Na ARAPHA RUSHEKE – Mahakama, Dodoma
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Doodoma, Mhe. Joachim Tiganga, hivi karibuni aliwaongoza watumishi kufanya ziara ya mafunzo katika
Hifadhi ya Ngorongoro.
Lengo
la ziara hiyo lilikuwa kujifunza kuhusu uhifadhi wa mazingira na wanyamapori,
historia, utamaduni pamoja na vivutio mbalimbali vya utalii vinavyopatikana
katika eneo hilo.
Ziara
hiyo ilijumuisha pia Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Suleimani Hassan, Naibu Wasajili na Watumishi wa Mahakama
kutoka Mkoa wa Dodoma na Wilaya zake za
Kongwa, Chamwino, Mpwapwa, Chemba na Kondoa.
Wakiwa
kwenye ziara hiyo, watumishi hao walipatiwa elimu kuhusu historia ya Hifadhi ya
Ngorongoro, wanyamapori wanaopatikana katika eneo hilo, shughuli za uhifadhi
pamoja na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika kulinda mazingira na
wanyamapori.
Elimu
hiyo imewasaidia watumishi kupata uelewa mpana kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa
mazingira na wanyamapori, pamoja na nafasi ya Hifadhi ya Ngorongoro katika
kulinda urithi wa Taifa na kukuza utalii nchini.
Watumishi
hao walitembelea eneo lenye mchanga
unaohama, ambapo walipata maelezo kutoka kwa Bw. Ndengere Ngisaruni kuhusu hali hiyo ya kipekee ya kimaumbile
ambayo imekuwa miongoni mwa vivutio vinavyowavutia watalii kutoka sehemu
mbalimbali duniani.
Aidha,
watumishi hao walitembelea Olduvai
Gorge, eneo maarufu kwa historia ya mwanadamu wa kale, ambapo walipata
fursa ya kujifunza kuhusu ugunduzi wa mabaki ya viumbe wa kale na historia ya
mwanadamu.
Katika
eneo hilo, watumishi walielezwa pia kuhusu historia ya Faru Fausta, aliyefariki akiwa na takribani miaka 57, pamoja na
taarifa mbalimbali zinazohusiana na historia ya wanyamapori na urithi wa eneo
hilo.
Ziara
hiyo pia iliwapa watumishi hao fursa ya kutembelea Boma la Kimasai, ambapo walijifunza kuhusu maisha, mila, desturi
na utamaduni wa jamii ya kimasai, pamoja na namna utamaduni huo unavyohifadhiwa
na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Akitoa
shukrani kwa niaba ya watumishi hao, Mhe.
Tiganga aliushukuru uongozi wa Hifadhi ya Ngorongoro kwa mapokezi
mazuri, ushirikiano na elimu waliyopewa wakati wa ziara hiyo.
Mhe.
Tiganga alisema ziara hiyo imekuwa fursa muhimu kwa watumishi kujifunza mambo
mapya nje ya mazingira yao ya kawaida ya kazi, huku ikiwapa nafasi ya kujenga
mshikamano, kubadilishana uzoefu na kuongeza uelewa kuhusu historia, mazingira
na utamaduni wa Tanzania.
Kwa
ujumla, ziara hiyo imekuwa sehemu ya kujenga maarifa na mshikamano miongoni mwa
watumishi wa Mahakama, sambamba na kuwapa fursa ya kutambua kwa undani zaidi
utajiri wa historia, mazingira, wanyamapori na tamaduni zinazopatikana nchini.
Ziara hiyo imehitimisha kwa mafanikio, ikiwaacha watumishi hao na maarifa mapya kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira, wanyamapori, historia na utamaduni wa Tanzania kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Bdogo Dodoma, Mhe.
Joachim Tiganga, akiwa katika picha ya pamoja na watumishi baadaya ya kuwasili
katika Hifadhi ya Ngorongoro.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe.
Joachim Tiganga, akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Hifadhi
ya Ngorongoro.
Sehemu ya watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma
wakiwa katika picha ya pamoja.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe.
Joachim Tiganga, akifafanua kitu mara baada ya kuwasili katika Hifadhi ya
Ngorongoro.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe.
Joachim Tiganga, akifafanua kitu mara baada ya kufika katika mabaki na masalia
ya vitu vya kale.
Watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma wakipatiwa
elimu wakati walipofika katika Hifadhi ya Ngorongoro.
Sehemu ya watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma
wakiendelea na utalii katika Hifadhi ya Ngorongoro.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe.
Joachim Tiganga, akiwa na watumishi wakiangalia mabaki ya Faru Fausta aliishi
miaka 57.
Watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wakiwa katika picha ya pamoja katika sehemu ya mchanga unaohama uliopo Hifadhi ya Ngorongoro.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni