Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Dar es Salaam
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi amewataka Wadau wa Mahakama na watumishi wa Mahakama kuendelea kufanya mazoezi, kushiriki michezo na kuendelea kuhamasishana katika kulinda afya.
Mhe. Maghimbi aliyasema hayo tarehe 22 Agosti 2026 katika Viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua Bonanza la Michezo lililoandaliwa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na Mahakama Kuu Divisheni za Biashara, Kazi, Ardhi, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Kituo cha Usuluhishi.
Bonanza hilo limehusisha Kanda nzima ya Dar es Salaam yaani Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani likiongozwa na Kaulimbiu isemayo ‘Afya bora kwa watumishi ni chachu ya Uwajibikaji.’
Akizungumza wakati akitoa hotuba ya ufunguzi wa Bonanza hilo, Jaji Maghimbi alisema angependa bonanza hilo lisibaki kuwa tukio la siku moja tu bali anatamani kuona utamaduni wa michezo na mazoezi ukiendelea.
“Ningependa bonanza hili lisibaki kuwa tukio la siku moja, ningependa kuona utamaduni wa michezo na mazoezi ukiendelezwa katika vituo vyetu mbalimbali vya kazi nchini. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kutenga muda kwa ajili ya afya yake. Mahakama inahitaji watumishi wenye afya njema, ari na nguvu za utekelezaji wajibu wao kwa wananchi,” alisema Mhe. Maghimbi.
Akizungumzia Kaulimbiu ya mwaka huu ya Bonanza Mhe. Maghimbi amesema kaulimbiu hiyo ni muhimu kwa sababu inawakumbusha kuwa, mafanikio ya Taasisi yoyote hayawezi kupatikana bila kujali afya na ustawi wa watumishi wake kwa maana mtumishi ndiye anayebeba majukumu ya Taasisi. Hivyo, wanapowekeza kwenye afya za watumishi wanawekeza katika tija, ufanisi na mafanikio ya taasisi.
Aliongeza kuwa, watumishi wenye afya bora wana uwezo wa kufanya kazi kwa umakini, ari na ufanisi, pia wanaweza kukabiliana na changamoto za kazi, kushirikiana vizuri na kutekeleza majukumu yao kwa wakati.
“Afya isipotiliwa maanani inaweza kuathiri mahudhurio kazini, uzalishaji, ubora wa huduma na hatimaye utendaji wa taasisi kwa ujumla,” alisema Jaji Mfawidhi huyo huku akiwasisitiza watumishi wote walichukulie suala la afya kama sehemu ya chachu ya uwajibikaji wao wa kila siku.
Jaji Maghimbi alisema, Bonanza limewapa fursa ya kufanya mazoezi, lakini pia limewakumbusha umuhimu wa kuwa na utamaduni wa michezo na mazoezi katika Maisha yao ya kila siku, michezo husaidia kuimarisha mwili kupunguza msongo wa mawazo na kujenga afya ya akili. Vilevile hujenga nidhamu, uvumilivu, ushirikiano na uwezo wa kufanya kazi kama timu moja. Amesema hizo ni tunu zinazohitajika kwa kiwango kikubwa katika maeneo yao ya kazi.
Vilevile, Mhe Maghimbi aliwasihi watumishi wasiishie kushiriki michezo wakati wa bonanza hilo pekee bali wajenge utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara na kuzingatia mtindo bora wa maisha kama kuzingatia ulaji bora wa chakula na kupima afya kila mara.
Aliongeza kwamba, Bonanza ni darasa la umoja na ushirikiano na kusisitiza kuwa bonanza hilo si mashindano ya michezo pekee bali ni jukwaa muhimu la kujenga umoja na kuimarisha mahusino kati ya Taasisi na Taasisi kuleta picha nzuri ya umuhimu wa kufanya kazi kwa kushirikiana, bila kuathiri mipaka yao ya utendaji kazi.
Kuhusu uwajibikaji na utumishi wa umma, Jaji Maghimbi alisema inahusisha moja kwa moja suala la uwajibikaji na kwamba uwajibikaji unahitaji mtumishi mwenye afya ya mwili na akili.
Mhe. Maghimbi alitoa ujumbe kwa washiriki wa bonanza kuwa, siku hiyo imekuwa muhimu kwakuwa imewakutanisha pamoja kama ndugu, wameshiriki mazoezi kwa wiki nzima na siku hiyo wamekutana pamoja kama familia katika kilele cha siku ya bonanza kubwa.
Aliwasihi kushiriki michezo kwakuwa inaleta furaha, nidhamu na kuheshimiana huku akisema kuwa, “tushindane kwa nguvu zote lakini tushindane kwa kuzingatia kanuni na moyo wa kiungwana.”
Alihitimisha kwa kuwatakia watumishi/washiriki bonanza jema kwa kusema, “mshindi wa kweli wa bonanza hilo ni yule atakayemaliza siku akiwa na afya bora, furaha mpya na rafiki mpya kutoka taasisi nyingine.”
Akitoa neno la utangulizi katika bonanza hilo, Jaji wa Mahakama Kuu ambaye pia ni mwenyekiti wa michezo wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam, Mhe. Arnold Kirekiano alisema kufanyika kwa bonanza hilo ni matokeo ya bonanza la tarehe 04 Oktoba, 2025 ambapo Jaji Mfawidhi aliagiza Kamati ya Bonanza hilo iandae bonanza lingine na mpaka sasa kamati imefanikiwa kuandaa bonanza hilo.
Katika bonanza hilo ilifanyika michezo mbalimbali kama Kukimbia na Yai, Mbio
za Mita 100, Kukimbia na Gunia, Kuvuta Kamba, Rede, ‘Pool Table’, Kukuna Nazi, Kuendesha
Baiskeli kwa Mwendo wa Polepole, Mashindano ya Kula, Kujaza Maji kwenye Chupa
kwa Kutumia Sponji, Kuweka Mrija kwenye Chupa kwa Kutumia sehemu ya Pua, mpira
wa pete, Mpira wa Kikapu, Mpira wa Miguu, Kucheza Bao, Kucheza Drafti, Kucheza Karata,
Kukimbiza Kuku, Kucheza kwenye viti ‘Chair Dance na ‘Golf’.
Washindi katika bonanza hilo wamepatiwa zawadi mbalimbali ikiwemo, vikombe, medali, kuku na pesa taslimu.
Bonanza hilo lilianza kwa mazoezi ya viungo na kupambwa na burudani mbalimbali za muziki (live band) na muziki wa asili.
Wadau wengine walioshiriki katika Bonanza hilo walitoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA), Taasisi ya Kuzui ana Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), PSSF, NSSF, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Jeshi la Polisi, Magereza, Ofisi ya Uhamiaji, Chama cha Madalali na Wasambaza Nyaraka Tanzania, Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya, Benki ya NMB.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Michezo wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam Mhe. Arnold Kirekiano akitoa neno la utangulizi na kumkaribisha Jaji Mfawidhi ili kufungua tamasha hilo.
Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Dkt. Cleoface Morris akisalimia na Timu ya Mpira wa Miguu ya Mahakama.
Washiriki wa shindano la kukuna nazi kwa wanaume na wanawake wakiendelea na shindano hilo.
Timu ya Kamba Wanaume na Wanawake Mahakama wakitekeleza jukumu la
kuvutana na kuibuka kidedea.
Mashindano ya kukimbia na gunia yakiendelea...
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro akifanya mazoezi ya viungo wakati wa Bonanza hilo lililofanyika tarehe 22 Agosti, 2026 katika Viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)










Hakuna maoni:
Chapisha Maoni