- Yagawa dozi ya bao mbilimbili kwa mechi za ufunguzi
- Jaji Mongella awahimiza kuendeleza moto huohuo
NA
PAUL PASCAL, Mahakama-Moshi
Timu
ya Mahamaka Sports Club inayoshiriki mashindano ya Shirikisho la Michezo ya
Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) kwa mwaka, 2026 imefanikiwa kuyaanza vema mashindano hayo kwa
ushindi mnono katika michezo yake iliyocheza tarehe 23 na 24 Septemba, 2026.
Michezo hiyo inaendelea kufanyika mkoani Kilimanjaro katika Viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi na katika viwanja Viwanja vya Moshi Club.
Michezo
iliyochezwa ni Mpira wa Miguu kwa Wanaume ambapo Timu ya Mahakama iliweza
kuibuka na ushindi wa magoli Mawili dhidi ya goli moja la kufutia machozi
kutoka Timu ya Mpira ya TAKUKURU huku Timu ya Kamba Wanaume wakiwaburuza
ipasavyo kwa pointi mbili kwa nunge Timu ya Katibu Tawala Mkoa wa Lindi sambamba
na kipigo hicho kwa Mkoa wa Lindi Timu ya Mahakama Kamba kwa wanawake waliwafurusha
pasi na huruma kwa pointi mbili timu ya wanawake kutoka Ofisi ya Katibu Tawala
Mkoa wa Kilimanjaro.
Hali
kama hiyo imeendelea leo tarehe 24 Septemba, 2026 ambapo Timu ya Mahakama Mpira
wa Pete kwa Wanawake imeshinda kwa jumla ya pointi 43 dhidi ya pointi 03 za Timu
ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).
Baada
ya kukamilika kwa ratiba hiyo ya mwanzo kwa michezo ya awali, Viongozi na Wachezaji
wote wa Timu ya Mahakama Sports Club wamefika katika Ofisi ya Jaji Mfawidhi
Mahakama Kuu Masjala Ndogo Moshi leo tarehe 24 Septemba, 2026 kwa ajili ya kuzungumza machache na kutiana
moyo kwa michezo inayofuatia.
Akizungumza
kwa niaba ya Viongozi na Wachezaji, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Club, Mhe. Martin Mushi amemueleza Jaji Mfawidhi, Mhe. Dkt. Lillian Mongella kuwa, wao
kama watumishi wa Mahakama ya Tanzania wamefika Kilimanjaro ili kuweza
kuwakikilisha na kuitetea Mahakama kwa nguvu zote katika mashindano hayo.
“Mhe
Jaji Mfawidhi Timu yetu ya Mahakama Sports Club imekuja na jumla ya Wachezaji
82 ambao watashiriki michezo ya Mpira wa Miguu, Mpira wa Pete, Kuvuta Kamba Wanaume
na Wanawake, Riadha Wanaume na Wanawake, Kuendesha Baiskeli Wanaume na Wanawake
pamoja na michezo yote ya ndani iliyoandaliwa na SHIMIWI kwa mwaka huu,” amesema
Mhe. Mushi.
Mhe.
Mushi aliongeza kwa kumueleza Jaji Mfawidhi kuwa, “tunapenda kukujulisha kuwa,
mpaka sasa Timu yetu ya Mahakama Sports Clubs haijapoteza mchezo wowote na
tunakuahidi na tunaahidi kwa Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kuwa
hatutowaangusha.”
Kwa
upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Moshi, Mhe.
Dkt Lillian Mongella aliwapongeza Viongozi na Wanamichezo wote na kuwaahidi
kushirikiana nao katika mashindano hayo ili lengo la Timu ya Mahakama liweze kutimia.
“Nianze
kwa kupongeza juhudi mlizoonesha kwa ushindi mnono tulioupata mpaka sasa
niwasihi juhudi hizo ziendelee mpaka tutakapochukua makombe mengi kadri
inavyowezekana, niwahakikishie ushirikiano katika kufikia malengo hayo ya timu
yetu naamini tukiunganisha nguvu zetu tunakwenda kuipeperusha vema bendera yetu
ya Mahakama,” alisema Jaji Mongella.
Mashindano ya SHIMIWI yanafanyikia Mkoani Kilimanjaro kuanzia tarehe 21 Septemba 2026 na yatafikia tamati tarehe 07 Oktoba, 2026 yakihusisha Timu za michezo mbalimbali zipatazo 64.
Viongozi wa Mahakama Sports wakisaini Kitabu cha wageni wakiongozwa na Mwenyekiti wa Timu hiyo, Mhe Martin Mushi (mwenye kitabu) mara baada ya kuwasiii katika Ofisi ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Moshi, Mhe. Dkt. Lillian Mongella (aliyeketi mbele) leo tarehe 24 Septemba, 2026.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni