Jumapili, 23 Agosti 2026

MAOFISA MAGEREZA MKOA WA NJOMBE WAPATIWA MAFUNZO YA MFUMO WA e-CMS

  •  Wafundishwa jinsi ya kupakua Nakala za Hukumu....
  • Wasisitizwa juu ya matumizi ya TEHAMA
Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe

Maofisa Magereza Mkoa wa Njombe wamepatiwa Mafunzo ya Mfumo wa Ki-elektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) yaliyolenga kuwaelekeza juu ya upakuaji wa nakala za hukumu na mienendo ya mashauri mahakamani.

Mafunzo hayo yaliyofanyika tarehe 19 Agosti, 2026 katika Gereza la Wilaya Njombe pamoja na Gereza la Wilaya Ludewa yalifunguliwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano ambapo washiriki walihudhuria mafunzo hayo kupitia Mkutano Mtandao (Video Conference) na tarehe 20 Agosti, 2026 mafunzo hayo yaliendelea kwa Maofisa wa Gereza la Wilaya Makete katika kumbi za Mahakama ya Wilaya Makete.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Luambano alisisitiza juu ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa ajili ya kusaidia upatikanaji wa nakala za hukumu kwa haraka na kwa unafuu kupitia Mfumo wa e-CMS ili kuepuka malalamiko yasiyo ya lazima kutoka kwa Mahabusu au Wafungwa.

“Kupakua hukumu na mienendo ya mashauri kunasaidia kuepusha muda na malalamiko yasiyo ya lazima juu ya upatikanaji wa nakala za hukumu kwa kuwa nakala za hukumu zinapatikana kupitia kwenye akaunti zenu za Magereza baada ya shauri kuwa limeshafanyiwa uamuzi,’’ alisema Naibu Msajili huyo.

Aliongeza kuwa, mfumo huo unaosimamia Mashauri Mahakamani    unalenga kuimarisha utoaji haki mapema ipasavyo na kwamba kupitia mfumo huo  kwa upande wa Mahakama Kuu Njombe kwa sasa  haitumii karatasi kupata nakala za hukumu bali zinapatikana kupitia kwenye mfumo.

Vilevile, Mhe. Luambano alibainisha kwa, mafunzo hayo yametokana na ziara ya Kamati ya Kusukuma Mashauri ya Jinai katika Gereza la Butimba jijini Mwanza ambapo baada ya kuwasilisha taarifa ya ziara hiyo kwa Jaji Kiongozi, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani alitoa maelekezo kwa Naibu Wasajili pamoja na Maofisa TEHAMA kwa kila Mahakama Kuu kutoa mafunzo kwa Maofisa Magereza juu ya kupakua  nakala za hukumu na mienendo kwenye Mfumo wa Kielektroniki wa Mahakama wa Usimamizi wa Mashauri (JoT e-CMS).

Mafunzo hayo yalihudhuriwa na Maofisa Magereza ya Njombe, Ludewa na Makete mkoani Njombe.


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano akisisitiza jambo kwa Maofisa Magereza wa Gereza la Wilaya ya Makete wakati wa Mafunzo ya Mfumo wa Ki-elektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) yaliyolenga kuwaelekeza juu ya upakuaji wa nakala za hukumu na mienendo ya mashauri mahakamani yaliyofanyika hivi karibuni.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano akizungumza jambo na Maofisa Magereza (hawapo katika picha) wakati wa mafunzo hayo.

Maofisa kutoka Gereza la Wilaya ya Makete. Kutoka kushoto ni SGT. Noah Mtofole, anayefuata ni SGT. Harid Katundu 
na kulia ni WRD. Jonathan Masele wakimsikiliza kwa umakini Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano.

 SGT.Ezekia Kalenga (aliyesimama) akijifunza kwa vitendo wakati wa mafunzo hayo. Walioketi kushoto ni WDR’S. Jamila Maulid anayefata ni SGT. Frank Nkosi wakielekezwa na Ofisa TEHAMA (hayupo katika picha).

Mafunzo kwa vitendo yakiendelea..






 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni