Jumanne, 22 Septemba 2026

WADAU WA HAKI JINAI WAKUTANA KWENYE KIKAO CHA KUSUKUMA MASHAURI YA JINAI

Na IMAN MZUMBWE –Mahakama, Songwe

Mahakama Kuu Tanzania Masjala Ndogo Songwe imefanya kikao cha kusukuma mashauri ya jinai (Case flow Management) kilichofanyika hivi karibuni katika Ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe.

Lengo la kikao hicho ilikuwa ni kufuatilia mwenendo wa mashauri yaliyopo mahakamani, kubaini changamoto zinazokwamisha uendeshwaji wake na kuweka mikakati ya kuahakikisha haki inapatikana kwa wakati.

Kikao hicho kiliongozwa na Naibu Msajili Mahakama Kuu Tanzania Masjala Ndogo Songwe Mhe. Joyce Minde, Mahakimu kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, Mahakama ya Wilaya Mbozi wakiongozwa na Mhe. Francis Kishenyi. 

Pamoja wadau wengine wa haki jinai wakiwemo  Ofisi ya Mashtaka Taifa Mkoa wa Songwe, TAKUKURU, Uhamiaji, Ustawi wa jamii, Jeshi la Magereza, Jeshi la Polisi, Huduma kwa jamii, Mawakili wa Kujitegemea pamoja na Ofisi ya Upelelezi Mkoa wa Songwe.

Aidha, kikao hicho kilipitia kwa pamoja utekelezaji wa maadhimio ya vikao vilivyopita katika Mahakama ya Wilaya Mbozi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe na Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songwe ikiwemo utekelezaji wa maadhimio kuwa madaktari wapewe mafunzo ya ndani kwa ajili ya kujifunza namna bora ya kujaza PF.3, Upelelezi wa mashauri ufanyike kwa wakati ili kupunguza mlundikano wa Mashauri mahakamani.

Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na hali ya mashauri ya jinai yakiwepo mashauri ya watoto na mashauri yanayotarajiwa kuingia kwenye mstari wa mlundikano ifikapo mwezi Disemba 2026.

Aidha, wadau wa haki jinai waliipongeza Mahakama kwa kazi nzuri wanayoifanya ikiwemo kuhakikisha mashauri yanasikilizwa kwa wakati na haki inatendeka kwani imepelekea kutokuwepo kwa mlundikano mashauri mahakamani na malalamiko kutoka kwa wananchi.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Songwe Mhe. Francis Kishenyi alisisitiza na kuwaomba Ofisi ya Upelelezi Mkoa wa Songwe kuzingatia suala la umri kwa washtakiwa  kwani kumekuwa na malalamiko juu umri kwa baadhi ya washtakiwa wa makosa ya  jinai wakati wanapofikishwa mahakamani na kuonekana kuwa mashauri mengine yalisitahili kuwa mashauri ya watoto.

Naibu Msajili Mhe. Joyce Minde alisisitiza uwepo wa ushirikiano wa Taasisi zote za haki jinai kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao ili kurahisha upatikana wa haki kwa wakati  kwa pande zote mbili ya jamhuri na washtakiwa.

Naye, mwakilishi wa Magereza Inspector Ally Saidi Chiutila alipendekeza kuwa wafungwa walio tayari kukiri makosa yao wasikilizwe kwa wakati ili kurahisisha mwenendo wa mashauri yao.

Mawakili wa Serikali kutoka katika Ofisi ya mwendesha mashtaka Mkoa Songwe waliaahidi kutekeleza maalekezo na mapendekezo yaliyotolewa katika kikao hicho.

Kikao hicho cha kusukuma mashauri ya jinai ni sehemu ya jitihada za Mahakama na wadau wa mfumo wa haki jinai katika kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kwa kuazingatia misingi ya haki, usawa, weledi na utawala wa sharia.

Mwenyetiki wa Kikao hicho cha kusukuma Mashauri ya Jinai Mkoa wa Songwe ambaye pia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Joyce Minde (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa haki jinai.

Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Mbozi Mhe. Nemes Chami akitoa taarifa ya Mahakama ya Wilaya ya Mbozi.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe Mhe. Francis kishenyi akitoa taarifa ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe.

Mdau wa haki Jinai kutoka Jeshi la Magereza Insepector Ally Saidi Chiutila akitoa hoja na mapendezo mbele ya kikao hicho.

Sehemu ya wadau wa mfumo wa haki jinai Mkoa wa Songwe wakimsikiliza na mkumfatilia kwa karibu Mwenyekiti wa kikao hicho Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Joyce Minde (hayupo pichani).

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Songwe Mhe. Joyce Minde wa (kwanza kulia) ambaye ni Mwenyekiti wa kikao akizungumza na wadau wa haki jinai katika kikao hicho na kwanza kushoto ni Katibu wa kikao Bw. Elibariki Charles Mpinga ambaye pia ni Wakili Serikali.

(Habari Hii Imehaririwa Innocent Kansha - Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni