Alhamisi, 24 Septemba 2026

JAJI NGUNYALE AWAAPISHA WASULUHISHI, WAAMUZI WA CMA BUKOBA

 Na MICHAEL RITTE, Mahakama – Bukoba

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Bukoba, Mhe. David Ngunyale amewaapisha Wasuluhishi na Waamuzi kutoka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Bukoba hatua inayofungua rasmi ukurasa wa utendaji kazi kwa Wasuluhishi na Waamuzi hao.

Hafla ya Uapisho huo ilifanyika tarehe 23 Septemba, 2026 Mahakama Kuu ya Bukoba ambapo mara baada ya kuwaapisha Maofisa hao, Jaji Ngunyale alisema, kiapo hicho, ni msingi wa maadili ya usuluhishi, na kwamba ni muhimu kuzingatia misingi ya maadili ya dini kutokana na kwamba kazi ya usuluhishi inagusa kutatua changamoto za watu wanaowazunguka.

“Kiapo hiki ni msingi wa maadili ya usuluhishi. Yatupasa kuzingatia misingi ya maadili ya dini zetu, ambapo kazi ya usuluhishi inagusa kutatua changamoto za watu wanaotuzunguka. Inatupasa kuzingatia utoaji haki, maana huathiri mnyororo wa maisha ya mtu, ambaye ni jamii, watu wanaomzunguka na familia. Asipopata haki yake ipasavyo, vivyo hivyo akipata haki yake kwa wakati, mnyororo wake utakuwa nafuu,” alisema Jaji Ngunyale huku akiwasihi kumuomba Mungu awasaidie kutenda haki.

Jaji Ngunyale alieleza kwamba, utoaji haki mapema ipasavyo una athari kubwa kwa mtu binafsi, familia yake, watu wanaomzunguka na jamii kwa ujumla, hivyo Wasuluhishi na Waamuzi wanapaswa kuwa mfano wa haki katika utendaji wao wa kila siku.

Aidha, aliwashukuru waliohudhuria kwa kuzingatia utaratibu uliowafikisha katika hatua hiyo ya uapisho, na kuwahimiza kuendelea kushirikiana katika mambo yanayowaunganisha, huku akiwasihi kumuomba Mungu ili kuwasaidia kutenda haki.

 

Jaji Mfawidhi Mahakama wa Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Bukoba, Mhe. David Ngunyale akiwaapisha Wasuluhishi na Waamuzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi tarehe 23 Septemba, 2026 Mahakama Kuu Bukoba. 

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Bukoba, Mhe. David Ngunyale akizungumza mara baada ya kuwaapisha Wasuluhishi na Waamuzi wa CMA tarehe 23 Septemba, 2026. 

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Bukoba, Mhe. Andrew Kabuka  akizungumza na kutoa neno la shukrani baada ya uapisho wa Wasuluhishi (Mediators) na Waamuzi(Abitrators). Pembeni yake ni sehemu ya waliohudhuria Uapisho wa  Wasuluhishi na Waamuzi wa CMA Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Bukoba tarehe 23 Septemba, 2026.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo  Bukoba, Mhe. David Ngunyale (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wasuluhishi na Waamuzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) (waliosimama nyuma) mara baada ya uapisho wao uliofanyika Mahakama Kuu ya Bukoba. Aliyeketi kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Bukoba, Mhe Said Mkasiwa na kulia ni Msuluhishi Muandamizi kutoka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi Bukoba (CMA),Wakili Godwin Migile.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni