chuma aliongeza kwa kusema kwamba, utamaduni mzuri wa kimahakama hujengwa
kupitia weledi, uadilifu na uwajibikaji kwa kuzingatia misingi iyokuwa na upendeleo, kuheshimu sheria na kuendelea kujifunza na kujielimisha mambo mapya ya kisheria
yanayojitokeza mara kwa mara ili kuendana na mabadiliko ya mazingira ya utoaji wa haki.
Washiriki walipata nafasi ya kuuliza maswali, kubadilishana uzoefu na
kujadili mifano mbalimbali ya vitendo kuhusu matumizi ya ushahidi wa
kielektroniki pamoja na masuala ya maadili katika utoaji wa haki. Majadiliano
hayo yalichangia kuongeza uelewa na kutoa mbinu za kukabiliana na changamoto
zinazojitokeza katika mazingira ya sasa ya kidijitali.
Mafunzo hayo
yametumika kama jukwaa
la kuimarisha
uwezo wa Mahakimu katika matumizi sahihi ya ushahidi wa
kielektroniki na kuwakumbusha umuhimu wa kuendelea kuzingatia maadili ya
kimahakama kama msingi bora wa utoaji
haki wenye ufanisi, uwazi na unaojenga imani kwa wananchi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Frederick Kapela Manyanda (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na Washiriki wa mafunzo ya Ushahidi wa Kielekroniki na Maadili ya kimahakama.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala
Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Frederick Kapela Manyanda akizungumza wakati wa kufungua
mafunzo maalum kwa Mahakimu yaliyolenga
kuimarisha uwezo wao katika kushughulikia mashauri yanayohusisha ushahidi wa
kielektroniki.
Viongozi walioshiriki katika Mafunzo hayo,
(kushoto) ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Sumbawanga
Mhe. Frederick Kapela Manyanda, (katikati) ni Mtendaji wa Mahakama Kuu, Masjala
Ndogo ya Sumbawanga Bw. Machumu Essaba na kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu,
Masjala Ndogo ya Sumbawanga, Mhe. Pamela Mazengo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Masjala Ndogo Sumbawanga Mhe. Frederick Kapela Manyanda (katikati aliyesimama) akijibu
Maswali yaliyo ulizwa na washiriki wa Mafunzo hayo ya Ushahidi wa
Kielektroniki.
Waheshimiwa Mahakimu wakiwa katika ukumbi wa Mahakama Kuu Sumbawanga, wakifatilia kwa umakini mafunzo hayo yaliyo kuwa yakitolewa.
Televisheni ikionesha Mkutano mtandao wakati
wa mafunzo hayo yaliyokuwa yakiwasilishwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Masjala Ndogo ya Simiyu Mhe. Wilbert Martin Chuma.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni