Jumatano, 23 Septemba 2026

JAJI TIGANGA AWATAKA WATUMISHI WAPYA KUWA WABUNIFU, WAADILIFU

Na ARAPHA RUSHEKE-Mahakama, Dodoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga, amewataka watumishi wapya wa kada ya sheria pamoja na ununuzi kutumia weledi, uadilifu na uelewa mpana wa sheria katika kutekeleza majukumu yao, kwa lengo la kulinda maslahi na rasilimali za Taifa.

Mhe. Tiganga alitoa wito huo Septemba 21, 2026, wakati akifungua Mafunzo Elekezi kwa Watumishi Wapya wa Kada ya Wanasheria pamoja na Ununuzi katika Utumishi wa Umma katika Ukumbi wa Mkutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), yakilenga kuwaandaa watumishi wapya  kufahamu vyema mazingira ya utumishi wa umma, wajibu wao, maadili, nidhamu pamoja na taratibu na mifumo inayowaongoza katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mhe. Tiganga aliwapongeza washiriki kwa kupata nafasi ya kujiunga na utumishi wa umma, akisisitiza kuwa ajira hiyo ni fursa ya kujenga taaluma na wakati huo huo ni dhamana kubwa inayohitaji uadilifu, uwajibikaji, nidhamu na uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu.

“Kuajiriwa kwenu si tu fursa ya kujenga taaluma na kutumikia Taifa, bali pia ni dhamana kubwa inayohitaji uadilifu, uwajibikaji, nidhamu na uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na taratibu za utumishi wa umma,” liesema Mhe. Tiganga.

Aidha, Jaji Mfawidhi alieleza kuwa mafunzo elekezi yana umuhimu mkubwa katika kumsaidia mtumishi mpya kuelewa mazingira ya kazi, wajibu wake, maadili na misingi ya utumishi wa umma, sambamba na kumjengea uwezo wa kutekeleza majukumu kwa ufanisi.

Akizungumzia nafasi ya kada ya sheria katika kulinda maslahi ya Taifa, Mhe. Tiganga aliwataka wanasheria hao kuwa na uelewa mpana unaokwenda zaidi ya taaluma ya sheria, ikiwemo kufahamu mifumo, taratibu na majukumu ya Serikali na utumishi wa umma.

Akinukuu kauli iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali jijini Arusha tarehe 13 Julai 2026, Mhe. Tiganga aliwakumbusha washiriki kuwa kada ya sheria ina nafasi muhimu katika kulinda rasilimali za Taifa.

Mhe. Tiganga alisema wanasheria wanapaswa kutambua kuwa ushauri wao wa kisheria, uandaaji na mapitio ya nyaraka, pamoja na uwakilishi wa Serikali katika mashauri, vinaweza kuwa na mchango mkubwa katika kulinda maslahi ya Serikali na wananchi.

Mbali na Mafunzo Elekezi, washiriki pia walipata mafunzo kuhusu Manunuzi ya Umma na Usimamizi wa Mikataba, pamoja na Ushughulikiaji wa Mashauri ya Nidhamu katika Utumishi wa Umma.

Kwa mujibu wa Mhe. Tiganga, mafunzo hayo ya ziada yatawasaidia washiriki kuongeza uelewa katika maeneo yanayohusisha kwa kiasi kikubwa matumizi na tafsiri ya sheria, hivyo kuwawezesha kutoa ushauri bora wa kisheria na kuchangia katika kulinda maslahi ya taasisi na Serikali kwa ujumla.

Jaji Mfawidhi aliwataka washiriki kuyatumia mafunzo hayo kama mwanzo wa safari ya kujifunza na kujiendeleza kitaaluma, akisisitiza umuhimu wa kujifunza kwa kuendelea kutokana na mabadiliko ya sheria, sera, teknolojia na mahitaji ya jamii.

Mhe. Tiganga pia alitoa shukrani kwa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kuandaa mafunzo hayo, pamoja na wawezeshaji kwa kutumia muda na utaalamu wao katika kuwajengea uwezo watumishi hao wapya.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga, akisistiza jambo wakati alipokuwa anafungua mafunzo kwa watumishi wapya.

Sehemu ya washiriki wakifuatilia kwa umakini mafunzo hayo.

Afisa Sheria Mwandamizi Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Donatus Nungu, ambaye pia ni Mwezeshaji wa Mafunzo hayo akitoa mafunzo hayo kwa washiriki.

Afisa Rasilimali Watu Mwandamizi Ofisi ya Raisi Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi Saada Ibrahim, ambye pia ni Mwezeshaji wa Mafunzo hayo akifafanua jambo wakati wa mafunzo hayo.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Tume ya Utumishi wa Mahakama, ambae pia ni Mwezeshaji wa Mfunzo hayo (wa kwanza kulia), Bi Lydia Churi akifafanua jambo wakati wa mafunzo hayo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo. Aliyekaa kushoto kwake ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe.Upendo Ngitiri na kulia kwake ni Mratibu wa Mafunzi hayo na  Hakimu Mkazi Mwandamizi kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe Husna Rweikiza.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Jamaica.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni