Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Mahakama Kuu ya Tanzania
Masjala Ndogo Kigoma imefanya kikao maalum cha maandalizi (pre-session) kilichoongozwa na Jaji
wa Kanda hiyo, Mhe. John Francis Nkwabi kwa lengo la kuweka mikakati madhubuti
ya kumaliza mashauri nane ya mauaji yaliyopangwa kusikilizwa Wilayani Kasulu mkoani
humo tarehe 21 Septemba, 2026.
Katika kikao hicho kilichofanyika
tarehe 11 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma kiliwaunganisha
wajumbe wa haki jinai kwa njia Mahakama Mtandao (Virtual Court) ambapo Mhe.
Nkwabi aliwakumbusha wadau wote kutimiza wajibu wao kwa uadilifu mkubwa ili
wananchi waweze kuona na kupata haki kwa mapema ipasavyo.
Jaji Nkwabi alisema, hatua
hiyo itasaidia kuimarisha amani na usalama katika jamii, na kueleza kuwa, ratiba
maalum ya usikilizwaji wa mashauri hayo nane imepangwa kwa umakini ili kuzuia
kuahirishwa kwa mashauri bila sababu za msingi.
Naye Naibu Msajili wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa aliwashukuru Wadau
kwa ushiriki wao na ushirikiano mkubwa waliotoa kwa Mahakama ili kuendelea
kutimiza majukumu yake ya kusikiliza mashauri.
Kwa upande wake Mtendaji
wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Bw. Yusufu Kasuka ameahidi juu
ya uwepo wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa ajili ya
kurahisisha usikilizwaji wa mashauri hayo ikiwa ni sambamba na kutoa uwezesho
kwa watumishi na Mawakili upande wa utetezi katika mashauri hayo.
Aidha, Wadau walikubaliana
kuimarisha mawasiliano na ushirikiano wa karibu na Mahakama, Ofisi ya Taifa ya
Mashtaka na upande wa utetezi ili kuhakikisha ushahidi na vielelezo
vinawasilishwa kwa wakati.
Kikao kilisisitiza kuhusu umuhimu
wa kutumia kikamilifu vikao vya maandalizi ili kupunguza muda unaotumika
mahakamani na kuharakisha usikilizwaji wa mashauri ya jinai, hasa ya mauaji.
Kikao hicho kilichowahusisha
Waendesha Mashtaka wa Serikali, Mawakili wa utetezi na Maofisa Magereza na Polisi
kililenga kuondoa vikwazo vyote vya kiutawala na kiufundi vinavyoweza
kuchelewesha mwenendo wa mashauri hayo, na hivyo kuhakikisha haki inatendeka mapema
ipasavyo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. John Nkwabi (katikati) akiongoza kikao cha pamoja na Wadau wa Mahakama Kigoma. Aliyeketi kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa, kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Bw. Yusufu Kasuka, wakifuatilia kwa makini hoja za wadau walizokuwa wakitoa kupitia Mahakama Mtandao wakati wa kikao kilichofanyika tarehe 11 Septemba, 2026.
Wajumbe wa Kikao cha Tathmini ya maandalizi ya kikao cha mashauri ya mauaji waliojiunga kwenye kikao kwa njia ya Mahakama Mtandao wakiwa katika Taasisi zao. Kikao hicho kilifanyika tarehe 11 Septemba, 2026.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi akisikiliza kwa makini Mdau wa Haki Jinai alipokuwa akiwasilisha mchango wake kwenye kikao cha tathmini ya maandalizi ya kikao cha mashauri ya mauaji kilichofanyika tarehe 11 Septemba, 2026.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa akifafanua jambo wakati wa kikao cha tathmini ya maandalizi ya kikao cha mashauri ya mauaji mkoani humo.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Kigoma, Bw. Yusufu Kasuka akifuatilia kwa makini mjadala uliokuwa ukiendelea kwenye kikao cha tathmini ya maandalizi ya kikao cha mashauri ya mauaji.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni