Na ARAPHA RUSHEKE – Mahakama, Dodom
Mahakama
Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Dodoma, tarehe 18 Septemba, 2026 ilifanya kikao
cha pamoja cha maandalizi ya vikao vya
mashauri ya jinai, kwa lengo kuweka mikakati ya kuhakikisha mashauri
yanasikilizwa na kukamilishwa kwa wakati.
Kikao
hicho kiliongozwa na Jaji Mfawidhi, Mhe.
Joachim Tiganga, na kuhudhuriwa na Majaji pamoja na wadau mbalimbali wa
mnyororo wa haki jinai.
Katika
kikao hicho, Naibu Msajili wa Mahakama
Kuu, Mhe Upendo Ngitiri, aliwasilisha taarifa mbalimbali kuhusu hali ya
mashauri ya jinai na maandalizi ya vikao vinavyotarajiwa kuanza mwezi Septemba
na Oktoba 2026. Jumla ya mashauri 35 kutoka Dodoma, Bahi, Kongwa, Chemba,
Mpwapwa, Singida, Iramba na Manyoni yamepangwa kusikilizwa katika vikao hivyo.
Mashauri
hayo yanajumuisha 25 ya mauaji, shauri
moja la kujaribu kuua, mashauri saba ya kuua bila kukusudia pamoja na mashauri
mawili ya usafirishaji haramu wa dawa za kulevya. Aidha, kikao
kilijadili hali ya mashauri 53 ambayo yanasuburi kupangiwa kikao.
Kikao
pia kilijadili hali ya mashauri ya mlundikano ambapo mikakati mbalimbali
ilianishwa. Mashauri yote yanayotarajiwa kufikia hatua ya mlundikano ifikapo
Desemba 2026 yalibainishwa na kuwekwa katika mikakati maalum ya kuhakikisha
yanakamilishwa kwa wakati.
Wadau
walipata fursa ya kuchangia na kujadili changamoto mbalimbali zinazochangia
kuchelewa kwa mashauri, pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na
changamoto hizo.
Miongoni
mwa mikakati iliyojadiliwa ni kuendelea kufanya vikao vya mashauri ya jinai
mara kwa mara, kutumia vikao vya
kuondosha mashauri, kuimarisha ushirikiano kati ya Mahakama na wadau wa
mnyororo wa haki jinai pamoja na kutumia Mahakama Mtandao katika kuharakisha usikilizaji wa mashauri,
hususan rufaa na maombi ya jinai.
Aidha,
maandalizi ya vikao hivyo yamehusisha usambazaji wa ratiba za vikao kwa wadau,
maandalizi na usambazaji wa hati za wito kwa mashahidi na washtakiwa pamoja na
kuwapatia Mawakili wa Kujitegemea nyaraka zinazohusiana na mashauri.
Akihitimisha
kikao hicho, Jaji Mfawidhi alisisitiza umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa
wadau katika kuhakikisha mashauri yanasikilizwa na kukamilishwa kwa wakati, ili
kuendelea kuimarisha utoaji wa haki kwa wananchi.
Kikao hicho kliefanyika ikiwa ni sehemu ya juhudi za Mahakama Kuu Dodoma za kuimarisha usimamizi wa mwenendo wa mashauri, kupunguza na kuzuia mlundikano na kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati.
Meza Kuu ikiongozwa Mwenyekiti wa Kikao hicho ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe.Joachim Tiganga (aliyekaa katikati). Kushoto kwake ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Biswalo Mganga na kulia kwake ni Jaji wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe Suleiman Hassan wakati wa kikao hicho.
Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Upendo Ngitiri, wakati akiwasilisha
taarifa yake wakati wa kikao hicho.
Sehemu
ya wajumbe wa kikao hicho wakiendelea na kikao.
Meza Kuu ikiongozwa Mwenyekiti wa Kikao hicho ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, Mhe.Joachim Tiganga (aliyekaa katikati). Ikiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kikao hicho waliohudhuria wakati wa kikao hicho.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Jamaica.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni