Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile, amewaongoza
wajumbe wa kikao cha Kamati ya Uongozi ya Mahakama kushuhudia mchezo wa mpira
wa miguu wa kirafiki kati ya Timu ya Mahakama Sports Kigoma na Timu ya Halmashauri
ya Wilaya ya Uvinza.
Mchezo huo uliofanyika
hivi karibuni katika Uwanja wa Shule ya Msingi Rugufu, ulikuwa na lengo la
kuimarisha na kudumisha ushirikiano pamoja na mahusiano mema kati ya Mahakama
na wadau wake katika Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.
Katika mchezo huo, kikosi
cha Mahakama Sports Kigoma kiliongozwa na Kapteni wake, Bw. Omary Magege.
Akizungumza kabla ya
kuanza kwa pambano hilo, Kocha wa Timu ya Mahakama Sports Kigoma, Bw. Ramadhan Kufakunoga
aliwahimiza Wachezaji wake kucheza kwa kujituma na nidhamu ya hali ya juu.
"Wachezaji wenzangu chezeni
mpira kwa kujituma maana bidii yenu ndiyo itakayofikia malengo ya kuwa washindi
wa mechi hii. Hata hivyo, matokeo yanapatikana baada ya dakika 90, hivyo
chezeni bila kusababisha majeruhi kwa timu pinzani kwa kuwa hii ni mechi ya
kirafiki," alisema Bw. Kufakunoga.
Kocha huyo aliongeza kuwa,
mchezo huo ni sehemu ya kupima uwezo wa timu yake ili kubaini na kurekebisha
mapungufu kabla ya kushiriki michuano mingine inayoratibiwa na Viongozi wa
Mahakama Sports Kigoma.
Kwa upande wake, Jaji
Mfawidhi, Mhe. Rwizile alisisitiza umuhimu wa mchezo huo katika kujenga afya na
kuimarisha mahusiano ya kiutendaji.
Alisema, "Mechi hii
ni ya kuimarisha mahusiano, hivyo chezeni kwa furaha, hii ni sehemu ya kujenga
afya zenu na tunategemea burudani nzuri kupitia ushindani wa mechi hii."
Baada ya dakika 90 za
mchezo huo, Timu ya Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza ilifanikiwa kuibuka na
ushindi wa bao 2-0 dhidi ya Timu ya Mahakama Sports Kigoma.
Licha ya kufungwa, benchi
la ufundi la Mahakama Sports lilieleza kuwa matokeo hayo yamekuwa kipimo kizuri
cha kubaini maeneo yanayohitaji uboreshaji ili kujenga timu imara zaidi kwa
ajili ya mechi zijazo.
Waliohudhuria walipongeza kiwango cha nidhamu, utulivu na weledi kilichooneshwa na timu zote mbili katika kufanikisha malengo ya mchezo huo.
Mchezo huo ulihudhuriwa pia na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Uvinza, Wajumbe wa Kikao cha Uongozi pamoja na wananchi waliojitokeza kushuhudia.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile akitoa mkono wa salamu kwa vikosi vya Timu ya Mahakama Sports Kigoma na Timu ya Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza kabla ya mechi kuanza hivi karibuni.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (wa pili kulia), Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma (wa kwanza kulia), Mhe. John Francis Nkwabi pamoja na wajumbe wa Kikao cha Uongozi wa Mahakama Kigoma wakifuatilia mechi iliyokuwa ikiendelea baina ya Timu ya Mahakama Sports Kigoma na Timu ya Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza iliyochezwa, katika uwanja wa Shule ya Msingi Rugufu mara baada ya kikao chao kumalizika.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (wa 10 kulia aliyevaa shati jeupe) akiwa katika picha ya pamoja ya Wachezaji wa Timu ya Mahakama Sports Kigoma (kulia)na Timu ya Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe.John Francis Nkwabi (wa kwanza kulia), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa Kigoma, Mhe. Aristida Valerian Tarimo na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya za Kigoma Uvinza, Buhigwe na Kibondo.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni