Ijumaa, 11 Septemba 2026

WATUMISHI MAHAKAMA MANYARA WAFANYA ZIARA YA MAFUNZO GEITA

Na DOTTO NKAJA-Mahakama, Geita

Katika kuendelea kuimarisha ufanisi wa utendaji kazi na kuboresha utoaji wa haki nchini, watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Manyara, wamefanya ziara ya mafunzo na kubadilishana uzoefu katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Geita.

Ziara hiyo iliyofanyika Septemba 7 na 8, 2026, imelenga kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika uratibu na uendeshaji wa mashauri, pamoja na shughuli za kiutawala.

Ujumbe wa Mahakama Manyara uliongozwa na Jaji Mfawidhi, Mhe. Dkt. Adam Mambi na ulihusisha Naibu Wasajili, Mtendaji, Hakimu, Maafisa Rasilimali Watu na Utawala, Mkaguzi wa Ndani, Madereva pamoja na watumishi wengine kutoka vituo mbalimbali vya Masjala hiyo.

Akizungumza wakati wa kuupokea ujumbe huo katika Ukumbi wa Mafunzo wa Mahakama Kuu Geita, Jaji Mfawidhi, Mhe. Projestus Kahyoza, aliwakaribisha na kuwapongeza viongozi na watumishi wa Manyara kwa kuichagua Geita kuwa kituo cha kujifunza na kubadilishana uzoefu.

“Tunawakaribisha sana ndugu zetu kutoka Manyara. Hapa ni mahali sahihi kwenu kujifunza. Tumekuwa tukiwezesha Mahakama kutoka maeneo mbalimbali kupata mafunzo na kubadilishana uzoefu katika masuala ya TEHAMA kwa lengo la kuboresha utoaji wa haki. Nanyi mtajifunza kutoka kwetu na sisi pia tutajifunza kutoka kwenu,” alisema Mhe. Kahyoza.

Kwa upande wake, Mhe. Dkt. Mambi aliipongeza Mahakama Kuu Geita kwa mapokezi mazuri na kueleza kuwa mafanikio yaliyopatikana katika matumizi ya TEHAMA ndiyo yaliyowavutia kufanya ziara hiyo.

“Tumesikia mambo mazuri ambayo Wanageita mnayafanya katika mapinduzi ya matumizi ya TEHAMA. Hivyo, tukaona ni vema tufike tujifunze kutoka kwenu na pia tushirikiane uzoefu wa Masjala zetu ili tuboreshe utendaji wetu wa kila siku,” alisema Mhe. Dkt. Mambi.

Katika ziara hiyo, watumishi wa Mahakama Kuu Geita, waliwasilisha mada mbalimbali kuhusu matumizi ya TEHAMA katika shughuli za kimahakama na kiutawala.

Miongoni mwa mada zilizowasilishwa ni matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa mashauri, unaowezesha uendeshaji wa mashauri kwa njia ya kielektroniki bila kutegemea matumizi ya karatasi. Mada hiyo iliwasilishwa na Naibu Msajili wa Masjala Ndogo Geita, Mhe. Fredrick Lukuna.

Washiriki pia walijifunza namna Mahakama za Wilaya zinavyotumia mifumo ya TEHAMA katika kutekeleza shughuli za kimahakama na kiutawala, pamoja na hatua zinazochukuliwa na Mahakama za Mwanzo katika kupunguza matumizi ya karatasi, kupitia mfumo wa Mahakama za Mwanzo Electronic Register.

Aidha, washiriki walipata fursa ya kujifunza namna huduma ya Kiosk inavyofanya kazi kwa kuwasaidia wananchi ambao hawana uelewa wa kutosha kuhusu matumizi ya TEHAMA ili waweze kupata huduma za kimahakama kwa urahisi. Mada hiyo iliwasilishwa na Afisa Kumbukumbu, Bi. Winfrida Warsha.

Kwa upande wa shughuli za kiutawala, Mtendaji wa Mahakama Geita, Bi. Masalu Kisasila, aliwasilisha mada kuhusu namna Mahakama hiyo ilivyopunguza na kuachana na matumizi ya karatasi katika shughuli mbalimbali za kiutawala kupitia matumizi ya mifumo ya kielektroniki.

Naye Afisa TEHAMA, Bw. Dotto Nkaja, aliwasilisha mifumo mbalimbali iliyobuniwa na Mahakama Geita kwa lengo la kurahisisha upatikanaji, uhifadhi na matumizi ya taarifa za kimahakama. Mifumo hiyo ni pamoja na Geita Repository Database, Geita Electronic Visitors na Geita Legal Decisions.

Katika kuendeleza mafunzo hayo, Septemba 8, 2026, Mhe. Dkt. Mambi, aliwasilisha mada kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa, ikiwemo Akili Bandia (Artificial Intelligence – AI), katika kufanya tafiti za kimahakama pamoja na maadili yanayopaswa kuzingatiwa katika matumizi ya AI wakati wa tafiti na uratibu wa mashauri mahakamani.

Mada hiyo iliwapa washiriki fursa ya kutafakari namna teknolojia mpya zinavyoweza kutumika kuongeza ufanisi katika shughuli za Mahakama, huku wakizingatia misingi ya maadili na utoaji wa haki.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya ujumbe huo, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Manyara, Mhe. Charles Mnzava, aliwapongeza watumishi wa Geita kwa bidii na weledi wao, akieleza kuwa juhudi hizo zimechangia kuboresha utendaji kazi na kupunguza mlundikano wa mashauri.

“Kwa kweli tumeona jitihada zenu katika usikilizwaji wa mashauri ya kila siku, lakini pia katika usimamizi wa rasilimali. Tunaahidi kutumia elimu tuliyoipata katika kuboresha utendaji wetu tutakaporejea Manyara,” alisema Mhe. Mnzava.

Ziara hiyo imehitimishwa kwa viongozi wa Masjala hizo mbili kuweka mikakati ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati yao, ikiwemo kuanzisha utaratibu wa kuwa Kanda Rafiki katika masuala ya kikazi, kijamii na kiutawala.

Aidha, Uongozi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Geita, umeahidi kufanya ziara ya kimafunzo katika Mkoa wa Manyara hivi karibuni. Hatua hiyo inatarajiwa kuendeleza na kuimarisha utamaduni wa kujifunza, kushirikishana uzoefu na kubadilishana mbinu bora za utendaji kazi ndani ya Mahakama.

Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika Mahakama na kuhakikisha teknolojia inatumika ipasavyo katika kuongeza ufanisi, kurahisisha upatikanaji wa huduma za haki na kuboresha utoaji wa haki kwa wananchi.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita, Mhe. Projestus Kahyoza, akiwakaribisha wageni kutoka Masjala Ndogo Manyara.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Manyara, Mhe. Dkt. Adam Mambi, akitoa elimu kwa watumishi waliohudhuria mafunzo katika Ukumbi wa Mafunzo wa Mahakama Kuu Geita, huku wengine wakishiriki kwa njia ya mtandao (Video Conference), kuhusu matumizi ya Kanuni za Ushahidi wa Kielektroniki pamoja na sheria zinazohusu matumizi sahihi ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence – AI).



Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Geita, Mhe. Fredrick Lukuna, akieleza namna Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri unavyorahisisha usikilizaji na uendeshaji wa mashauri, pamoja na kupunguza matumizi ya karatasi mahakamani.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Geita, Bi. Masalu Kisasila, akielezea namna matumizi ya TEHAMA yanavyorahisisha na kuboresha utekelezaji wa shughuli za kiutawala Mahakamani.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Manyara, Mhe. Charles Mnzava, akitoa shukrani baada ya kukamilika kwa mafunzo.

Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Geita, Mhe. Projestus Kahyoza (kulia) na Mhe. Griffin Mwakapeje (kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Manyara, Mhe. Dkt. Adam Mambi.


Picha ya pamoja ya viongozi na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo za Geita na Manyara, katika Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Geita.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni