Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba
Rwizile amewasisitiza watumishi wa Mahakama hiyo juu ya umuhimu wa kuzingatia
maadili ya kazi zao na kuepuka vitendo vyote vya rushwa vinavyoweza kuharibu
sifa ya Mhimili wa Mahakama na kukosesha haki kwa wananchi wanaowafuata huduma.
Mhe.
Rwizile aliyasema hayo tarehe 07 Agosti, 2026 kwenye ukumbi wa
mikutano wa Mahakama Kuu Kigoma alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja
yaliyolenga kuwajengea uelewa watumishi wa Mahakama hiyo kuhusu elimu ya kuzuia
na kupambana na rushwa mahali pa kazi sambamba na kuimarisha misingi ya
uadilifu, uwazi, na uwajibikaji katika utoaji wa haki kwa wananchi.
"Rushwa
ni adui wa haki; watumishi wa Mahakama tunapaswa kuwa mstari wa mbele katika
kulinda na kusimamia maadili ya utumishi wa umma ili wananchi waendelee kuamini
mfumo wetu wa utoaji haki usioacha shaka ili haki hiyo ipatikane mapema
ipasavyo," alisisitiza Jaji Mfawidhi huyo.
Aidha,
Mhe. Jaji Rwizile aliwasisitiza zaidi watumishi hao kuwa uadilifu ni nguzo kuu
katika kusimamia sheria na kwamba Mahakama inapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika
jamii.
Mada
kuu za mafunzo hayo ziliwasilishwa na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kigoma, Bi. Asha Kwaliko.
Katika
uwasilishaji wake, Bi. Kwaliko aliwafahamisha watumishi hao kuhusu aina
mbalimbali za rushwa, madhara yake kisheria na kijamii, pamoja na mbinu za
kujikinga na vishawishi kazini.
Bi.
Kwaliko alieleza kwa kina wajibu wa kila mtumishi katika kutoa taarifa za
vitendo vya rushwa na kueleza sheria mbalimbali zinazowalinda watoa taarifa
(whistleblowers).
Aidha,
aliwakumbusha watumishi hao kuwa TAKUKURU itaendelea kushirikiana kwa karibu na
Mahakama Kuu Kigoma katika kutoa elimu endelevu na kuchukua hatua kali dhidi ya
yoyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Kwa
upande wake Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kigoma, Bw. John Mgallah, alisema
kuwa, rushwa inaweza kutafsiriwa kama kitu chochote cha thamani kinachotolewa
au kupokelewa na mtu yeyote kinyume na sheria ili kupata huduma au kutoa huduma
na vilevile rushwa ni utumiaji mbaya wa madaraka ili kujinufaisha au
kumnufaisha mtu mwingine kwa kupindisha sheria, kanuni au taratibu za nchi.
Naye
Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka
aliwashukuru Viongozi hao wa TAKUKURU na kusema kuwa Mafunzo waliyotoa yataleta tija kubwa katika
kuongeza ufanisi wa kazi kwa watumishi, kupunguza mianya ya rushwa na
kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama katika Mkoa huo.
Hata
hivyo, Bw. Kasuka alibainisha kuwa mafunzo hayo yalifanyika katika Mahakama za Wilaya
sita ambazo ni Kibondo, Uvinza, Buhigwe, Kakonko, Kasulu na Kigoma pamoja na
Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma pamoja na watumishi wa Mahakama za Mwanzo na
kadhalika.
Sehemu ya watumishi wa Mahakama Kigoma wakifuatilia kwa makini mada iliyokuwa ikiendelea kutolewa hivi karibuni na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kigoma, Bi. Asha Kwaliko (aliyesimama) wakati wa Mafunzo kuhusu madhara ya Rushwa kwa Watumishi wa Mahakama yaliyofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile akitoa neno kwa msisitizo alipokuwa akifungua Mafunzo kuhusu madhara ya Rushwa kwa Watumishi wa Mahakama yaliyofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kigoma, Bi. Asha Kwaliko akifafanua jambo kwa msisitizo wakati wa Mafunzo kuhusu madhara ya Rushwa kwa Watumishi wa Mahakama yaliyofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma.
Mtendaji wa Mahakama Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka akitoa neno la shukrani kwa viongozi wa TAKUKURU Mkoa wa Kigoma kwa kukubali kutoa mafunzo kwa watumishi wa Mahakama juu ya athari za rushwa mahali pa-kazi.
Naibu Mkuu wa TAKUKURU (M) Kigoma, Bw. John Mgalla (aliyesimama) akiwasilisha mada ya maadili na wajibu wa watumishi wa Mahakama katika mapambano dhidi ya rushwa.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Kigoma na Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji wa Mahakama Masjala Ndogo ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka (wa pili kulia), Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kigoma, Bi. Asha Kwaliko (wa pili kushoto), Naibu Mkuu wa TAKUKURU (M) Kigoma, Bw. John Isaac Mgallaha (wa kwanza kushoto), Hakimu Mkazi wa Wilaya Kigoma, Mhe. Anna Kahungu na waliosimama nyuma ni sehemu ya watumishi wa Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kigoma na Mahakama zake za Mwanzo.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni