Jumanne, 11 Agosti 2026

WATUMISHI IJC DODOMA WAVUTIWA NA UZURI WA ZIWA MANYARA

Na ARAPHA RUSHEKE – Mahakama, Dodoma

Watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma (IJC), tarehe 9 Agosti, 2026 walitembelea Hifadhi ya Taifa ya Lake Manyara kwa lengo la kujifunza, kujenga uelewa kuhusu uhifadhi wa mazingira na kutambua fursa mbalimbali za utalii zinazopatikana nchini Tanzania.

Ziara hiyo iliongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga. Wakiwa kwenye ziara hiyo, watumishi hao walipata fursa ya kujifunza kwa vitendo kuhusu historia, mazingira, wanyamapori pamoja na shughuli mbalimbali za utalii zinazopatikana katika hifadhi hiyo.

Akitoa elimu kwa watumishi hao, Afisa Utalii, Afande Clara Temu, alisema Hifadhi ya Taifa ya Lake Manyara ina ukubwa wa takribani kilomita za mraba 648.7, ambapo kilomita za mraba 386 ni eneo kavu huku sehemu nyingine ikiwa ni eneo la Ziwa.

Temu amesema hifadhi hiyo ina vivutio mbalimbali vinavyowavutia watalii kutoka ndani na nje ya Tanzania, ikiwemo Simba wanaopanda miti, chemchem za maji ya moto, Ziwa Manyara pamoja na utalii wa ndege, ambapo hifadhi hiyo ina zaidi ya aina 400 za ndege.

Ameongeza kuwa Ziwa Manyara pia ni muhimu kwa uhifadhi wa ndege wa majini na ni makazi ya wanyama mbalimbali wakiwemo viboko.

Katika ziara hiyo, watumishi hao walipata fursa ya kutembelea Tree Canopy Walkway, kivutio kinachowawezesha watalii kutembea juu ya njia zilizojengwa katikati ya miti na kupata mwonekano wa kipekee wa mazingira ya hifadhi.

Akitoa maelezo kuhusu kivutio hicho, Muongoza Watalii Regina Dunduli alisema Tree Canopy Walkway ilijengwa mwaka 2016 na kuanza kutumika mwaka 2017, ikiwa na madaraja tisa (9) pamoja na majukwaa 10.

Bi. Dunduli alisema kuwa njia hiyo imejengwa katikati ya miti ikiwemo miti ya mahogany na inawapa watalii fursa ya kuona kwa karibu aina mbalimbali za ndege, wanyama na mimea.

Alieleza kuwa watu wasiozidi wanne wanaruhusiwa kutumia sehemu hiyo kwa wakati mmoja, huku watalii wakitakiwa kuzingatia maelekezo ya waongoza watalii na taratibu za usalama.

Kwa mujibu wa Bi. Dunduli, shughuli hiyo huchukua kati ya dakika 45 hadi saa moja, huku watalii wakitakiwa kuwa watulivu na kuzungumza kwa sauti ya chini ili kutowasumbua wanyama.

Watumishi hao pia walielezwa kuwa Hifadhi ya Taifa ya Lake Manyara inatoa fursa za shughuli mbalimbali za utalii, zikiwemo walking safari, kuangalia machweo ya jua (sunset viewing), kupiga makasia, utalii wa ndege pamoja na utalii wa usiku.

Aidha, watalii wanaweza kufanya matembezi marefu kwa miguu yanayoweza kuchukua kati ya saa moja hadi saa nne, kulingana na aina ya shughuli wanayochagua. Kwa watalii wenye mahitaji maalum ya usafiri, pia kuna uwezekano wa kutumia helikopta kutembelea maeneo mbalimbali ya hifadhi.

Ziara hiyo imewapa watumishi hao fursa ya kujifunza kwa vitendo umuhimu wa utalii wa ndani, uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za asili, huku ikiwahamasisha kutambua na kuthamini utajiri wa vivutio vilivyopo nchini.

Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha watumishi kujifunza nje ya mazingira ya kazi, kujenga uelewa mpana na kuendelea kuutangaza utalii wa ndani kwa kutembelea na kufahamu vivutio mbalimbali vinavyopatikana nchini.

Afisa utalii wa Lake Manyara, Afande Crala Temu akitoa elimu ya hifadhi kwa watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo  Dodoma baada ya kuwasili katika hifadhi hiyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga (wa kwanza kushoto) akiwa na Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe Suleiman Hassan mara baada ya kuwasili katika Hifadhi ya Lake Manyara.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe Joachim Tiganga, (wa tatu kutoka kulia)akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi waliotoka Mahakama pamoja na Hifadhi ya Lake Manyara, wa nne kutoka kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe Suleiman Hassan, anayefuatia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe Upendo Ngitiri, akifuatiwa ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe. Zabibu Mpangule, wa kwanza kulia ni Kaimu Mtendaji wa Mahakama Dodooma, Bw. Stanslaus Makendi na wa pili kulia Afisa Utalii wa Hifadhi ya Lake Manyara, Afande Crala Temu.

Watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuwasili katika hifadhi hiyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga, akifurahia jambo mara ya kutembelea katika daraja hilo.

Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Suleimani Hassan akitembea katika daraja pamoja na watumishi wengine.

Watumishi wa Mahakama Kuu Dodoma wakifurahia jambo.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe Upendo Ngitiri, akifurahia jambo wakati akimaliza kutembea katika daraja hilo.

Afisa Utalii, Afande Crala Temu (aliyepo katikati) akitoa shukran kwa Jaji wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Suleimani Hassan (wa kwanza kulia )baada ya kukabidhiwa zawadi kutoka kwa watumishi hao.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni