Ijumaa, 18 Septemba 2026

JAJI MTULYA AKUTANA NA MKUU WA MKOA MBEYA

    .Asisitiza Ushirikiano katika kuimarisha utendaji kazi

Na MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya amefanya ziara ya kikazi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Jumanne Abdallah Sagini, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha ushirikiano na uhusiano baina ya Mahakama na Ofisi hiyo ili kuwezesha utendaji bora wa shughuli za kimahakama.

Ziara hiyo imelenga pia kujitambulisha kwa Mkuu wa Mkoa pamoja na kujadili changamoto mbalimbali za kiutawala zinazohusiana na utendaji wa Mahakama katika Masjala hiyo, hususan masuala yanayohitaji ushirikiano na mamlaka za Serikali ya Mkoa, Halmashauri, Kata na Vijiji.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe. Mtulya, alieleza kuwa baadhi ya maeneo na miundombinu ya Mahakama katika Mkoa wa Mbeya yamekuwa yakiingiliwa na mamlaka nyingine bila ushirikishwaji wa Mahakama, hali ambayo inaweza kuathiri matumizi na ulinzi wa mali na maeneo ya Mahakama.

Katika ziara hiyo, Jaji Mfawidhi pia alitoa pongezi kwa Diwani wa Kata ya Makongolosi kwa jitihada za kuwashirikisha wananchi na wadau mbalimbali katika ujenzi wa jengo jipya la Mahakama ya Mwanzo Makongolosi, baada ya jengo la awali kuharibiwa wakati wa ghasia zilizotokea kipindi cha uchaguzi Mkuu mwishoni mwa mwezi Oktoba 2025.

Akizungumzia utekelezaji wa Nguzo ya Tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama, inayolenga kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama na ushirikishwaji wa wadau, Jaji Mfawidhi alibainisha kuwa Mahakama Kuu Mbeya imeendelea kuwa na ushirikiano mzuri na wadau mbalimbali wa haki, wakiwemo Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, TAKUKURU na taasisi nyingine zinazohusika katika mfumo wa utoaji haki.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Jumanne Abdallah Sagini, amemshukuru Jaji Mfawidhi kwa ziara hiyo na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya Ofisi yake na Mahakama.

Mhe. Sagini amesema ziara hiyo imempa fursa ya kupata taarifa na uelewa zaidi kuhusu baadhi ya changamoto zinazoikabili Mahakama katika Mkoa wa Mbeya na kwamba Ofisi yake iko tayari kushirikiana na Mahakama katika kuzitafutia ufumbuzi.

“Nashukuru kwa ujio wenu na kunifungua macho katika baadhi ya mambo ambayo sikuyafahamu katika mkoa wangu na kunipa mwanga wa namna ya kuyafanyia kazi. Naahidi ushirikiano mkubwa kwa Mahakama na pale uonapo masuala yangu ya kiutawala yanakwamisha utendaji wa shughuli za kimahakama, milango iko wazi, nakukaribisha wakati wowote kuweza kurekebisha hilo,” alisema Mhe. Sagini.

Mkuu wa Mkoa pia ameeleza kuwa Serikali ya Mkoa itafuatilia migogoro na changamoto zilizobainishwa, huku akimuagiza Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Bw. Festo Chonya, kuwasilisha taarifa rasmi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa inayoainisha maeneo yenye changamoto za kiutawala katika Mkoa wa Mbeya, ili kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa katika kuzitatua.

Hatua hiyo imetia msisitizo wa kuendelea kujenga ushirikiano wa karibu, mawasiliano na mahusiano ya kikazi kati ya Mahakama na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, hatua inayotarajiwa kuchangia katika kuondoa vikwazo vya kiutawala na kuweka mazingira bora kwa Mahakama kutekeleza jukumu lake la msingi la utoaji wa haki kwa wananchi.

Viongozi wengine walioambatana na Mhe. Mtulya, katika ziara hiyo ni Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Mhe. Benard Mpepo, Naibu Msajili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Mhe. Zawadi Laizer, Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Bw. Festo Chonya, Afisa Utumishi Mwandamizi wa Mahakama Kuu Mbeya, Bw. Alintula Ngalile na Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi Mhe. Jane Mwaitumile.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Jumanne Abdallah Sagini (kulia) akisalimiana na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (kushoto) alipowasili ofisini kwake jijini Mbeya.
Sehemu ya Viongozi mbalimbali wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya wakifuatilia mazungumzo kati ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Sigini na Jaji Mfawidhi Mhe. Mtulya walipotembelea ofisini kwake 

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Jumanne Abdallah Sagini (wanne kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya walipotembelea ofisini kwake wakiongozwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (wanne kushoto).


Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, Bw. Festo Chonya, (aliyesimama) akijitambulisha kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Jumanne Abdallah Sagini, Kulia ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Benard Mpepo.

Naibu Msajili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Mhe. Zawadi Laizer akijitambulisha Mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Jumanne Abdallah Sagini (hayupo pichani)

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Jumanne Abdallah Sagini akiwa ofisini kwake akiwasikiliza Viongozi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya (hawapo pichani) walipotembelea ofisini kwake.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya, akiwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mbeya. 

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya akitia sahihi kitabu cha wageni wakati alipowasili ofisini ya Mkuu wa Mkoa Mbeya.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni