Na MWANDISHI WETU-Mahakama, Dar es Salaam
Mtendaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Jingu, tarehe 26 Agosti, 2026 alifanya ziara
katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo cha Usuluhishi pamoja na Mahakama Kuu Divisheni
ya Ardhi kwa lengo la kujitambulisha.
Ziara hiyo imekuwa ya
kwanza kufanyika tangu ateuliwe na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kushika wadhifa huo.
Lengo lingine lilikuwa
kufahamu kwa kina utekelezaji wa majukumu ya Mahakama hizo, kutathmini
mafanikio yaliyopatikana pamoja na kubaini changamoto zilizopo katika
utekelezaji wa majukumu.
Akizungumza na
watumishi, Dkt. Jingu aliwasisitiza kuwa na upendo, mshikamano na kufanya kazi
kwa ushirikiano ili kuhakikisha Mahakama inaendelea kutoa huduma bora na kwa
ufanisi kwa wananchi.
Alisisitiza umuhimu wa
watumishi kushirikiana katika kutatua changamoto na kutekeleza majukumu yao kwa
weledi, uadilifu na kujituma.
Katika ziara hiyo, Mtendaji Mkuu aliambatana na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, ambaye aliwapongeza watumishi kwa kazi nzuri wanayoifanyika na kusisitiza umuhimu wa kutenga muda kwa ajili ya kufanya mazoezi ya mwili ili kuimarisha afya na ustawi wao wanapotekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Mhe. Nkya pia aliwahimiza watumishi wa Mahakama hizo kuiishi salamu ya Mahakama inayosisitiza uadilifu, weledi na uwajibukaji katika kazi na kuwataka kuwa na maadili na matumizi ya lugha nzuri wanapowahudumia wananchi.
Naye Kaimu Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Isaya Arufani, alimshukuru Mtendaji
Mkuu kwa kufanya ziara hiyo, kufanya majadiliano na watumishi na kuahidi kuzifanyia
kazi changamoto zilizowasilishwa.
Ziara hiyo imekuwa muhimu katika kuimarisha mawasiliano, ushirikiano na uongozi kati ya watumishi na uongozi wa Mahakama ya Tanzania, pamoja na kuweka msisitizo katika utoaji wa huduma bora na ufanisi wa Mahakama.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, akizungumza akiwa katika Ofisi ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, Bw. Donald Makawia, akitoa utambulisho wakati wa kikao hicho.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, akizungumza wakati wa kikao hicho. Katikati ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Njingu na kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Niku Mwakatobe (kulia) akichukua kumbukumbu muhimu wakati wa kikao hicho.
Sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi na Divisheni ya Ardhi (juu na chini), wakimsiliza Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Njingu (hayupo katika picha).













Hakuna maoni:
Chapisha Maoni