- Amsisitiza kuzingatia Maadili, Weledi
Na AIDAN
ROBERT,Mahakama-Kigoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile leo tarehe 08 Septemba, 2026, amemuapisha Bw. Machumu Chirya kuwa Muamuzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) wa mkoani humo.
Uapisho wa Muamuzi huyo uliofanyika ofisini kwa Jaji Mfawidhi unamuwezesha rasmi Bw. Chirya, kutekeleza majukumu yake ya kisheria ya uamzi wa migogoro ya kikazi na ajira, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha upatikanaji haki kwa wote mapema ipasavyo ili kupunguza mlundikano wa mashauri ya migogoro ya kazi mkoani humo.
Aidha, Mhe. Rwizile ametumia nafasi hiyo kutoa nasaha kwa Muamuzi huyo, ambapo amemkumbusha kuzingatia misingi ya maadili, weledi wa hali ya juu na kujituma katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku.
Aidha, Jaji Rwizile amemsisitiza Muamuzi huyo kuwa uaminifu na kufuata
sheria kwakuwa ni nguzo kuu katika kutatua migogoro ya kikazi kwa haki, maslahi ya
pande zote mbili (Waajiri na Wafanyakazi) jambo litakalochochea amani na
utulivu mahali pa kazi mkoani Kigoma.
“CMA inaendelea kuwa nguzo
muhimu katika usuluhishi na uamuzi wa migogoro ya kistaarabu na nje ya Mahakama
za kawaida, jambo linalochochea ustawi wa uchumi na usalama mahali pa kazi, tunakutakia
kila la heri katika kutekeleza majukumu yako mapya ya kulijenga Taifa lenye
amani na usawa mahali pa kazi,” amesema Jaji Mfawidhi huyo.
Tukio la Uapisho huo limehudhuriwa na Naibu
Masajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa, Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Yusufu Kasuka pamoja Wasaidizi wa Sheria wa Majaji wa Mahakama Kuu Kigoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (aliyesimama mbele) akimuapisha Bw. Machumu Chirya kuwa Muamuzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA). Aliyesimama kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa na Watumishi wengine wakifuatilia kiapo hicho.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (kushoto) akimkabidhi hati ya kiapo chake Muamzi, Bw. Machumu Chirya mara baada ya kula kiapo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile akitoa neno baada ya kumuapisha Bw. Machumu Chirya kuwa Muamuzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (aliyeketi mbele) akizungumza mara baada ya kumuapisha Muamuzi mpya wa CMA, Bw. Machumu Chirya (wa kwanza kulia).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo, Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (wa tano kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Muamuzi mpya wa CMA , Bw. Machumu Chirya (kulia) aliyeapa leo tarehe 08 Septemba, 2026. Wengine ni Viongozi wengine wa Mahakama Kuu Kigoma walioshuhudia uapisho wa Muamuzi huyo.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni