Alhamisi, 10 Septemba 2026

JAJI MWENEMPAZI AMUAPISHA OFISA USULUHISHI NA UAMUZI

Na SHARIFU MOKIWA - Mahakama Sumbawanga

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Sumbawanga Mhe. Thadeo Mwenempazi, amemuapisha Bw. Ayubu Joseph Mniko kuwa Msuluhishi na Muamuzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Mkoa wa Rukwa.

Uapisho huo umefanyika tarehe 9 Septemba, 2026, katika Ofisi ya Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga na kuhudhuriwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Sumbawanga, Mhe. Pamela Mazengo, pamoja na Afisa Mfawidhi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Mkoa wa Rukwa Bi. Salome Kamwela.

Akizungumza baada ya kumuapisha Bw. Mniko, Mhe. Mwenempazi amesema anatarajia kwamba, katika utekelezaji wa majukumu yake atatenda haki bila upendeleo na kuhakikisha haki inatolewa kwa wakati mapema ipasavyo.

Mhe. Mwenempazi amemtaka Bw. Mniko kujipanga na kuwa tayari katika kutekeleza majukumu yake, akisisitiza umuhimu wa kuwa na utayari wa kuwaelewesha wananchi pale wanapokuwa hawajaelewa masuala mbalimbali yanayohusu majukumu yake ili kuepusha malalamiko na minong’ono inayoweza kujitokeza kutokana na kutokuelewana kwa wadaawa.

“Anatakiwa kutenda haki, kutokuwa na upendeleo na kutoa haki kwa wakati. Pia anatakiwa kujipanga na kuwa tayari kwa kuwa wakati mwingine watu hawajui, hivyo asione shida kumuelewesha mtu ili kuepusha minong’ono,” amesema Mhe. Mwenempazi.

Kwa upande wake, Bw. Mniko amesema kipaumbele chake katika kutekeleza majukumu yake katika nafasi hiyo ni kuhakikisha anatimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na kutenda haki.

“Nitahakikisha natimiza majukumu yangu kama sheria inavyonitaka na kutenda haki,” amesema Bw. Mniko.

Uapisho huo ni sehemu ya taratibu za kumuwezesha Bw. Mniko kuanza kutekeleza majukumu yake katika nafasi ya Msuluhishi na Muamuzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Mkoa wa Rukwa, kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazotawala utekelezaji wa majukumu hayo.






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni