Jumanne, 22 Septemba 2026

MAHAKAMA KUU MBEYA YATEMBELEA GEREZA KUU RUANDA

Na MUKSINI NAKUVAMBA – Mahakama, Mbeya

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya amefanya ziara ya kutembelea Gereza Kuu Ruanda jijini Mbeya hivi karibuni kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali zinazoendelea gerezani pamoja na kusikiliza changamoto za wafungwa na mahabusu.

Akiwasilisha taarifa ya Gereza, Mkuu wa Gereza Ruanda Mbeya Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Christopher Fungo, alieleza hali za wafungwa na mahabusu waliopo gerezani, ambapo kwa sasa kuna jumla ya Wafungwa 693 na Mahabusu 204. ACP Fungo alieleza changamoto mbalimbali zinazolikabili Gereza hilo.

“Mhe. Jaji mfawidhi, Gereza letu linakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo wafungwa kutokupata Vitabu vya Kumbukumbu za Rufaa kwa wakati hasa kwa wafungwa kutoka Masjala za Iringa, Sumbawanga na Mbeya pia Mahabusu kusubiri muda mrefu wito wa Mahakama suala linalopelekea kuwa na mlundikano mkubwa wa mahabusu Gerezani,” alisema ACP Fungo.

Taarifa hiyo ilihitimishwa kwa kumuomba Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Mtulya kuongeza ushirikiano na vyombo vingine vya haki jinai ili kukamilisha upelelezi wa kesi kwa wakati ili kukabiliana na changamoto ya msongamano wa mahabusu gerezani.

Aidha, Naibu Msajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Bernard Mpepo alieleza kuwa Kitengo cha Mahakama ya Rufani kilichopo Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya wamekuja na Vitabu ili kuwapatia wale ambao walikuwa na changamoto ya kutokupata vitabu kwa wakati.

Sambamba na hilo Mhe. Mpepo alieleza kuwa, Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya inatarajia kuendesha Vikao Vitatu vya Mashauri ya Jinai, kwa upande wa mashauri ya Mauaji kwa pamoja kuanzia tarehe 5 Oktoba, 2026, hivyo kwa wale ambao walikuwa wanasubiri wito wa kuitwa mahakamani Mashauri yao yataanza kusikilizwa.

Mhe. Mtulya alifanya ukaguzi gerezani kwa kutembelea sehemu za kulala wafungwa na mahabusu, zahanati, jikoni na sehemu ya kugawia chakula wafungwa na mahabusu. Katika ziara hiyo Mhe. Mtulya alikutana na Wafungwa na Mahabusu ambao waliwasilisha changamoto zao kwa Mahakama na Wadau wengine alioambatana nao. 

Katika risala iliyosomwa na wafungwa na mahabusu walieleza changamoto zao zinazowakabili na mapendekezo yao. Sehemu ya Risala yao inaeleza kuwa,

“Tunaomba idadi ya mashauri yanayosikilizwa kuongezwa ili kuturahisishia kupata haki zetu kwa wakati. Pia tunaomba wakati wa kupanga vikao vya mashauri ya Mahakama ya Rufani kuwe na ushirikishwaji wa Naibu Msajili na Mkuu wa Gereza ili kutoa kipaumbele kwa watuhumiwa waliokaa muda mrefu gerezani.”

Mhe. Mtulya vilevile, alitoa fursa kwa Wafungwa na Mahabusu wenye shida binafsi kwake, kwa Naibu Msajili na wadau wengine wa haki jinai alioambatana nao kuonana nao kwa utaratibu uliowekwa na waliweza kusikilizwa shida zao.

Vilevile, Mhe. Mtulya alitembelea Gereza Kuu Ruanda upande wa Wanawake ambapo kwa upande huo pia alipokea Risala ya Wafungwa na Mahabusu Wanawake ambapo nao waliwasilisha changamoto zao.

Aidha, Mhe. Mtulya alihitimisha kwa kutoa shukrani kwa Uongozi wa Gereza, Wafungwa na Mahabusu wa Gereza la Ruanda. “Nawashukuru kuwa pamoja nasi kuwasikiliza hoja zenu, tumezichukua na tutazifanyia kazi,” alisema Mhe. Mtulya.

Kwa upande wake Mkuu wa Gereza ACP Fungo alitoa shukurani zake kwa ujio wa ugeni huo, kwa kuwa umekuwa na tija kubwa kwao kwa kutoa fursa kadhaa ikiwemo kulipia gharama za matibabu kwa wagonjwa, kuwapatia matunda wafungwa na mahabusu na kushughulikia suala la kupunguza mlundikano wa mahabusu Gerezani.

Katika ziara hiyo Mhe. Mtulya aliambatana na Naibu Msajili Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Bernad Mpepo, Kaimu Mtendaji Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Mbeya Bw. Alintula Ngalile, Naibu Msajili Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Zawadi Laizer, Mahakimu, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), TAKUKURU, Mwenyekiti TLS Chapta ya Mbeya, Afisa huduma kwa Jamii na wadau wengine wa Haki jinai.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (mwenye suti ya buluu katikati), na viongozi wengine alioambatana nao katika ziara hiyo wakiwa kwenye picha ya pamoja na Uongozi wa Gereza Kuu Ruanda Mbeya, Wengine ni Mkuu wa Gereza Ruanda ACP Christopher Fungo (wa saba kuhoto), Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Mbeya Mhe. Benard Mpepo (wa sita kushoto), Kaimu Mkuu wa Gereza Ruanda ACP Grace Mbedule na Naibu Msajili Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mhe. Zawadi Laizer (wa sita kulia)

Viongozi mbalimbali wa Mahakama Masjala Ndogo ya Mbeya na wadau walioambatana na Mhe. Fahamu Mtulya (hayupo pichani), wakizunguka maeneo mbalimbali ya Gereza la Ruanda.

Viongozi mbalimbali wa Mahakama Masjala Ndogo ya Mbeya na wadau walioambatana na Mhe. Fahamu Mtulya (hayupo pichani), wakizunguka maeneo mbalimbali ya Gereza la Ruanda.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (kulia), akizunguka kufanya ukaguzi wa maeneo mbalimbali ya Gereza Ruanda, akiwa na mwenyeji wake Mkuu wa Gereza ACP. Christopher Fungo.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya Mhe. Fahamu Mtulya (kushoto) akipokelewa na Uongozi wa Gereza kuu Ruanda Mbeya wakiongozwa na Mkuu wa Gereza Kamishna Msaidizi wa Magereza, (ACP) Christopher Fungo.

(Habari Hii imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni