· Awataka Watumishi kutooneana wivu, kuinuana na kupendana
Na EVA
LESHANGE & AMIRI BAKARI, Mahakama - Singida
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Singida, Mhe. Ayoub Mwenda
amewataka Watumishi wa Mahakama mkoani humo kutooneana wivu na kufanyiana
hujuma badala yake wadumishe ushirikiano, upendo na mshikamano mahali pa kazi ili
kuongeza ufanisi katika utoaji haki kwa wananchi.
Mhe. Mwenda
aliyasema hayo tarehe 07 Septemba, 2026 alipokuwa wilayani Manyoni katika ziara
yake ya ukaguzi wa shughuli za Mahakama kwa robo ya kwanza mkoani Singida.
Ziara hiyo ilianzia katika Mahakama za Mwanzo za Mwamagembe, Rungwa na Mgandu
zilizopo Wilaya ya Manyoni na kumalizia kwenye Mahakama ya Wilaya Manyoni.
Akizungumzia
msingi wa utendaji kazi mwema, Jaji Mwenda alisema kuwa, ushirikiano wa dhati
na kupendana ndiyo nguzo kuu inayowafanya watumishi kufanya makubwa hata pale
wanapokuwa wachache.
"Acheni
kuoneana wivu, ombeaneni mema, pendaneni na hamasishaneni na msifanyiane hujuma.
Kila mmoja amsapoti mwenzake," alisisitiza Jaji Mfawidhi huyo.
Mhe.
Mwenda aliongeza kuwa, mshikamano huo unapaswa kuonekana baina ya ngazi zote za
Uongozi na Watumishi wa kawaida, na kusisitiza kwa kusema, "tusaidiane, wa
chini amsaidie bosi wake azidi kupanda, na bosi pia awasaidie wa chini yake
wazidi kupanda."
Akitoa
pongezi kwa watumishi wa Mahakama alizotembelea, Jaji Mfawidhi huyo alisema,
"nichukue nafasi hii kuwapongeza Mahakimu na Watumishi wote kwa kufanya
kazi kwa ushirikiano bila kujali uchache wenu. Pamoja na uchache wenu, ni vema
tukafanya kazi kwa weledi, kujituma, kuwajibika na kuhakikisha haki inapatikana
kwa wananchi mapema ipasavyo kwani ndio lengo kuu la Mahakama."
Katika
ziara hiyo, Mhe. Mwenda alieleza kwamba, kipimo halisi cha utendaji kazi mzuri
kinatokana na mrejesho (feedback) kutoka kwa Wadau wa Mahakama, hususan Jeshi
la Magereza (Wafungwa na Mahabusu) pamoja na Mkuu wa Wilaya. Alieleza kuwa,
alipita kwa Mkuu wa Wilaya ya Manyoni na kupata mrejesho chanya kuhusu utendaji
kazi wa Mahakama hizo.
Ili
kuendelea kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama, Jaji Mwenda aliwataka
watumishi hao kuongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri bila kuvunja sheria na
miongozo, na kuweka mikakati thabiti ya kuondoa mlundikano wa mashauri (case backlog).
Mbali
na kuzungumza na watumishi, Mhe. Mwenda alitembelea Mradi wa Ujenzi wa Mahakama
ya Mwanzo Rungwa unaoendelea tangu mwaka 2024 ambapo alipata wasaa wa
kuzungumza na Mkandarasi Emmanuel Mchaki na kubaini changamoto zinazochelewesha
mradi huo kuwa, ni pamoja na upatikanaji wa vifaa, na nguvu kazi.
Mkandarasi
wa Mradi huo alisema kuwa, ameshafikia zaidi ya asilimia 40 ya ujenzi huo na
ameahidi kumaliza ujenzi huo kwani kwa kiwango kikubwa vifaa (materials) tayari
vipo eneo la mradi huo.
Jaji
Mwenda alimshauri Mkandarasi kutumia nguvu kazi kutoka maeneo ya jirani na
mradi ili kuimarisha uhusiano mwema kati ya jamii na Mahakama.
Ziara hiyo ya ukaguzi inatarajiwa kuendelea katika Mahakama za Wilaya za Iramba, Mkalama pamoja na Mahakama zake za Mwanzo na Mahakama ya Wilaya Singida pamoja na Mahakama zake za Mwanzo pamoja na Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Singida, Mhe. Ayoub Mwenda akipokelewa na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Manyoni alipowasili katika Mahakama hiyo tarehe 07 Septemba, 2026 kwa ziara ya kikazi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Singida, Mhe. Ayoub Mwenda (katikati) akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Manyoni (hawapo katika picha) alipokuwa katika ziara ya kikazi. Kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Singida, Mhe. Jasmine Abdul na kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Manyoni, Mhe. Alisile Mwankejela.
Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Manyoni wakifuatilia kikao kilichokuwa kikiendelea kwenye Ukumbi wa Mahakama ya Wilaya ya Manyoni tarehe 07 Septemba, 2026.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Singida, Mhe. Ayoub Mwenda (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Manyoni mara baada ya kufanya Ukaguzi katika Mahakama hiyo. Wa kwanza kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Singida, Bw. Filbert Matotay, wa pili kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Singida, Mhe. Jasmine Abdul na wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Manyoni, Mhe. Alisile Mwankejela.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Singida, Mhe. Ayoub Mwenda (aliyevaa tai nyekundu) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Haki Jinai alioambatana nao kukagua Gereza la Mahakama ya Wilaya Singida.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Singida, Mhe. Ayoub Mwenda (wa kwanza kushoto) akiongoza ukaguzi Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Rungwa. Wa pili kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Singida, Bw. Filbert Matotay, akifuatiwa na Mkandarasi wa Mradi huo pamoja na Viongozi wengine walioambatana na Jaji Mfawidhi wakati wa ukaguzi wa Mradi huo.
Muonekano wa Jengo la Mahakama ya Mwanzo Rungwa lililopo katika Wilaya ya Manyoni linaloendelea na ujenzi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Singida, Mhe. Ayoub Mwenda akitoa ushauri kwa
mkandarasi katika mradi wa mahakama ya mwanzo
Rungwa katika wilaya ya Manyoni.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni