Jumanne, 11 Agosti 2026

TMJA MBEYA WAHIMIZWA KUIMARISHA WELEDI, MAADILI NA MSHIKAMANO

Na MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya

Majaji na Mahakimu wa Mahakama ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Mbeya, wametakiwa kuendelea kudumisha weledi, maadili, mshikamano na mahusiano mema katika utendaji wa kazi, huku wakihimizwa kuongeza maarifa na kufanya tafiti za kitaalamu kwa ajili ya kuimarisha weledi katika utoaji haki.

Wito huo umetolewa katika kikao cha Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (TMJA) Masjala Ndogo ya Mbeya, kilichofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 7 hadi 9 Agosti 2026, katika fukwe za Ziwa Nyasa, Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya.

Akizungumza katika kikao hicho, Mlezi wa TMJA Masjala Ndogo ya Mbeya, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Fahamu Mtulya, amewakumbusha wanachama kuzingatia malengo ya chama hicho, hususan kudumisha hadhi na heshima baina ya Majaji na Mahakimu, pamoja na kuimarisha maarifa, uelewa na uwezo wao katika kufanya tafiti za kitaalamu.

“Miongoni mwa malengo ya TMJA Mbeya ni pamoja na kudumisha hadhi na heshima baina ya Majaji na Mahakimu na kuimarisha zaidi maarifa, uelewa na uwezo wetu katika kufanya tafiti za kitaaluma. Hivyo, tupo hapa ikiwa ni sehemu ya kutekeleza malengo hayo. Tuwe tayari kuzingatia na kujifunza ili tukitoka hapa tuwe Mahakimu wenye weledi zaidi,” alisema Mhe. Mtulya.

Mhe. Mtulya pia alisisitiza umuhimu wa kuthaminiana, kujaliana, kuheshimu viongozi, kuzingatia nidhamu na kuepuka ubaguzi, huku akiwataka wanachama kuendelea kushikamana kupitia vikundi vilivyoanzishwa kwa ajili ya kusaidiana wakati wa shida na raha.

Kwa upande wake, Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Benard Mpepo, alisisitiza umuhimu wa maadili, mawasiliano na mahusiano mazuri katika mazingira ya kazi.

“Ili uwe na utendaji kazi mzuri, ni lazima muwe na mahusiano na mawasiliano mazuri na viongozi wenu,” amesema Mhe. Mpepo, akiongeza kuwa ni muhimu kujenga mahusiano mazuri kati ya Majaji, Mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama ili kuboresha utendaji kazi.

Naye, Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Bw. Festo Chonya, amewataka watumishi kuepuka ubinafsi, kuzingatia taratibu na itifaki, pamoja na kujenga utamaduni wa upendo, kujali na kusaidiana, kadhalika amewataka watumishi kuendelea kumuunga mkono Jaji Mfawidhi katika utekelezaji wa majukumu yake ya kiuongozi.

Aidha, Mwenyekiti wa TMJA Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Asha Njovu, amewashukuru wanachama wanaotekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji, akiwahimiza kuendelea kudumisha viwango hivyo katika utumishi wao.

Kikao hicho pia kiliambatana na mafunzo kuhusu mbinu za kukabiliana na msongo wa mawazo pamoja na umuhimu wa malezi ya kitaaluma kwa Mahakimu (Mentorship Programme) yaliyolenga kuimarisha uwezo na ustawi wa kitaaluma wa washiriki.

Mbali na kikao na mafunzo hayo, wanachama walipata fursa ya kuburudika na kushiriki shughuli za utalii katika fukwe za Ziwa Nyasa, hatua iliyosaidia kuimarisha zaidi mahusiano na mshikamano miongoni mwa wanachama.

Kikao hicho ni sehemu ya jitihada za TMJA Masjala Ndogo ya Mbeya katika kuimarisha weledi, maadili, mshikamano na uwezo wa kitaaluma wa Majaji na Mahakimu, kwa lengo la kuendelea kuboresha utoaji wa haki na huduma kwa wananchi.

Mlezi wa TMJA Masjala Ndogo ya Mbeya, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (katikati) akiwa kwenye kwenye picha ya Pamoja na viongozi na wanachama wa TMJA Masjala Ndogo ya Mbeya wakati wa mafunzo na kikao hicho.

Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (TMJA) Masjala Ndogo ya Mbeya wakiwa kwenye kikao kilichoambatana na mafunzo ya Mentorship Programme


Sehemu Viongozi wa Mahakama walioshiriki katika Kikao hicho cha TMJA Masjala Ndogo ya Mbeya. 

Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (TMJA) Masjala Ndogo ya Mbeya wakiwa kwenye kikao kilichoambatana na mafunzo ya Mentorship Programme

Mlezi wa TMJA Masjala Ndogo ya Mbeya, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (wa pili kushoto) akiwa na viongozi wengine wa Mahakama  wakiwa kwenye picha ya pamoja na wanachama wapya wa TMJA Mbeya

Mlezi wa TMJA Masjala Ndogo ya Mbeya, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (wapili kushoto) akiwa na viongozi wengine wakikata keki kwa pamoja kuwakaribisha wanachama wapya wa TMJA Masjala hiyo.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Bw. Festo Chonya (aliyesimama) akizungumza katika kikao hicho (katikati) ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Benard Mpepo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Mbeya Mhe. Tedy Mlimba (aliyesimama) akizungumza katika kikao hicho, kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Kyela Mhe. Roster Mofuga na kushoto ni Naibu Msajili Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Zawadi Laizer.

Mwenyekiti wa TMJA Mbeya Mhe. Asha Njovu (aliyesimama wapili kushoto) akifungua kikao hicho, (wa kwanza kushoto) ni katibu wa TMJA Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Angela Byera na Mlezi wa TMJA Masjala Ndogo ya Mbeya, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (Katikati)

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha-Mahakama)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni