Ijumaa, 28 Agosti 2026

WATUMISHI MBEYA WAZURU MAKAO MAKUU, TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA

Na MUKSINI NAKUVAMBA - Mahakama, Mbeya

Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Mbeya wamefanya ziara ya kikazi ya kuzuru Makao Makuu ya Mahakama na Tume ya Utumishi wa Mahakama jijini Dodoma, kwa lengo la kuongeza uelewa wa masuala ya kiutumishi, kujifunza mifumo ya uendeshaji wa shughuli Mahakama na kubadilishana uzoefu ili kuimarisha utendaji kazi na utoaji wa huduma.

Ziara hiyo imeongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Fahamu Mtulya, akiambatana na Viongozi pamoja na watumishi.

Aidha, Watumishi hao walipata fursa ya kujifunza kwa kina kuhusu masuala yanayohusu utumishi ndani ya Mahakama, ikiwemo utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayosimamia utendaji wa Mahakama.

Aidha, watumishi hao walitembelea Ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama, ambako walipata maelezo kuhusu majukumu ya Tume, hususan katika usimamizi wa masuala ya rasilimali watu, nidhamu, maadili na maendeleo ya watumishi wa Mahakama.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Naibu Katibu Tume ya Utumishi wa Mahakama anayeshughulikia Nidhamu na Maadili, Bi. Alesia Mbuya, aliwakaribisha watumishi hao na kuwapongeza kwa kutenga muda wa kutembelea Ofisi za Tume, akieleza kuwa, ziara hizo ni muhimu katika kuongeza uelewa na kuimarisha ushirikiano pamoja na kubadilishana uzoefu katika masuala ya kiutumishi.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Fahamu Mtulya, alieleza umuhimu wa watumishi kupata fursa za kujifunza kutoka katika maeneo mbalimbali ya Mahakama, akisisitiza kuwa maarifa na uzoefu unaopatikana kupitia ziara hizo ni muhimu katika kuboresha utendaji kazi wa kila siku.

Mbali na Ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama, watumishi hao walitembelea maeneo mbalimbali ya kimkakati katika Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, ambako walijifunza namna matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inavyotumika katika kurahisisha na kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Mahakama.

Miongoni mwa maeneo yaliyotembelewa ni ukumbi mpya wa mikutano ulioandaliwa kwa mifumo ya kisasa ya TEHAMA, ambapo watumishi hao walijionea namna teknolojia inavyowezesha uendeshaji wa mikutano, mafunzo na shughuli mbalimbali za kitaasisi kwa ufanisi.

Vilevile, walitembelea Chumba cha Mifumo ya TEHAMA, ambacho ni miongoni mwa maeneo muhimu katika miundombinu ya kiteknolojia iliyopo ndani ya Jengo la Makao Makuu ya Mahakama. Katika eneo hilo, watumishi walipata maelezo kuhusu uratibu, usimamizi na uendeshaji wa mifumo ya TEHAMA inayosaidia shughuli za Mahakama.

Ziara hiyo pia iliwapa watumishi hao fursa ya kutembelea Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dodoma, ambako walipokelewa na na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga.

Mhe. Tiganga, aliwashukuru watumishi hao kwa dhamira yao ya kuendelea kuimarisha ushirikiano, kujenga molari ya utendaji kazi kwa watumishi, matumizi ya teknolojia, uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi, kwa kuweka mkazo katika kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuendeleza rasilimaliwatu kama msingi wa ufanisi.

Viongozi na Watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya wakiwa Mbele ya jengo la Tume ya Utumishi wa Mahakama walipotembelea katika ziara hiyo.

Viongozi na Watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya wakiwa kwenye picha ya pamoja na mwenyeji wao Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dodoma Mhe, Joachim Tiganga, Mbele ya jengo la Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dodoma walipotembelea katika ziara hiyo.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja viongozi wa Masjala hiyo walipotembelea Mahakama Kuu Masjala Ndogo wa Dodoma.




Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (aliyesimama mbele) akizungumza na watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya walipotembelea ofisi ya Tume ya utumishi wa Mahakama

Viongozi na Watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya wakiwa ndani ya ukumbi mpya wakisasa uliopo ndani ya Jengo la Makao Makuu ya Mahakama.

Viongozi na Watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya wakiwa Mbele ya jengo la Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni