Ijumaa, 28 Agosti 2026

WATUMISHI WA MAHAKAMA ARUSHA WAPATIWA MAFUNZO YA NAMNA YA KUPAMBANA NA MAJANGA YA MOTO

Na SETH KAZIMOTO – Mahakama Arusha

Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Arusha wamepatiwa mafunzo ya namna ya kupambana na Majanga ya Moto mahali pa kazi.  

Mafunzo hayo yalifunguliwa hivi karibuni na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Arusha, Mhe. Frank Mahimbali ambapo alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwakuwa, yanasaidia kuokoa maisha ya wafanyakazi.

Akizungumzia suala la kupambana na majanga ya moto, Jaji Mahimbali alisema pia, mafunzo ya kupambana na majanga ya moto mahali pa kazi ni jambo muhimu kwa sababu, kulinda mali za Taasisi, na kupunguza hasara kubwa za kiuchumi zinazoweza kusababishwa na ajali za moto za ghafla.

Amesisitiza kuwa, umuhimu wa mafunzo hayo hauishii tu kazini bali pia hata nyumbani wanapoishi watumishi hao.

Faida za mafunzo ya moto ni nyingi na muhimu kwani husaidia kuokoa maisha, Wafanyakazi wanapata uelewa jinsi ya kutoka nje kwa usalama na haraka, wanapata ujuzi wa kutumia vizima moto kabla moto haujasambaa na hivyo kupunguza hasara kwa kuepusha mali na vifaa vya ofisi kuungua.

Utoaji wa elimu na mafunzo ya kupambana na majanga ya moto mahali pa kazi ni takwa la kisheria linalowataka Waajiri kuhakikisha usalama na afya ya wafanyakazi wao. Nchini Tanzania, sheria kuu inayosimamia suala hili ni Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi Na. 5 ya 2003.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, wajibu wa Mwajiri ni kutoa elimu kwa kuwapa wafanyakazi mafunzo ya kuzuia na kupambana na moto, kuweka vifaa sahihi vya kuzimia moto mahali pa kazi, kuandaa njia za dharura na milango ya kutokea wakati wa hatari, na ukaguzi wa mara kwa mara kwa lengo la kuhakikisha mifumo ya tahadhali na kuzimia moto inafanya kazi vizuri.

Aidha, katika mafunzo hayo watumishi pia walijengewa uelewa juu ya Mpango Mkakati wa Mahakama ili kuwajengea uelewa wa kutosha watumishi na hivyo kuwawezesha kuwa na taarifa sahihi zinazowasaidia kufanya maamuzi sahihi kila inapohitajika.

Mahakama Kanda ya Arusha ilialika Kampuni ya TGN ya Arusha ambayo hujishughulisha na masuala ya kupambana na majanga ya moto na utoaji elimu juu ya namna bora ya kupambana na moto.

Wataalamu wa kampuni hiyo walitoa elimu ya nadharia na vitendo ambapo watumishi mbalimbali waliweza kuzima moto kwa vitendo huku wengine wakishuhudia namna uzimaji moto unavyofanyika.


Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Arusha wakifanya mafunzo ya kuzima moto kwa vitendo wakisimamiwa na Wataalamu kutoka Kampuni ya TGN inayojishughulisha na kupambana na majanga ya moto, mafunzo haya yaliyofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano Mahakama Kuu Arusha.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali akifungua Mafunzo ya namna ya kupambana na Majanga ya Moto mahali pa kazi yaliyofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Watumishi wa Mahakama  Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Arusha wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa mafunzo hayo.

Mtaalamu wa kupambana na majanga ya moto kutoka Kampuni ya TGN Arusha, Bw. Badru Juma akitoa elimu ya kuzima moto kwa watumishi wa Mahakama Arusha. Mafunzo hayo yalifanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano Mahakama Kuu Arusha.


Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Arusha wakifanya mafunzo ya kuzima moto kwa vitendo wakisimamiwa na Wataalamu kutoka Kampuni ya TGN inayojishughulisha na kupambana na majanga ya moto, mafunzo haya yaliyofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano Mahakama Kuu Arusha.


Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Arusha, Bi. Grace Kapama akitoa mada juu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa watumishi wa Mahakama Arusha. Mafunzo hayo yaliyofanyika hivi karibuni yalienda sambamba na ya namna ya kupambana na Majanga ya Moto mahali pa kazi yaliyofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



                            

 

                                                           

 


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni