Jumatatu, 10 Agosti 2026

JAJI KIONGOZI ATEMBELEA NA KUFANYA UKAGUZI MAHAKAMA YA WILAYA CHAMWINO

Na ARAPHA RUSHEKE & JAMES BUSANYA - Mahakama

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, amefanya ziara katika Mahakama ya Wilaya Chamwino na kukagua miundombinu ya Mahakama hiyo, huku akitoa maelekezo mbalimbali yanayolenga kuimarisha utoaji wa huduma za haki kwa wananchi.

Ziara hiyo imefanyika leo tarehe 10 Agosti 2026 wakati alipotembelea Mahakama ya Wilaya Chamwino iliyoanza kutoa huduma rasmi kuanzia tarehe 24 Julai 2026, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Mahakama ya Tanzania za kusogeza huduma za haki karibu zaidi na wananchi. Kabla ya kuanzishwa kwa Mahakama hiyo, huduma za kimahakama kwa wananchi wa Wilaya ya Chamwino zilikuwa zikitolewa na Mahakama ya Wilaya Dodoma mjini.

Katika ziara hiyo, Mhe. Dkt. Siyani alikagua jengo na miundombinu ya Mahakama hiyo pamoja na kuzungumza na watumishi, ambapo alieleza kufurahishwa na jengo hilo na kuwapongeza waliokuwa wakisimamia ujenzi wake.

Nimefurahi leo tuna jengo zuri lenye viwango. Nawapongeza waliokuwa wanasimamia ujenzi huu. Tumesogeza huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Chamwino. Mahakama hii itawaletea nafuu, kuwaokolea muda na gharama,” alisema Jaji Kiongozi.

Alisema kuanzishwa kwa Mahakama hiyo ni hatua muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za haki karibu na maeneo yao, akiwataka viongozi wa Mahakama kuendelea kufikiria namna ya kusogeza huduma kwa wananchi bila kuathiriwa na mipaka ya kijiografia.

Jaji Kiongozi aliutaka Uongozi wa Mahakama ya Wilaya Chamwino kushirikiana na viongozi wa Kata katika maeneo yanayohudumiwa na Mahakama hiyo, ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa kuhusu huduma zinazotolewa na Mahakama, ikiwemo kupitia njia za mtandao nakufanya vipindi kwa njia ya Radio.

Aidha, alisisitiza matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za Mahakama, akieleza kuwa teknolojia inaweza kusaidia kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi na kupunguza utegemezi wa matumizi ya makaratasi.

Katika kusisitiza matumizi ya TEHAMA, Mhe. Dkt. Siyani aliagiza timu ya wataalum kuhakikisha huduma za mtandao ziunganishwe haraka katika Mahakama hiyo ili ziweze kusadifu ubora wa jengo na huduma za kimahakama kwa wananchi, akieleza kuwa uwepo wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ni fursa inayopaswa kutumika kikamilifu katika kuboresha huduma za Mahakama.

Alibainisha pia kuwa, ushahidi unaweza kutolewa katika Mahakama kwa njia ya Mahakama Mtandao, pale ambapo utaratibu huo unaruhusiwa kisheria, hatua ambayo inaweza kusaidia kurahisisha mwenendo wa mashauri na kupunguza usumbufu kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, Jaji Kiongozi alisisitiza umuhimu wa Mahakama kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wananchi wanaofika kupata huduma, akionya watumishi dhidi ya kuweka vikwazo visivyo vya lazima, hivyo mwananchi anapofika mahakamani anapaswa kuhudumiwa kwa wakati.

Mhe. Dkt. Siyani pia alitoa maelekezo kuhusu utunzaji wa vielelezo na kuvirejesha kwa wahusika mara baada ya mashauri kukamilika mahakamani, akitaka kuwepo kwa utaratibu maalum wa kuhakikisha vielelezo hivyo vinatunzwa kwa usalama na kwamba wenye mali wanarejeshewa kwa kufuata sheria na taratibu zinazokubalika.

Akizungumzia utunzaji wa mazingira, Jaji Kiongozi alisisitiza kuwa, majengo ya Mahakama yanapaswa kwenda sambamba na mazingira safi na yanayovutia, akiwataka watumishi kupanda miti na maua pamoja na kuhakikisha uchafu unaondolewa katika maeneo ya Mahakama.

Tusikubali jengo letu na miundombinu yetu ichakae kwa wepesi. Watumishi tushirikiane kulitunza jengo letu na kulifanyia usafi. Mazingira yetu ya ndani na nje ya Mahakama yawe vizuri,” alisema Dkt Siyani.

Aliagiza uongozi wa Mahakama ya Wilaya Chamwino kusimamia utekelezaji wa mpango wa utunzaji mazingira na upandaji miti katika maeneo ya Mahakama, akieleza kuwa taasisi jirani zinapaswa kuvutiwa na mazingira bora yatakayowekwa na Mahakama hiyo.

Katika kuimarisha utendaji kazi, Jaji Kiongozi aliwataka watumishi wa Mahakama ya Wilaya Chamwino kuwa na utamaduni wa kujifunza, kukumbushana na kufundishana, akisema kuwa mafanikio yanahitaji watumishi wenye utayari wa kujifunza mambo mapya kila wakati.

Kama mnataka mafanikio muwe na utaratibu wa kukumbushana kwa kufundishana. Watu bora ni wale wanaojifunza. Msibweteke na mnachokijua, vipo vingine hamvijui. Mnaweza kufundishana wenyewe mambo mengi na muhimu,” alisema Jaji Kiongozi

Akihitimisha ziara hiyo, Mhe. Dkt. Siyani aliwataka watumishi kujitathmini mara kwa mara kuhusu namna wanavyowahudumia wananchi na kuhakikisha kila anayefika mahakamani anapata huduma kwa heshima, weledi, uadilifu na kwa wakati.

Mahakama ya Wilaya Chamwino inahudumia wananchi wapatao 486,176, Wilaya hiyo inayoundwa na tarafa tano (5), Kata 36, Vijiji 107 na Vitongoji 814. Kuanzishwa kwa Mahakama hiyo ni hatua muhimu katika kusogeza huduma za haki karibu zaidi na wananchi, kuwaokoa muda na gharama, pamoja na kuimarisha imani ya wananchi katika mfumo wa utoaji haki nchini.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (aliyeketi kiti cha mbele), akipokea taarifa fupi ya Mahakama ya Wilaya ya Chamwino Kutoka kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma Mhe. Joachim Tiganga (wa pili kulia) wakati wa ziara ya kutembelea Mahakama ya Wilaya Chamwino na kukagua miundombinu ya Mahakama hiyo leo tarehe 10 Agosti, 2026.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (kulia) akitete jambo na Waendesha Mashitaka wa Serikali wakati alipotembelea Ofisi hiyo ya wadau wanaotoa huduma mahakamani hapo.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (kushoto), akikagua sehemu ya miundombinu jengo la Mahakama ya wilaya Chamwino huku akiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma Mhe. Joachim Tiganga (kulia aliyenyoosha mkono) wakati wa ziara ya kutembelea Mahakama ya Wilaya Chamwino na kukagua miundombinu ya Mahakama hiyo.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (kushoto) akizungumza na kupata maelekezo kutoka kwa mtumishi wa mahakama hiyo kwenye dirisha la Mapokezi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akiwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Chamwino wakikagua sehemu ya miundombinu ya jengo la Mahakama ya wilaya Chamwino huku akiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma Mhe. Joachim Tiganga. 
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma Mhe. Joachim Tiganga (aliyenyoosha mkono) akimuonesha eneo la vielelezo Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akiwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama wakati wa ziara hiyo.
Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dodoma Bw. Bedson Mariba (wa kwanza kushoto) akimuonesha Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani eneo la mipaka ya Mahakama ya Wilaya Chamwino wakati alipokuwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama wakati wa ziara hiyo.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (aliyenyoosha mkono) akitoa maelekezo kwa Viongozi wa Mahakama juu ya utunzaji wa mazingira ya Mahakama ya Wilaya Chamwino.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (katikati), akisisitiza jambo wakati alipokuwa akiongea na watumishi na viongozi wa Mahakama (hawapo pichani) wakati wa ziara ya kutembelea Mahakama ya Wilaya Chamwino na kukagua miundombinu ya Mahakama hiyo. Wengine ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma Mhe. Joachim Tiganga (wa kwanza kushoto) na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Kiaki Nkya wa kwanza kulia.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Chamwino mara baada ya ziara ya ukaguzi wa jengo hilo.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania alioambatana nao katika  ziara ya ukaguzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya Chamwino.

Muonekano wa jengo la Mahakama ya Wilaya Chamwino.

Muonekano wa jengo la Mahakama ya Wilaya Chamwino.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)

(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)



 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni