Jumatatu, 7 Septemba 2026

BALOZI MDOGO WA BURUNDI MKOANI KIGOMA AFANYA ZIARA MAHAKAMA KUU KIGOMA

Na AIDAN ROBERT,Mahakama-Kigoma.

Balozi mdogo wa Jamhuri ya Burundi nchini Tanzania anayehudumia Mkoa wa Kigoma, Bw. Kekenwa Jeremia, hivi karibuni alifanya ziara Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Kigoma na kufanya mazungumzo na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Augustine Rwizile.

Lengo kuu la ziara hiyo ya Kiofisi iliyofanyika tarehe 04 Septemba, 2026 lilikuwa ni kujitambulisha upya na kutoa taarifa rasmi kwa Jaji Mfawidhi kuwa ameongezewa muda wa kuhudumu katika nafasi yake ya ubalozi mdogo nchini Tanzania. Hatua hiyo, inatajwa kuwa chachu kubwa ya ushirikiano wa karibu katika kutoa huduma za haki kwa raia wa Burundi.

Aidha, Balozi huyo alitumia fursa hiyo kufikisha salamu maalum za Serikali ya Jamhuri ya Burundi kwa Mahakama Kigoma, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kitaasisi katika nyanja za sheria, haki, na usalama wa wananchi wa nchi hizo mbili Tanzania na Burundi ambao wamekuwa wakiishi kwa amani na udugu wa karibu mkoani Kigoma.

Vile vile alimjulisha Mhe. Rwizile kuwa, Rais wa Jamhuri ya Burundi amependa kumuongezea muda wa kuendelea kufanya kazi katika nafasi hiyo ya Balozi ili kuhudumu katika ubalozi mdogo hapa nchini, uamuzi unaolenga kuendeleza kazi.

“Naleta salamu maalum kutoka Serikali ya Jamhuri ya Burundi kwa lengo la kuendeleza na kuimarisha uhusiano mwema na ushirikiano wa kitaasisi baina yetu, hasa katika masuala yanayohusu huduma za kisheria na kijamii mkoani Kigoma, mahusiano haya thabiti yanazidi kuchochea amani, usalama na ushirikiano mzuri kwa wananchi wetu wanaoishi na kufanya shughuli zao mkoani Kigoma,” alisema Balozi huyo.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Augustine Rwizile alimkaribisha na kumpongeza Balozi huyo kwa kuongezewa muda wa kazi, akibainisha utayari wa Mahakama Kuu Kigoma kuendelea kushirikiana ki-taasisi ili kuhakikisha haki inatendeka na ustawi wa jamii unalindwa.

“Ziara hii inazidi kuimarisha daraja la kidiplomasia na udugu uliopo kati ya Tanzania na Burundi, ikithibitisha dhamira ya dhati ya Viongozi wa nchi hizi katika kudumisha amani na maendeleo endelevu,” alisema Jaji Rwizile.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (kulia) akiwa katika mazungumzo Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Burundi, Bw. Kekenwa Jeremia alipotembelewa na Balozi huyo ofisini kwake Mahakama Kuu Kigoma tarehe 04 Septemba, 2026.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na mgeni wake Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Burundi, Bw. Kekenwa Jeremia (hayupo katika picha).


Mazungumzo yakiendelea. Kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (kulia), wa pili kulia ni Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Burundi nchini Tanzania mkoani Kigoma, Bw. Kekenwa Jeremia, wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa, wa pili kushoto ni Msaidizi wa Balozi Mdogo wa Burundi Mkoani Kigoma, Bw. Nininahazwe Adalbert.

Picha ya Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Burundi nchini Tanzania Mkoani Kigoma, Bw. Kekenwa Jeremia (katikati). Kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Fadhili  Mbelwa na kushoto ni Msaidizi wa Balozi Mdogo wa Burundi Mkoani Kigoma, Bw. Nininahazwe Adalbert.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni