Alhamisi, 24 Septemba 2026

HAKIMU MKAZI MSTAAFU EPHRAIM KIBONA AFANYIWA HAFLA YA KUAGWA

Na MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya

Viongozi na watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya wamekutana na kufanya hafla ya kumuaga Hakimu Mkazi Mstaafu Mhe. Ephraim Joel Kibona, ambaye amestaafu Utumishi wa Umma baada ya kuitumikia Mahakama ya Tanzania kwa kipindi cha miaka 25 jambo linaloashiria utumishi uliotukuka.

Mhe. Kibona ameitumikia Mahakama kwa muda mrefu, ambapo katika sehemu kubwa ya utumishi wake alihudumu kama Msaidizi wa Kumbukumbu na Msimamizi wa Kitengo cha Jinai katika Mahakama Kuu Mbeya. Baada ya kujiendeleza kielimu, alibadilishwa kada na kuwa Hakimu Mkazi mwaka 2026, nafasi ambayo ameendelea kuitumikia hadi alipostaafu akiwa bado anahudumu Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya.

Akizungumza katika hafla hiyo, Hakimu Mkazi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Sarah Mungure ambaye alifanya kazi na Mhe. Kibona katika Masjala ya Jinai, alimshukuru kwa utumishi wake na kueleza kuwa amekuwa mtumishi mwenye sifa ya utiifu, uadilifu na unyenyekevu. 

“Tunashukuru kwa utumishi wako uliotukuka. Tunakutakia kila la heri, uwe na afya njema na Mungu azidi kukubariki. Uendeleze tabia ya utiifu, uadilifu na unyenyekevu wakati wote huko uendako nje ya maisha ya utumishi. Nasi kama watumishi wenzako tunakuomba radhi pale tulipokukosea na Mungu azidi kutuunganisha,” alisema Mhe. Mungure.

Kwa upande wake, Mhe. Kibona alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumpa afya na uhai katika kipindi chote cha utumishi wake, huku akitoa shukrani kwa viongozi na watumishi wenzake kwa ushirikiano alioupata katika kutekeleza majukumu ya kiutumishi na kijamii.

“Ninamshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa uzima na uhai tangu nilipoianza safari yangu ya kuajiriwa hadi sasa ninapostaafu utumishi. Nawashukuru viongozi na watumishi wenzangu kwa kushirikiana nami katika majukumu ya kiutumishi na kijamii pia …

… Ninatambua kuwa changamoto katika utumishi wa umma hazikosekani. Ninawaombeni radhi viongozi na watumishi wenzangu na pale nilipokosea naomba mnisamehe. Nawatakieni kila la heri, tuzidi kuendeleza na kudumisha upendo uliojengeka baina yetu,” alisema Mhe. Kibona

Nao, Viongozi na Watumishi walimtakia maisha mema baada ya kustaafu, kuendelea kudumisha mahusiano mema yaliyojengwa katika kipindi chake cha utumishi, huku wakimtakia afya njema, amani na baraka katika hatua hiyo mpya ya maisha.

Hatua ya kustaafu kwa Mhe. Kibona inaashiria mwisho wa safari yake ya utumishi rasmi, lakini pia mwanzo wa ukurasa mpya wa maisha unaobeba kumbukumbu ya mchango wake katika Mahakama ya Tanzania.

Hafla hiyo fupi ya kumuaga ilihudhuriwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Fahamu Mtulya, Majaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Angaza Mwipopo, Mhe. Mussa Pomo na Mhe. Saidi Kalunde, Naibu Msajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Bernard Mpepo, Mahakimu, Maafisa pamoja na watumishi wa kada mbalimbali.

Hakimu Mkazi Mstaafu Mhe. Ephraim Kibona (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya (wa pili kushoto) ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Fahamu Mtulya, (wa kwanza kushoto) ni Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Mussa Pomo, (wa pili kulia) ni Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Angaza Mwipopo, (wa kwanza kulia) ni Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Said Kalunde.

Viongozi na watumishi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya wamekutana na kufanya hafla ya kumuaga Hakimu Mkazi Mstaafu Mhe. Ephraim Joel Kibona katika ukumbi wa Mahakama Kuu Mbeya.

Viongozi na watumishi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya wamekutana na kufanya hafla ya kumuaga Hakimu Mkazi Mstaafu Mhe. Ephraim Joel Kibona katika ukumbi wa Mahakama Kuu Mbeya.

Mstaafu Ephraim Kibona (katikati) akikabidhiwa keki yenye nembo ya Timu yake pendwa kutoka kwa waheshimiwa Majaji.

Mstaafu Ephraim Kibona akifanya maandalizi ya kufungua shampeni wakati wa hafla hiyo.

Mstaafu Ephraim Kibona (katikati) akikabidhiwa zawadi ya Jezi ya Timu yake pendwa kutoka kwa waheshimiwa Majaji.

Mstaafu Ephraim Kibona akimlisha keki Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Mussa Pomo.

Mstaafu Ephraim Kibona akilishwa keki na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Fahamu Mtulya.

Mstaafu Ephraim Kibona (kulia) akikata keki katika hafla ya kuagwa kwake.

Waheshimiwa Majaji wakiwa wameketi katika hafla hiyo wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Fahamu Mtulya (wa pili kulia)

Hakimu Mkazi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Sarah Mungure, (aliyesimama) akitoa neno la pongezi na shukurani kwa Mstaafu.

Naibu Msajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Bernard Mpepo, akitoa neno la shukurani katika hafla hiyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Fahamu Mtulya (katikati) akizungumza machache wakati wa hafla hiyo.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni