Jumapili, 27 Septemba 2026

JAJI DING’OHI AKAGUA MAHAKAMA, MAGEREZA MTWARA

Na MWANDISHI WETU-Mahakama, Mtwara

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Mtwara, Mhe. Said Ding’ohi, amefanya ziara ya ukaguzi wa shughuli za Mahakama katika Mkoa wa Mtwara, ili kutathmini utendaji kazi, kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi pamoja na kuangalia namna ya kuendelea kuboresha huduma za utoaji haki kwa wananchi.

Katika ziara hiyo, Mhe. Ding’ohi aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama, Mhe. Seraphine Nsana, Mtendaji wa Mahakama Mtwara, Bw. Lucas Jang’andu pamoja na viongozi wengine.

Ziara hiyo ilianza kwa kukagua Gereza Kuu la Lilungu lililopo Mtwara Mjini, ambapo Jaji Ding’ohi alipata fursa ya kuzungumza na Askari Magereza na kupata taarifa fupi kuhusu hali ya Gereza hilo.

Aidha, alikutana na wafungwa na mahabusu waliopo katika Gereza hilo, ambapo alisikiliza maoni, changamoto na masuala mbalimbali yanayowakabili.

Mhe. Ding’ohi pia alitembelea Mahabusu ya Watoto iliyopo Mtwara Mjini, ambapo alikutana na watumishi wanaosimamia watoto hao na kujionea mazingira wanayoishi.

Ziara hiyo ilitoa fursa ya kufahamu hali ya huduma zinazotolewa kwa watoto waliopo mahabusu pamoja na changamoto zinazohitaji kupewa kipaumbele.

Baada ya hapo, Jaji Ding’ohi aliendelea na ziara katika Mahakama ya Mkoa wa Mtwara, Mahakama za Wilaya za Mtwara Mjini, Tandahimba, Newala, Nanyumbu na Masasi, pamoja na Mahakama za Mwanzo za Dihimba, Mpapura, Mnyawa, Kitangari, Newala na Mchauru.

Katika kila kituo, Mhe. Ding’ohi alipokea taarifa fupi kuhusu utendaji wa Mahakama, mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zinazowakabili watumishi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Miongoni mwa mafanikio yaliyoelezwa katika vituo hivyo ni matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika shughuli za Mahakama, hatua ambayo imeendelea kurahisisha baadhi ya shughuli za utoaji haki na usimamizi wa mashauri.

Aidha, ilielezwa kuwa vituo hivyo vinaendelea kufanya juhudi kuhakikisha mashauri yanasikilizwa mapema ipasavyo na kuepuka mlundikano wa mashauri.

Watumishi pia wanashiriki katika utoaji wa elimu ya sheria kwa wananchi kupitia vipindi vya redio na katika shule, ikiwa ni sehemu ya kuwafikia wananchi na kuwaelimisha kuhusu masuala mbalimbali ya sheria na huduma za Mahakama.

Pamoja na mafanikio yaliyopo, ziara hiyo ilibainisha changamoto mbalimbali zinazokabili Mahakama Mtwara, hususan katika baadhi ya Mahakama za Mwanzo.

Miongoni mwa changamoto hizo ni uchakavu wa majengo ya baadhi ya Mahakama za Mwanzo ambazo zilijengwa muda mrefu, hali inayohitaji matengenezo au ujenzi wa majengo mapya yenye mazingira bora kwa ajili ya utoaji huduma za haki.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa vitendea kazi, hasa katika baadhi ya Mahakama za Mwanzo, pamoja na baadhi ya vituo kutokuwa na upatikanaji wa umeme.

Aidha, ilibainishwa changamoto ya uchakavu wa vyombo vya usafiri, hususan pikipiki zinazotumika kuwawezesha watumishi kufikia maeneo mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumza na watumishi katika vituo mbalimbali, Jaji Ding’ohi aliwasisitiza kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uwajibikaji, weledi na uadilifu, huku wakizingatia wajibu wao wa kuitumikia jamii katika kuhakikisha wananchi wanapata haki mapema ipasavyo.

Aliwasisitiza watumishi kuendelea kutumia mifumo ya TEHAMA iliyopo na kuwahamasisha wananchi kuelewa na kutumia huduma zinazopatikana kupitia mifumo hiyo, hatua ambayo inaweza kusaidia kurahisisha upatikanaji wa huduma za Mahakama.

Aidha, Mhe. Ding’ohi aliwapongeza Mahakimu pamoja na watumishi wa Mahakama kwa kujituma katika utekelezaji wa majukumu yao na kwa juhudi wanazofanya katika kuhakikisha mashauri yanashughulikiwa kwa wakati.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Mtwara, Mhe. Said Ding’ohi, akisalimiana na mmoja wa watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Kitangari wakati wa mapokezi.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Mtwara, Mhe. Said Ding’ohi, akisaini kwenye daftari la wageni waliofika Mahakama ya Mwanzo Kitangari.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Mtwara, Mhe. Said Ding’ohi, (mstari wa mbele wa tatu kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja baada ya ukaguzi katika Mahakama ya Mwanzo Kitangari.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Mtwara, Mhe. Said Ding’ohi, akisalimiana na mmoja wa watumishi wa Mahakama ya Wilaya Tandahimba wakati wa mapokezi.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Mtwara, Mhe. Said Ding’ohi, (katikati) akwa kwenye picha ya pamoja wakati wa ukaguzi wa Mahakama ya Mwanzo Dihimba.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Mtwara, Mhe. Said Ding’ohi, (katikati mstari wa mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa ukaguzi wa Gereza Kuu Lilungu lilipo Wilaya ya Mtwara Mjini.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Mtwara, Mhe. Said Ding’ohi, (katikati mstari wa mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mahabusu ya watoto iliyopo Wilaya ya Mtwara mjini.

 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Mtwara, Mhe. Said Ding’ohi, akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mahamaka ya Mwanzo Mnyawa ambapo alipanda mti wa kumbukumbu.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Mtwara, Mhe. Said Ding’ohi, (aliyekaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Newala.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Mtwara, Mhe. Said Ding’ohi, (wa pili kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Tandahimba.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Mtwara, Mhe. Said Ding’ohi,  (katikati mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja katika Mahakama ya Mwanzo Nanyumbu.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Mtwara, Mhe. Said Ding’ohi, (kushoto) akikagua ujenzi wa jengo jipya la Mahakama ya Wilaya Masasi.

 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Mtwara, Mhe. Said Ding’ohi, akikagua jengo jipya lilijengwa la Mahama ya Mwanzo Mchauru.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dubai.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni