Na EVA LESHANGE & AMIRI BAKARI, Mahakama- Singida
Watumishi
wanaofanya majukumu ya ziada Mkoani Singida wamepatiwa mafunzo yaliyosheheni mada mbalimbali kwa
ajili ya kuwajengea uwezo ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi.
Watumishi
hao 14 wanaonufanika na mafunzo hayo ni Wasaidizi wa Ofisi na Walinzi kutoka
Wilaya ya Singida, Manyoni na Iramba ambao mbali na kufanya majukumu ya Kada walizoajiriwa
nazo ambazo ni ulinzi na Usaidizi wa Ofisi lakini wamekuwa wakifanya kazi za
usaidizi wa kumbukumbu na kuingia Mahakamani.
Akifungua
mafunzo hayo tarehe 21 Agosti, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Singida,
Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Singida, Mhe. Evodia
Kyaruzi aliwapongeza watumishi hao kwa kuwa tayari kufanya majukumu hayo katika
kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi.
“Watumishi
wenzangu kipekee kabisa niwashukuru kwa utayari mliouonesha na kuwa wabunifu
kuhakikisha shughuli za kila siku za Mahakama hazikwami, hivyo basi kwa umuhimu
tumeona kuandaa mafunzo haya ya kuwajengea uwezo ili kuhakikisha mnatoa huduma
bora zaidi kwa wateja na kuhakikisha tunafikia malengo ya taasisi,” alisema
Mhe. Kyaruzi.
Aidha,
Naibu Msajili huyo aliwasisitiza washiriki kuwa huru wakati wa kuchangia mada na
kubainisha maeneo ambayo yanahitaji kuboreshwa kwani Menejimenti inaamini baada
ya mafunzo hayo kutakuwa na mabadiliko makubwa katika utendaji kazi.
Mada
zilizotolewa ni pamoja na Majukumu ya kila siku katika Masjala za Mahakama za
Mwanzo, Masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na matumizi
sahihi ya Mashine za kufanyia (POS) na Masuala ya uhasibu hususani kwenye
kuandaa taarifa za maduhuli na ujazwaji wa vitabu.
Watoaji
wa mada hizo walikuwa ni Bw. Paul Ndonde, Msaidizi wa Kumbukumbu, Bi. Elizabeth
Bwaila, Ofisa Hesabu Msaidizi na Bi.Valentina Nkullanga, Ofisa TEHAMA.
Nao
washiriki wa mafunzo hayo walishukuru kwa fursa hiyo adhimu ya kupewa nafasi ya
kuhuduria mafunzo hayo kwani wamepata uelewa wa mambo mengi na kuhaidi kuacha
kufanya kazi kwa mazoea na kuendelea kufanya
kazi kwa uadilifu na weledi.
Msaidizi wa Kumbukumbu Mahakama ya Mwanzo Utemini, Bw. Paul Ndonde akielekeza jambo kwa watumishi waliohudhuria mafunzo hayo (hawapo katika picha).
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni