Na LIGHTNESS KABAJU-Mahakama ya Kazi, Dar es Salaam
Mtendaji Mkuu
wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Jingu, amefanya ziara katika Mahakama Kuu ya
Tanzania Divisheni ya Kazi, ikiwa ni ziara yake ya kwanza katika Mahakama hiyo
tangu ateuliwe na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushika wadhifa
huo.
Dkt. Jingu
aliambatana na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, pamoja na Katibu
wa Mtendaji Mkuu, Bw. Thomas Mdenya na Katibu wa Msajili Mkuu, Mhe. Jovin
Bishanga.
Ziara hiyo
ililenga kujitambulisha rasmi kwa watumishi, kufahamu mwenendo wa utekelezaji
wa majukumu na kusikiliza changamoto zinazowakabili katika mazingira yao ya
kazi.
Akizungumza
wakati wa ziara hiyo, Dkt. Jingu alisema ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za
uongozi wa Mahakama kuendelea kuwa karibu na watumishi na kupata uelewa wa moja
kwa moja kuhusu changamoto wanazokutana nazo katika kutekeleza majukumu yao.
Alisisitiza
umuhimu wa watumishi kushirikiana na uongozi katika kutafuta suluhisho la
changamoto hizo, huku wakizingatia wajibu wao wa kutoa huduma bora, kwa wakati
na kwa weledi kwa wananchi.
Katika kikao
hicho, watumishi walipata fursa ya kuwasilisha changamoto, hoja na mapendekezo
mbalimbali yanayohusu mazingira ya kazi na utekelezaji wa majukumu yao. Dkt.
Jingu aliahidi kuzifanyia kazi kwa kuzingatia taratibu na mamlaka zilizopo.
Kwa upande
wake, Msajili Mkuu aliwasihi watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii,
uadilifu na kujituma katika kutekeleza majukumu yao. Alisisitiza umuhimu wa
kudumisha upendo, mshikamano na misingi ya kazi, akieleza kuwa ushirikiano
miongoni mwa watumishi ni muhimu katika kufanikisha malengo ya Mahakama.
Ziara hiyo
imeendelea kuonesha dhamira ya uongozi wa Mahakama ya Tanzania ya kuwa karibu
na watumishi, kusikiliza changamoto zao na kuweka mazingira bora ya utendaji
kazi.
Dhamira hiyo inaenda sambamba na jukumu la Mahakama la kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya haki mapema ipasavyo, kwa ufanisi na kwa kuzingatia misingi ya haki na utawala wa sheria.
Mtendaji Mkuu
wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Jingu,
akizungumza na watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi (juu na chini).
Mtumishi wa Mahakama
Kuu Divisheni ya Kazi akitoa hoja kwenye kikao hicho.
Meza Kuu inayoongozwa
na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Jingu (katikati).
Picha ya Meza
Kuu inayoongozwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Jingu (katikati
waliokaa) na Viongozi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.
Picha ya Meza
Kuu inayoongozwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Jingu (katikati
waliokaa) na watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi (juu na chini).
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni